Na Mwandishi wetu Timesmajira online
MASHIRIKA yanayotetea haki za watoto nchini yameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa mabadiliko ya vifungu vya sheria ya ndoa vinavyomruhusu mtoto wa kike kuolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18.
Ombi hilo limetolewa jijini Dar-es-Salaam wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambayo huadhimishwa kila ifikapo June 16 kwa ajili ya kuwakumbuka watoto waliouwawa na Serikali Soweto mwaka 1976 wakiwa katika maandamano ya kudai haki zao.
Wamesema ni wakati sasa Serikali kutambua kuwa ili mtoto wa Afrika aweze kufika mahali na kutambulika ni vizuri sheria na miongozo ikampa nafasi na fursa ya kufikia malengo.
Akizungumza na waandishi wa habari Mwakilishi kutoka Shirika lisilo la Kiserikali lililoazishwa ili kukuza na kulinda haki za watoto nchini(C-Sema)Jane Haule amesema inapaswa kufika wakati Serikali kusikia kilio cha wadau hao kwa kubadilisha sheria ya mwaka 1971 kifungu cha 13 ambacho kinasema mtoto wa kike anaweza kuolewa akiwa na miaka 15.
Amesema wanaharakati hao wamekuwa wakipaza sauti kupinga vitendo vya ukatili kwa watoto na kupinga muendelezo wa ucheleweshwaji wa mabadiliko ya vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya ndoa vinavyomruhusu mtoto wa kike kuolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18.
“Tunatamani kuona inafika mahala wabunge wetu wanafikia hatua ya kubadilisha sheria kwasababu mahakama tayari ilishaamua na kuona inafika tamati ili mtoto wa kike aweze kufika umri sahihi wa kuolewa,”amesisitiza
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Jukwaa la Utu wa Mtoto(CDF) Alice Mtuga amesema suala la mabadiliko ya sheria ya ndoa imekuwa ni kilio cha mda mrefu hivyo ameiomba serikali kufuatilia suala hili na kuhakikisha mchakato wa ubadilishaji wa sheria ndoa unapewa kipaumbele.
“Tunaiomba Serikali yetu sikivu ifuatilie suala hili kwa ukaribu ili iweze kufikia hatma ya kupata sheria ambayo itaweza kuimarisha ulinzi wa mtoto na jamii ya kitanzania”amesema Mtuga.
Naye Mwanafunzi kutoka shule ya Tandika Sekondari Nisele Salvatory amesema ni wakati sasa mtoto wa kike kupewa nafasi kama anavyopewa mtoto wa kiume na kwa pamoja kuwalinda dhidi ya ukatili wa Kijinsia.
“Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 pamoja na sheria ya mwaka 2019 zote kwa pamoja zimekuwa zikipelekea kumuathiri kisaikolojia na kimazingira,”amesema Nisele.
Mwajuma Imma mkazi wa Mabibo alitoa wito kwa jamii kumlinda mtoto wa kike na kupaza sauti juu sheria ya ndoa ili iweze kubadilisha kwa lengo bora la ustawi wa mabinti.
Katika maadhimisho hayo Mashirika nane yalishiriki katika maadhimisho hayo ni Msichana Initiative Organization, Tai Tanzania, C -Sema, Flaviana Matata Foundation, Jukwaa la Utu wa mtoto, Missing Child Tanzania, Tanzania Ending Child Marriage Network, Jamii Forum ambapo kwa pamoja walifanya matembezi ya amani.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa