Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza
Wadau na wamiliki wa mabwawa nchini Tanzania,wametakiwa kuzingatia miongozo,mipango pamoja na kufanya ufuatiliaji na tathimini ya hali ya mabwawa muda wote.
Ambapo kwa sasa nchini Tanzania kuna takribani mabwawa 700 maeneo mbalimbali pamoja na mabwawa ya taka sumu takribani 60 huku tathimini ya hali ya usalama kwa sasa ikionesha kuwa mabwawa hayo yapo vizuri hayana viatashiri.

Wito huo umetolewa Novemba 19,2025 na Mkurugenzi wa Huduma za Ubora wa Maji kutoka Wizara ya Maji,Mteki Chisute,wakati akifungua mkutano wa mwaka wa usalama wa mabwawa unaofanyika kwa siku tatu mkoani Mwanza.
Chisute amesema,endapo taasisi mbalimbali na watu binafsi watazingatia miongozo na kuweza kuaanda mipango ambayo itawezesha kukabiliana na hatari mbalimbali ambazo zinaweza kujitokeza katika mabwawa itasaidia kuchukua hatua kwa haraka na nchi kubaki salama.
“Kwa maana unapofanya tathimini ni rahisi kugundua kama kuna kihatarishi chochote juu ya usalama wa mabwawa na kuchukua hatua za kuzuia hatari hiyo.Hivyo pamoja na faida za mabwawa wadau mbalimbali na wamiliki mnapaswa kuhakikisha mnaweka mipango mahususi ya kuhakikisha hakuna kihatarishi chochote kinachoweza kuhatarisha usalama wa mabwawa yetu,”amesema Chisute.
Sanjari na hayo Chisute, amesema Serikali imefanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha inatumia teknolojia mpya kwa ajili ya uimara wa mabwawa na kuhakikisha yanadumu kwa muda mrefu.
Ambapo imeweza kununua mitambo mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha mradi wa uchimbaji wa mabwawa na ujenzi wake pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu na wamiliki ili waweze kufanya usimamizi.
“Baada ya kupata mitambo katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu kuna mabwawa yamejengwa kwa ukubwa tofauti yakiwemo mamkubwa,ya kati na madogo,hiyo yote ni kuwa na mabwawa mengi,kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji na kuhifadhi taka sumu ili isije kuingia kwenye mazingira na kuleta athari,”amesema Chisute.

Kwa upande wake,Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wachimbaji Tanzania(Tanzania Chamber of Mines), Mhandisi Benjamin Mchwanpaka,amesema, kila mradi unapoanza lazima wafuate taratibu za kutathimini athari za mazingira na kuweka mpango wa kuhakikisha bwawa la maji au sumu linakuwa limekidhi vigezo na kufuata vibali vyote kutoka taasisi zinazohusika ikiwemo idara ya maji na Tume ya Madini.
“Wakaguzi hutembelea migodi mara kwa mara ili kuhakikisha mabwawa ya kuhifadhia taka yanadhibitiwa ipasavyo,endapo kutatokea tatizo la nyufa au dalili zozote za hatari mifumo ya ufuatiliaji inatambua mapema ili hatua za haraka zichukuliwe na kulinda watu,mali na mazingira dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na taka zinazohifadhiwa kwenye mabwawa hayo,”amesema Mhandisi Mchwanpaka.
Amesema hakuna mgodi unaoruhusiwa kutiritisha maji yenye kemikali au taka kwani ni uchafuzi wa mazingira na kufanya hivyo ni kinyume na Sheria.Hivyo wanaendelea kuhamasisha migodi kufuata Sheria za nchi na mamlaka husika kusimamia utekekalezaji wake.

Naye Meneja wa Ufungaji wa Mgodi(Mine Closeru Manager) wa Mgodi wa Barrick-Buzwagi Gold Mine,Zonnastaal Mumbi,amesema mgodi huo umeweka nguvu kuhakikisha usalama wa mabwawa katika maeneo ambayo wanafanya kazi kwa kulinda wafanyakazi na jamii inayowazunguka.
Ambapo wanavyanzo vya kukusanya na kuhifadhi maji ili yasiharibu mazingira pia wanayo mifumo kwenye mabwawa hayo inayotoa taarifa ya kiwango cha maji kinachotokea na ubora wake ili kuhakikisha hayaendi kuleta madhara katika mazingira.
Haya hivyo Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira kutoka NEMC,Dkt.Menan Jangu,amesema kuna aina mbili za mabwawa moja ni yakutunzia maji na mengine ni ya kutunzia taka sumu kwenye migodi.
Hivyo ametaadharisha kuwa endapo mabwawa hayo hatayazingatia taratibu zilizopo yatasababisha athari kwa jamii na mazingira.
“Bwawa la maji kama halikujengwa kwa kuzingatia taratibu zilizopo likibomoka maeneo yaliyo chini yataathirika ikiwemo makazi na watu kutapoteza maisha.Pia mabwawa ya kutunzia tope sumu kama kwenye migodi mifumo yake isipokuwa sawa,sumu itaenda kwenye vyanzo vya maji na mashamba na kuleta athari,”amesema.



More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina