Na Mwandishi wetu, timesmajira
MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Jaji Mshibe Ali Bakari ameipongeza TMA kwa kuendelea kushirikisha sekta mbalimbali nchini katika shughuli za utoaji wa huduma za hali ya hewa.
Alibainisha hayo wakati akifungua rasmi Mkutano wa 24 wa Wadau wa Utabiri wa msimu wa mvua za Masika (Machi hadi Mei), 2024 uliofanyika katika ukumbi wa PSSSF, Dodoma, Tarehe 19/2/2024.
“Tunapoelekea kutoa utabiri wa mvua za Masika 2024, lengo kuu la kukutana hapa ni kuwezesha matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kwa wote na kwa wakati, ninapenda kuipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa kuendelea kushirikisha wadau mbalimbali katika shughuli zao za utoaji wa huduma za hali ya hewa ambazo ni pamoja na utabiri wa misimu ya mvua. Ushirikiano huu ni mfano wa kuigwa na unafaa kuendelea hasa katika kipindi hiki ambapo dunia pamoja na nchi yetu inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa”. Amesema na kuongeza.
“Tunapojiandaa kupokea taarifa ya utabiri wa Masika, Machi hadi Mei, 2024 ni muhimu sana kila mmoja wetu kuwa na jukumu la kufuatilia kwa karibu, kuelewa, kupanga na kukabiliana na hali ya hewa inayotarajiwa katika sekta yake”. Amesema Jaji Mshibe Bakari.
Awali, Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri TMA, Dkt. Hamza Kabelwa amesema “Mkutano huo ni mwendelezo wa sehemu ya ushirikishwaji wadau hususan wataalamu kutoka sekta mbalimbali katika kuandaa taarifa zinazolenga kuchochea matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa.
Katika mkutano huo walikuwa na majadiliano ambayo ni muhimu katika kuendeleza na kuimarisha utoaji wa huduma za hali ya hewa na matumizi yake kwa jamii.
Mkutano huu ni muhimu sana kwa wadau wa hali ya hewa katika kujifunza na kuongeza uelewa kuhusu matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa katika sekta zao”.
Naye Mwakilishi kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (World Food Programme – WFP) Sasha Guyetsky, ambaye pia ni Mkuu wa Utafiti, Tathmini na Ufuatiliaji, WFP Tanzania, ameishukuru TMA kwa ushirikiano wanaoendelea kutoa kwa WFP pamoja na wadau wengine nchini.
Aidha, ameeleza kuwa hivi karibuni TMA na WFP wamesaini ushirikiano wa miaka mitano wa kiutendaji ili kuweza kuimarisha utoaji huduma za hali ya hewa wenye kuleta tija.
Mmoja wa wadau kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Consolata Mbanga alieleza namna taarifa za awali za msimu wa mvua za Vuli, 2023 zilivyosaidia katika kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo pamoja na kuandaa mpango Taifa wa dharura kwa mikoa iliyotarajiwa kuathirika kutokana na hali ya El Niño.
Katika mkutano huu, wadau walipata fursa ya kuona utabiri wa hali ya hewa katika kipindi cha mwezi Machi hadi Mei, 2024 na kutoa michango yao juu ya athari zinazotarajiwa katika sekta husika pamoja na ushauri ili kuwezesha kuandaa mbinu na mipango ya kukabiliana na athari hizo.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi