December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau wa Afya watakiwa kushiriki kongamano la utengamao

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Wadau wa afya na maendeleo wametakiwa kushiriki katika kongamano la pili la  utengamao “Rehabilitation Summit” na kuwa sehemu ya juhudi za kuboresha mfumo wa afya na huduma za utengamao nchini kwani ushiriki wak utawezesha kuwa na majadiliano yenye manufaa kwa jamii nzima.

Wito huo ulitolewa jana Jijini Dar es Salaam,na  Mkurugenzi Mtendaji  wa Asasi ya Rehab Health,  Remla Shirima wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu ujio wa kongamano hilo ambalo  limeenda  sambamba na kaulimbiu isemayo “Kuendeleza Ajenda ya Utengamao: Kuimarisha Mifumo ya Afya nchini Tanzania.” linalotarajiwa  kuanzia tarehe 18 hadi 20 Septemba 2024 katika ukumbi wa JNICC. 

Pi alisema Kongamano hilo ambalo litazinduliwa Rasmi na Waziri was Afya Jenista Mhagama lina lengo la kuwakutanisha wataalam, watoa huduma za afya, watunga sera, na washirika mbalimbali ili kujadili mikakati ya kuendeleza huduma za utengamao chini Tanzania 

“Tunalenga kuimarisha mfumo wa afya kwa kuhakikisha huduma za utengamao zinafika katika ngazi za
msingi za huduma za afya na jamii. Pia, tunataka kubadilishana maarifa kuhusu utafiti wa hivi karibuni, uvumbuzi, na mbinu bora za kuboresha huduma za utengamao kwa wagonjwa.”


Aidha alisema wanatarajia kupata ushiriki wa wazungumzaji kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwemo watunga sera, wataalamu wa afya, wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, na wataalamu wa sekta ya afya.

Pia alisema wamejumuisha wawakilishi kutoka wizara husika, ikiwemo Wizara ya Afya, pamoja na wadau wengine kutoka sekta mbalimbali.

“Majadiliano ya Wadau
Katika kongamano hili, tutakuwa na mijadala mbalimbali itakayojadili masuala muhimu kama vile, jinsi ya kuongeza upatikanaji wa huduma za utengamao katika maeneo ya vijijini na yenye uhaba wa rasilimali, kuimarisha shirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuboresha miundombinu ya huduma za utengamao, kutoa mapendekezo muhimu ya kisera na hatua za kuboresha huduma za utengamao chini
Tanzania lakini pia nafasi ya teknolojia na uvumbuzi katika kuboresha huduma za utengamao, n.k.”

Remla aliishukuru Wizara ya Afya kwa ushirikiano wao wa karibu na msaada mkubwa walioutoa kwa tukio hilo lakini pia juhudi zao kwa ujumla. 

“Tunathamini sana mchango wao katika kuhakikisha mafanikio ya kongamano hili.” Alisema 


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya Dkt. H. Nyembea alisema wizara ya afya inatambua na kuthamini mchango wa huduma za utengamao katika kuimarisha mfumo wa Afya kwani huduma hizo ni sehemu muhimu za kuweza kutibu na kusaidia watu wenye maradhi ya muda mrefu na majeraha na kuweza kuwarejeshea hali zao za kawaida na kuboresha maisha yao.

Pia alisema katika juhudi za serikali katika kuimarisha mfumo wa Afya nchini, serikali kwa kupitia wizara ya Afya imekuwa ikiweka msisitizo mkubwa katika kuhakikisha huduma za Afya zinakua bora hasa zikijumuisha huduma za utengamao ili
Kuweza kukidhi mahitaji ya watanzania wote pasipo na ubaguzi bila kujali hali zao za kiuchumi na maeneo yao ya kijeografia

“Utengamao ni sehemu muhimu ya mkakati huu katika Wizara ya Afya na serikali kwa ujumla kwani unatoa msaada kwa wagonjwa wenye uhitaji wa huduma za urekebishaji wa viungo, kutoa matibabu wa maradhi ya mda mrefu na msaada was kisaikolojia ili kuweza kuwarejesha kwenye maisha ya kawaida na kuboresha Afya zao”

“Huduma za utengamao si jambo la hiari bali ni hitaji muhimu la kuhakikisha mfumo wa Afya unaweza kuwasaidia wananchi wote wenye mahitaji ya kuweza kurejesha afya zao baada ya kupata maradhi hivyo serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea kufanya kazi na wadau mbalimbali wa sekta nje ya serikali ili kuhakikisha huduma hizi zinapanuka na kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa katika upande wa vijijini”

Naye Mratibu Mwandamizi wa Jeshi la Polisi na Mwanasheria na Mratibu wa mafunzo wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, SSP Deus Sokoni, alisema katika kuhakikisha afya ya mtu inatengamaa wanahakikisha wanalinda maisha ya mtu na mali zake pale anapotumia barabarani hivyo ili kupunguza vifo, ajari na majeruhi wanahakikisha uwepo wa elimu ya usalama barabarani.

Kaimu Meneja Mwandamizi wa Mawasiliano na Uhusiano kutoka Benki ya CRDB, Peter Segeja alisema kupitia udhamini wao wanaamini utakwenda kusaidia katika kuleta matokeo chanya hada katika jamii wanayoihudumia kwani uwezo wao wa kupata huduma hizo za utengamao wa Afya inakwenda kuwasaidia kuweza kurudi katika hali zao za kawaida.

“Sisi kama Taasisi ya kifedha, tunatambua manufaa ya kiuchumi ya mfumo huo hivyo inatufanya tuwe mstari wa mbele kusaidia hayo kwani watu hao wakishapata huduma hizo wanaweza kurejea katika kuchangia uzalishaji wa Taifa na kukua kiuchumi kwa ujumla”

Hilda Mlay kutoka Taasisi isiyo ya kiserikali  inayojikita kutoa elimu kuhusiana na Afya ya Jamii pamoja na Tafiti  (MDH) alisema katika kongamano hilo watashiriki katika shughuli mbalimbali kama vile majadiliano ya Afya kuhusiana na huduma za utengamao, matibabu ya mguu wa kifundo, tafiti ndogo walizozifanya kuhusiana na  walichojifunza kupitia utekelezaji wa mradi huo wa mguu kufundo kwa kuweza kutoa mawazo kwa wadau wa afya lakini pia kutoa elimu mbalimbali kuhusu mguu kifundo.