January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau muziki wa dansi waitwa Dodoma

Na Daudi Magesa , TimesMajira Online, Mwanza

WAPENZI na wadau wa Muziki wa Dansi nchini wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye hafla ya utoaji wa Tuzo za muziki huo za ‘Cheza Kidansi Music Award’, zitakazotolewa Desemba mwaka huu jijini Dodoma.

Tuzo hizo ambazo zilianzishwa na kuzinduliwa mwaka 2019, mwaka huu zitahusisha vipengele 11 kwa wasanii wa muziki huo uliowahi kuvuma na kukonga nyoyo za wapenzi wa muziki huo miaka ya 70 kabla ya kutetereka na kushuka chati.

Vingele 11 vya tuzo hizo vitakavyoshindaniwa ni Bendi Bora, Wimbo Bora, Video Bora, Mtunzi Bora, Mwimbaji Bora, Mwanamuziki Bora, Mwanamuziki Bora Vhipukizi, Rapa Bora, Tuzo ya Heshima na Wimbo Bora wa Kushirikiana (Best Collabo).

Pia vipengele vya Mnenguaji Bora, Mpiga vyombo Bora na Wanamuziki kutoka nje ya nchi ikiwemo Jamhuri ya Kidemkrasi ya Congo (DRC) viliondolewa ili kuongeza chachu kwa vipengele vilivyopitishwa na kukuza muziki huo nchini.

Vipengele hivyo vilianishwa na watalaam waliobobea kwenye tasnia ya muziki wa dansi nchini waliokaa na kuvichambua kwa umakini na umahiri mkubwa kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Cheza Kidansi, Benard James amesema kuwa, msimu huu tuzo hizo zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na mwaka jana.

Amesema, maboresho yaliyofanyika yameongeza ushindani na kuchochea wasanii wa muziki huo kuwasilisha kazi nyingi na zenye ubora wa hali ya juu.

“Mwaka huu ushindani na upinzani utakuwa mkubwa kutokana na maboresho ya tuzo ambayo yamechochea wanamuziki wengi kuwasilisha kazi (tungo) zenye ubora na ubunifu wa hali ya juu, tunaamini ushindani utakuwa kwenye eneo la rapa bora ambalo wengi na wenye majina makubwa wameshiriki kwa kuingiza nyimbo zao binafsi na za bendi ,” amesema James.

Amewataka wanamuziki na bendi zilizotoa kazi zao mwaka huu kutunza taarifa zao ili kurahisisha mchujo wa kuwapata washindi na akashauri watembee mtandao wa Cheza Kidansi kupata taarifa za tuzo.

Akitaja sababu za tuzo hizo kutolewa jijini Dodoma, Mkurugenzi huyo amesema, kwakuwa tuzo hizo zinalenga kuzisogeza kwa wananchi ili kuchochea ari na kuwaamsha mashabiki wa muziki wa dansi nchini ili kuuhuisha muziki huo.