November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wa maji Lushoto wataka wananchi wasiharibu mazingira

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto

Baadhi ya wadau wa maji Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wamesema dhamira ya Serikali ni kumtua mama ndoo kichwani, huenda isiweze kutimia kwenye Tarafa ya Mlalo kutokana na baadhi ya wananchi kuharibu mazingira kwa kulima kwenye moyo na vyanzo vya maji.

Wameyasema hayo kwenye mkutano wa Wadau wa Maji na Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO’s) Tarafa ya Mlalo na Mlola Kata ya Ngwelo kwa uratibu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Lushoto, kwa ajili ya kuunganisha vyombo hivyo ili viweze kuleta tija kwa jamii.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga (katikati) akizungumza kwenye Mkutano wa Wadau wa Maji Tarafa ya Mlalo.

“Serikali inafanya jitihada za kumtua mwanamke ndoo kichwani, lakini kwa Tarafa ya Mlalo jambo hilo linaweza kushindikana kwa sababu ya uharibifu wa mazingira,kipaumbele cha kwanza cha maji ni kunywa binadamu siyo kunyweshea mashamba,”amesema Diwani wa Kata ya Mlalo Rashid Rajab maarufu Madagaa.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga amesema wanaunganisha vyombo vya watoa huduma ya maji ili kuleta ufanisi na nguvu za kiutendaji.

Hivyo wameamua kuviunganisha vyombo kwa ngazi ya Tarafa na kutakuwa na vyombo vya watumia maji (CBWSO’s) saba kwenye Wilaya ya Lushoto kikiwemo cha Mlalo Wasso.

Mwenyekiti wa Bodi ya Maji Mlalo Wasso, Waziri Ngereza akizungumza na wadau wa maji mara baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti kwa miaka mitatu.

Mratibu wa CBWSO’s Mkoa wa Tanga Hans Mwiyola amesema viongozi wa vijiji na wadau wengine wa maji wana wajibu wa kuwahimiza wananchi kulipia maji ili kuwezesha Bodi za Maji ziweze kujiendesha na kuweza kufanyia ukarabati miradi ya maji huku akihimiza fedha zinazopatikana zipelekwe benki.

Mratibu wa CBWSO’s Mkoa wa Tanga Hans Mwiyola akitoa mada kwenye Mkutano wa Wadau wa Maji Tarafa ya Mlalo.

Katika mkutano huo ambao ulikwenda sambamba na uchaguzi wa viongozi wa Bodi ya Maji ya Mlalo Wasso, ambapo Waziri Ngereza alichaguliwa kuwa Mwenyekiti na kuahidi kupeleka maji kwenye vijiji vyenye shida ya maji ikiwemo Majulai kilichopo Kata ya Mwangoi.

Wadau wa Maji Tarafa ya Mlalo wilayani Lushoto wakiwa kwenye kikao.