Na Israel Mwaisaka Sumbawanga
WACHIMBAJI wadogo wawili Wamefariki dunia ndani ya mgodi,baada ya kukosa hewa kutokana na kuchimba shimo lenye urefu wa mita 21.5 na kisha kuamua kuwasha mashine maalumu ya kutoa maji ndani ya mgodi huo ili waweze kuendelea na kazi ya kuchimba kutafuta madini.
Tukio hilo limetokea Julai 23, majira ya saa 9;30 alasiri, katika Kijiji cha Kalundi,kata ya Kipande, tarafa ya Kate wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, ambapo wachimbaji wadogo waliofahamika kwa majina ya Justine Salawa(27) mkazi wa kijiji cha Kalundi pamoja na Fredy Agustino mkazi wa Kijiji cha Kaoze wilayani Sumbawanga walikufa ndani ya mgodi kutokana na kukosa hewa safi.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa,Kamishna Msaidizi wa Polisi,Ralph Meela amesema kuwa wachimbaji hao waliingia kwenye shimo hilo wakiwa watatu na kuendelea na kazi ya kuchimba madini, na ghafla maji yaalibuka hali iliyosababisha kushindwa kuendelea na kazi hiyo, hivyo kuamua kuwasha mashine kwa ajili ya kutoa maji hayo.
Baada ya kuwasha mashine hiyo, moshi ulitanda katika shimo hilo, hali iyosababisha kukosa hewa safi na kuzidiwa na hewa ukaa, kisha mmoja kati yao alifanikiwa kutoka nje na kuokoa maisha yake,huku wachimbaji wawili walishindwa kupata msaada wa haraka na kufariki dunia.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Kamanda wa Polisi Meela baada ya tukio hilo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilifika katika eneo la tukio, lakini kutokana na umbali mrefu walichelewa na walikuta watu hao wamekwisha fariki dunia na kufanikiwa kuitoa miili hiyo ndani ya mgodi huo kisha kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kukabidhiwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya maziko.
Amesema polisi wanamshikiria mfanyabiashara mmoja(52), mkazi wa eneo la Kantalamba mjini Sumbawanga ambaye ni mmiliki wa mgodi huo kwa kosa la kuanzisha mgodi huo na kufanya uchimbaji wa madini bila kuwa na kibali.
Ametoa wito kwa wananchi wanaomiliki migodi na maeneo ya machimbo ya madini kufuata taratibu na kuwa na vibali.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa