November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau sekta ya bima na mambo yakujivunia miaka mitatu ya Samia

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

KIPINDI cha miaka mitatu cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, cha kuanzia Machi 2021 hadi Machi 2024, maeneo mengi yapata mafanikio makubwa na kujivunia kwa nchi.

Mafanikio hayo yanadhihirisha ushupavu wake kwenye uongozi, ikiwa ni mara ya kwanza nchi yetu kuongozwa na Rais mwanamke, kwani awamu zote tano zilizotangulia marais wake walikuwa wanawake.

Tumeshudia wizara na taasisi mbalimbali zikianika mafanikio ya kiongozi huyo. Miongoni mwa taasisi zilizopata mafanikio hayo chini ya uongozi wa Rais Samia ni Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA)

Mafanikio ya TIRA yanaanikwa na Kamishna wa Bima Tanzania, Dkt Baghayo Saqware, ambapo kupitia sera zilizolenga kukuza uchumi na kuimarisha sekta za kifedha, Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia imechukua hatua kadhaa ambazo zimewezesha kuongezeka kwa shughuli za bima nchini.

Rais Samia ameboresha mazingira ya biashara nchini, ikiwa ni pamoja na kuondoa vikwazo vinavyoweza kuzuia ukuaji wa sekta ya bima.

Hatua hii imewavutia wawekezaji na kusaidia kuongeza ushindani katika soko la bima.

Ndani ya miaka mitatu, Serikali imefanya kazi na taasisi za kifedha kuboresha miundombinu inayohitajika kwa shughuli za bima.

Hiyo ni pamoja na kusaidia kuanzisha mifumo ya kielektroniki ambayo inaruhusu utoaji wa huduma za bima kwa ufanisi zaidi.

Yote yamewezekana kwa juhudi kubwa za Serikali kupitia TIRA ilianzishwa kwa sheria ya Bima Sura Na. 394 ikitekeleza majukumu ya kusajili na kutoa leseni kwa watoa huduma za bima, kuandaa na kutoa kanuni na miongozo mbalimbali ya kusimamia soko la bima na kurekebisha sheria, kutoa elimu ya bima kwa umma, kulinda haki za mteja wa bima na kushauri Serikali kuhusu masuala yanayohusu bima.

Mafanikio ya TIRA kwa kipindi cha Miaka Mitatu ya awamu ya sita chini ya Samia ni pamoja na kuandaa na kutoa kanuni na miongozo ya kusimamia soko la bima na kurekebisha sheria Soko la bima linaongozwa kwa sheria, kanuni, miongozo na taratibu mbalimbali.

Kati ya mwaka 2022 na 2023, TIRA kwa kushirikiana na wadau wa bima wamefanikiwa kuandaa miongozo mbalimbali kwa ajili ya kusimamia na kuendeleza soko la bima.

Miongozo hiyo ni pamoja na Miongozo ya usimamizi wa ubakizaji wa bima na bima mtawanyo, miongozo ya bima ya afya na usajili wa watoa huduma za afya, mion¬gozo ya utoaji wa ithibati kwa warekebishaji na watengene¬zaji wa vyombo vya moto katika sekta ya bima, miongozo ya uendeshaji huduma za takaful na miongozo ya utoaji huduma za bima kidijitali.

Mingine ni; miongozo ya maofisa wauza bima, miongozo ya utekelezaji wa viwango vya kimataifa vya taarifa ya kifedha kuhusu mikataba ya bima (IFRS 17), miongozo ya uwekezaji na usimamizi wa ukwasi, miongo¬zo ya kushughulikia madai ya bima, miongozo ya uendeshaji wa biasharaya benkiwakala na miongozo ya viwango elekezi vya fidia ya bima kwa madai ya majeraha ya mwili na vifo kwa mtu wa tatu kutokana na ajali za magari.

Kusajili na kutoa leseni kwa watoa huduma za bima Mamlaka imefanikiwa kusajili watoa huduma za bima kama ifuatavyo; Kampuni nne za bima mtawanyo, kampuni 36 za bima, wataalamu Nane wa ushauri wa bima mtawanyo na wataalamu nane wa ushauri wa bima mtawanyo waliopewa Ithibati, Kampuni Sita za Bima Mtawanyo zilizopewa Ithibati.

Pia imesajili wataalamu 116 wa ushauri wa bima, mawakala 1096 wa bima, benki wakala 30, wauza bima kidigitali 14, wakadiriaji hasara 56, kampuni Sita za takwimu za bima, wachunguzi binafsi Sita pamoja na maafisa wauza bima 100, waendesha bima za Takaful wawili, washauri wa bima za Takaful mmoja na watoa huduma za afya wanane.

