Ashura Jumapili, Timesmajira online, Bukoba
Wadau wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), wamesema upatikanaji wa mafuta umekuwa na changamoto hasa maeneo ya Wilaya za mipakani zinazopakana na nchi jirani.
Hivyo wameiomba EWURA kuongeza suala la utoaji elimu kwa kushirikiana na maofisa biashara,wakurugenzi na wananchi ili kuondokana na changamoto hiyo.
Hayo yameelezwa katika semina ya wadau wa mamlaka hiyo iliyofanyika Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba mkoani kagera iliyowahusisha Maofisa Biashara wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Uwekezaji,Biashara na Viwanda Wilaya ya Ngara mkoani Kagera Privanus Katigira,amesema suala la mafuta ni changamoto kwa Wilaya za mipakani kwa sababu vichochoro ni vingi.
Huku akibainisha kuwa kuna wakati EWURA walipeleka mafuta Ngara usiku lakini asubuhi Wilaya hiyo haikuwa mafuta kabisa.
“Naomba EWURA muongeze elimu kwa kushirikiana na maofisa biashara,wakurugenzi na wananchi kwa sababu madhara yanayopatikana ni makubwa hivi karibuni eneo la Rusumo wa 4 familia moja waliuawa kwa sababu ya kutunza mafuta ndani ya nyumba,”amedai Katigira na kuongeza kuwa;
“Kutorosha mafuta nchini ni kudororesha uchumi sababu mafuta yetu yanaenda nje ya nchi bila kufuata taratibu,”.
Pia amesema elimu walioyoipata itawasadia kushirikiana na EWURA kudhibiti mambo yanayohusu huduma za nishati na maji badala ya kubaki kufuatilia leseni za halmashauri tu kwa sababu sheria inawataka na wao kufanya hivyo.
Ofisa Biashara kutoka Wilaya ya Kyerwa Mathew Nyarufunjo ,amesema maeneo ya mipakani yanachangamoto kubwa ya kupata huduma za mafuta kwa wakati hasa eneo lake.
Nyarufunjo amesema eneo la Kyerwa hata wawekezaji wanashingwa kujenga vituo vya mafuta kutokana na miundombinu ya barabara kuwa mibovu hivyo kutowavutiwa.
Amesema kutokana na changamoto hiyo baadhi ya wafanyabiashara wanaamua kutumia pikipiki kufuata mafuta vituoni na kwenda kuyauza kwa bei kubwa ili na wao wapate faida wakati mwingine uuza kwa bei kubwa zaidi.
Meneja Ewura Kanda ya Ziwa George Mhina,
amesema wanadhibiti ubora, usalama na tija ya watoa huduma katika sekta za nishati na maji,kutathimini na kupitisha marekebisho ya huduma ikiwa ni pamoja na tozo.
Amesema wanasikiliza malalamiko na kutatua migogoro, kuelimisha umma kuhusu shughuli za udhibiti wa huduma za nishati na maji.
Huku nyenzo wanazotumia kudhibiti upande wa mafuta ni sera ya Nishati na Maji, sheria ya Ewura sura ya 414 ya sheria za Tanzania, sheria ya Mafuta ya mwaka 2015 ( sura ya 392 ),sheria ya Umeme na sheria ya maji safi na usafi wa mazingira na kanuni zinazoandaliwa na Waziri wa sekta husika.
Amasema pia wamepata mafanikio kama uagizaji wa mafuta wa pamoja,kupungua kwa uchakachuaji wa mafuta,urahisishwaji wa ujenzi wa vituo,uzingatiaji wa sheria kwa watoa huduma umeimarika na kuongeza uwekezaji wa vituo vijijini.
“Kuna changamoto ya uuzaji wa mafuta kwenye madumu,kukosekana kwa elimu kwa baadhi ya wadau,uwekezaji mdogo wa vituo vya mafuta kwenye maeneo ya vijijni,rasilimali na ukubwa wa nchi,”ameeleza Mhina.
Awali Kaimu Mkuu kuu wa Mkoa wa Kagera Erasto Siima,amesema wanatakiwa kuhamasisha uwekezaji shirikishi katika maendeleo ya kisekta na kujenga miundombinu.
Huku mdhibiti anawajibu wa kusimamia huduma katika sekta ya Nishati na Maji kwa njia ya uwazi na kuchochea uwekezaji endelevu kwa kuzingatia sheria,kanuni na taratibu zenye kuongeza tija na kuleta nafuu kwa pande zote zinazohusika.
Amesema pamoja na shughuli za Ewura kudhibti wanatakiwa kuhakikisha mafuta yanapatikana kwa bei sahihi ili bidhaa hiyo iendelee kutoa mchango katika ustawi wa uchumi wa nchi na kutovunja shughuli za kiuchumi.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu