November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wa kilimo wapongeza hotuba ya Samia kuhusu TADB

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Dar

WADAU katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi wamepongeza hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan iliyoelezea mpango wa Serikali ya kuiongezea fedha Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili iweze kutoa mikopo mingi zaidi kwa riba nafuu, sambamba na kuchangia ukuaji na maendeleo ya sekta hizo pamoja na viwanda.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau nchini wameelezea matumaini yao makubwa kuwa TADB ikiwezeshwa zaidi, mchango wake katika maendeleo na ukuaji kwa sekta husika utaongezeka mara dufu ikiwemo kuimarisha ujenzi wa uchumi wa viwanda hapa nchini.

Mkulima wa soya na mahindi katika Wilaya ya Songea Vijijini, Christian Ngatunga, mbali na kupongeza hotuba hiyo, amesema mpango wa kuongezea nguvu TADB ufanyike mapema ili msimu ujao wa kilimo uweze kuwanufaisha wakulima wengi.

“Hatua hii inaonesha dhamira ya kweli ya Serikali ya kuendeleza na kuinua sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi ambapo TADB imekuwa ikitoa mikopo kwa zaidi ya miaka mitano sasa, hivyo ikiongezewa fedha itaweza kuchochea ukuaji wa kilimo na uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata mazao,” amesema Ngatunga.

Amesema tija ya kuongeza uzalishaji wa mazao unategemea na uwekezaji mkubwa kwenye maandalizi ya shamba na matumizi ya zana bora za kilimo, hivyo wakulima wakiwezeshwa mikopo kupitia TADB, kutakuwa na mapinduzi ya kilimo nchini na kuchangia sehemu kubwa katika pato la taifa.

Zao la kahawa

Akihutubia Bunge kwa mara ya kwanza, Rais Hassan aliwaeleza Watanzania kupitia Bunge kuwa serikali ya awamu ya sita imekusudia kuongeza fedha katika benki ya TADB ili iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Rais Hassan alieleza kuwa kilimo kinachangia asilimia 100 ya chakula nchini, asilimia 60 ya malighafi za viwandani, asilimia 27.7 ya pato la Taifa, na asilimia 25 ya fedha za kigeni, huku changamoto kubwa ikiwa katika upatikanaji wa mitaji , mbegu bora, hivyo nguvu kubwa itaelekezwa kwenye tafiti za mbegu bora, na kuwekeza zaidi TADB ili iweze kutoa mikopo yenye riba nafuu zaidi kwa wakulima, wavuvi na wafugaji..

Joel Elinasha, mkulima wa shayiri kutoka Kiteto mkoani Manyara, ameeleza kufarijika na hotuba ya Rais Hassan kwani imejaa maono makubwa hususani katika swala la utafiti wa mbegu bora ambao utawezesha kuongezeka uzalishaji wa mazao.

“Nguvu kubwa iwekezwe kwenye tafiti za mbegu, mbolea na afya ya udongo jambo litakalosaidia kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao nchini, kadhalika na kuiwezesha kifedha benki ya TADB ili iweze kuwafikia wananchi wengi kwa mikopo,” amesema, Elinasha.

Naye, Benson Shija mfugaji kutoka Bariadi, mkoani Simiyu alisema yupo tayari kujifunza njia bora ya ufugaji wa kisasa na kuachana na ufugaji wa kuhamahama kama alivyoeleza Rais Hassan katika hotuba yake, lengo ni kuifanya sekta ya ufugaji kukua na kuchangia sehemu kubwa katika pato la taifa.

“Tumekuwa na changamoto ya mbegu bora za mifugo hali inayotufanya kuwa na mifugo mingi pasipo kuwa na tija, hivyo kupitia njia za kisasa za ufugaji tutaweza kunufaika na shughuli hii,” amesema Shija.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine alimshukuru Rais Hassan kwa kutambua mchango wa TADB katika ukuaji wa sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi, huku akisisitiza kwamba benki hiyo itaendelea kutoa mchango mkubwa katika sekta hizo ili kuweza kuwanufaisha wakulima wengi zaidi.

“Mpaka Desemba 2020, TADB imekwisha nufaisha wakulima 1,788,202 na kutoa mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 300 katika mikoa 26 ya Tanzania Bara na Zanzibar. Mikopo hii imewezesha kukua kwa minyororo ya thamani kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi,” amesema Justine.

“Hivyo, hotuba ya Rais Hassan imetuongezea nguvu zaidi, na sisi kama benki tunaahidi kwamba tutaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuweza kufikia dira ya Rais katika eneo la kilimo, ufugaji na uvuvi kama aliyoelezea kupitia hotuba yake,” amesema Justine.