Utoaji wa elimu kwa umma Mamlaka inaendelea na mkakati wake wa utoaji wa elimu kwa umma kwa kushirik¬isha wadau wote kwenye sekta. Lengo ni kufikia asilimia 80 ya Watanzania wote wenye umri wa miaka zaidi ya 18 ifikapo mwaka 2030.

Aidha, mamlaka inaendelea na utekelezaji wa mkakati wa utoaji elimu na uhamasishaji kwa wizara na taasisi za umma kutekeleza sheria ya bima na sheria ya manunuzi, Na.7 ya mwaka 2011.

Hadi Julai 2023, Mamlaka imezitembelea Wizara za Kilimo, Nishati, Uchukuzi, Ujenzi na TAMISEMI.

Mkakati huu ni endelevu na utazifikia wizara, idara na taasisi mbalimbali za umma. Kulinda haki za mteja wa bima Mamlaka imeendelea kuzisimamia kampuni za bima kuhakikisha zinalipa madai na fidia stahiki kwa wakati na kwa haki.

Hadi sasa ulipaji wa madai na fidia umefikia asilimia 95 hivyo kupungua kwa malalamiko.

Hata hivyo asilimia 5 ya madai na fidia yana changamoto ambazo TIRA inafuatilia na kutoa suluhisho. Kwa mfano, ulipaji wa madai ya bima za kawaida uliongezeka kwa asilimia 10.1 kutoka sh. bilioni 301.9 mwaka 2021 hadi sh. bilioni 332.09 mwaka 2022.

Malipo ya madai na mafao ya bima za maisha yaliongezeka kwa asilimia 29.3 kutoka sh. bilioni 95.7 mwaka 2021 hadi sh. bilioni 123.71 bilioni mwaka 2022 .

Jumla ya kiasi cha madai kilicholipwa mwaka 2022 ni sh. bilioni 455.80 hivyo, kupunguza umaskini kwa wanufaika na kufanya biashara kuwa endelevu.

Aidha, TIRA inaendelea na uendeshaji wa mikutano ya kupokea maoni na kusikiliza malalamiko ya bima kwa wananchi ambapo hivi karibuni imefanikiwa kuandaa mikutano mitano katika kanda zake zote.

Kuishauri Serikali kuhusu bima Mamlaka imeendelea kuishauri Serikali katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na eneo la ukatiaji wa bima za lazima, ukatiaji wa bima kwa mali za Serikali na Bima ya Afya kwa wote.

Hivi karibuni TIRA imefanya mkutano na Makatibu Wakuu pamoja na Naibu Katibu Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo ilifanya wasilisho kuhusu tathmini iliyofanywa na TIRA juu ya ukatiwaji bima wa mali za Serikali na pia kutoa ushauri juu ya maswala mbalimbali ya bima.

Kuhusu ukuaji wa sekta ya bima kwa miaka mitatu, Dkt. Saqware anasema sekta hiyo imekua kwa asilimia 26.7 ambapo mauzo ghafi ya bima yameongezeka kutoka sh. bilioni 911 mwaka 2021 hadi kufikia sh. 1,158 bilioni mwaka 2022.

Mchango wa sekta ya bima kwenye pato la Taifa unazidi kuongezeka kutoka asilimia 1.68 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 1.99 mwaka 2022.

Mamlaka imeendelea kuongeza gawio Serikalini ambapo kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Juni 2023 Mamlaka imelipa gawio kwa Serikali la jumla ya sh. bilioni 2.9.

Aidha, sekta ya bima imechangia kwenye ajira kwa vijana ambapo hadi Septemba 2022 imetoa ajira za kudumu kwa watanzania 4, 173. Mafanikio mengine yaliyopatikana Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2022/2023 Mamlaka imepata mafanikio kadhaa ikiwa ni pamoja na Uanzishaji wa Konsotia ya Bima ya Kilimo Ili kutekeleza skimu ya bima ya kilimo Tanzania kwa ufanisi, Julai 10, 2023, kulizinduliwa Konsotia ya Bima ya kilimo (Agriculture Insurance Con¬sortium).

Konsotia hiyo imeanzishwa ili kuweka ufanisi katika utekelezaji wa Skimu ya Taifa ya Bima ya Kilimo (TAIS) na kuongeza uwezo wa kimtaji wa soko la bima nchini kwa ajili ya kukinga majanga kwenye sekta ya kilimo.

Konsotia hiyo imeundwa na kampuni za bima zinazotoa bima ya kilimo zipatazo 15 ikiwa ni pamoja na kampuni tatu za bima mtawanyo zilizosajiliwa nchini na za kikanda ambazo ni Tanzania Reinsurance Com¬pany (TAN-RE), Africa Reinsurance Corporation (Africa Re), na PTA Reinsurance Company (ZEP-RE).

Mtaji wa kukinga majanga wenye thamani ya Sh 300 bilioni umetengwa kwa ajili ya kukinga majanga kwenye sekta ya kilimo.

Pamoja na mambo mengine Konsotia hiyo itasaidia kuongezeka kwa upatikanaji wa mtaji unaohitajika na kutumika katika ulipaji wa fidia na madai ya bima kwenye sekta ya kilimo, kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango na mikakati ya kitaifa ya kilimo, kurahisisha ulipaji wa madai ya mkulima mara janga linapotokea, kuongezeka kwa imani kwa mkulima kuhusiana na umuhimu na matumizi ya bima, kuchochea ukuaji wa sekta ya kilimo na sekta ya bima, kuvutia uwekezaji kwenye sekta ya kilimo na sekta ya bima na kuongeza ajira kwa Watanzania.

Uanzishaji wa Konsotia ya Bima ya Mafuta na Gesi Konsotia ya Bima ya Mafuta na Gesi ilizinduliwa Novemba 16, 2022 jijini Dar es Salaam Mantiki ya kuanzisha konsotia hii ni kuhakikisha miradi yote ya gesi na mafuta inabakiza sio chini ya asilimia 45 ya ada zitokanazo na gesi na mafuta, kufuatia kutokuwa na uwezo wa soko la ndani, vihatarishi vya nishati, vilielekezwa nje ya nchi kwa asilimia 100 jambo lisilo na tija kwenye uchumi wa nchi.

Aidha, kuanzishwa kwa mira¬di mikubwa ya nishati kama vile bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ni fursa kwenye sekta ya bima kujipanga kwa ajili ya kuongeza tija, uchumi na ajira nchini.

Malengo ya kuanzisha kon¬sotia ni kutoa fursa kwa kam¬puni za bima za ndani kushiriki na kuandikisha vihatarishi vya nishati ya Gesi na Mafuta ndani ya nchi na kushiriki katika bima ya mradi wa LNG, unaokadiriwa kuwa na gharama ya uwekezaji wa Dola za marekani bilioni 40 hivyo kuongezeka kwa ada za bima za kila mwaka na faida zitokanazo na kamisheni.

Mikakati ijayo ya TIRA hadi mwaka 2025/26 TIRA kwa kushirikiana na wadau wa bima inaendelea na utekelezaji wa mipango na mikakati ya Taifa pamoja na maelekezo ya viongozi wa juu wa kitaifa akiwemo Rais Dkt Samia na Rais Dkt Mwinyi waliyoyatoa kwa nyakati tofauti.

Miongoni mwa mikakati ya TIRA kwa mwaka 2025/26 ni; kuanzisha na kutekeleza Mpango wa kitaifa wa Bima ya Kilimo, uanzishwaji wa bodi ya wataalamu wa Bima, Hifadhi ya Jamii na Takwimu Bima.

Kuunganisha mifumo ya kidigitali na taasisi mbalimbali za umma ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi, LATRA, NIDA, TASAC, TRA, PTA, ZRA.

Lengo ni kuongeza usimamizi na maendeleo ya soko la bima, kuendelea na utoaji wa elimu ya bima kwa umma na wadau mbalimbali. Kufungua ofisi za Bima Mtawanyo za Kikanda ambazo Serikali inamiliki hisa za moja kwa moja au kupitia taasisi zake ili kampuni hizo ziweze kufungua ofisi nchini kwa utaratibu wa mikataba ya uenyeji na kuendelea kukusanya mao¬ni ya wananchi kwa lengo la kuhuisha Sheria ya Bima Sura 394.

“Naomba kumpongeza na kumshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uongozi bora na kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji ikiwa ni pamoja na kwenye sekta ya bima na Rais wa Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi kwa melekezo yake na kwa ushirikiano wake,” anasema Dkt Saqware.

TIRA kwa kushirikiana na Bodi ya Taifa ya Bima itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwenye sekta ya bima kwa ajili ya kuendeleza na kusimamia soko la Bima kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Kwa mujibu wa Dkt. Saqware TIRA ni taasisi ya Muungano chini ya Wizara ya Fedha na inaongozwa na Kamishna wa Bima akisaidiwa na Naibu Kamishna wa Bima na inasimamiwa na Bodi ya Taifa ya Bima inayoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi.

Anasema ili kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake na kusogeza huduma kwa wananchi, TIRA hadi kufikia sasa ina ofisi zifuatazo;

Makao Makuu Dodoma, ofisi ya Zan-zibar, Dar es Salaam na Kanda ya Magharibi (Tabora, Katavi na Kigoma).

Nyingine ni Kanda ya Ziwa (Mwanza, Mara, Shinyanga, Kagera, Simiyu na Geita) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya, Njombe, Rukwa, Iringa na Songwe) Kanda ya Kaskazini (Arusha, Kilimanjaro na Tanga), Kanda ya Kati (Dodoma, Singida na Manyara) Kanda ya Kusini (Lindi, Mtwara na Ruvuma) na Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam, Pwani na Morogoro)