September 30, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wachimbaji wahamasishwa kutumia Teknolojia  uchimbaji madini

Na Joyce Kasiki,Geita

VIONGOZI wa sekta ya madini mkoani Geita wamewahamasisha wachimbaji, wanawake na wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu katika Maonyesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Dkt.Samia Suluhu Hassan mkoani Geita.

Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Madini Mkoa wa Geita, Mshana  Jeremiah, ametoa kauli hiyo katika  maonyesho ya teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita  wakati akizungumza na waandishi wa habari huku akisema siku ya Ijumaa Oktoba  2, 2026  itatumika kujadili na kuhamasisha ushiriki wa Watanzania katika rasilimali za madini na gesi kupitia dhana ya Local Content.

Amesema siku hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi na wadau mbalimbali, akiwemo Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA), John Bina Wambura, pamoja na Mchungaji Mwamposa, ambaye anatarajiwa kushiriki maonyesho hayo kama mmoja wa wachimbaji.

Aidha, Waziri wa Madini, Anthony Peter Mavunde, anatarajiwa kushiriki katika shughuli hizo, kuanzia kwenye semina hadi kukutana na wachimbaji kwa ajili ya kusikiliza changamoto zao na kutoa miongozo kuhusu shughuli za uchimbaji.

Mjumbe wa Kamati ya Mwanamke na Madini, Rehema, amewataka wanawake wanaojihusisha na mnyororo wa thamani wa madini mkoani Geita na maeneo mengine kujitokeza kwa wingi kushiriki katika semina na shughuli mbalimbali zitakazofanyika wakati wa maonyesho hayo.

Rehema amesema ushiriki wa wanawake ni muhimu katika kuhakikisha wanatumia na kunufaika na fursa zinazopatikana ndani ya sekta ya madini.

Kwa upande wake, Jeremiah amesema sekta ya madini imeendelea kubadilika kutokana na matumizi ya sayansi, maabara na teknolojia za kisasa katika shughuli za uchimbaji.

Amesema tofauti na zamani ambapo baadhi ya wachimbaji walitegemea imani na taratibu zisizo za kisayansi katika kutafuta madini, wachimbaji wa sasa wameanza kutumia maarifa na teknolojia ili kuongeza ufanisi na tija.