Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline, Dodoma
RAIS Samia Suluhu Hassan, ametunukiwa tuzo na wabunge wanawake nchini kwa kushirikiana na Kampuni ya Oryx Gas Tanzania kwa kutambua mchango wake katik kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Tuzo hiyo kwa Rais Dk.Samia imetolewa jana Mjini Dodoma wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Nishati Safi Kupikia Duniani, ambapo Kampuni ya ORYX pamoja na wabunge wanawake, wabunge vinara katika nishati safi walitumia maadhimisho hayo kujadili kwa kina mchango wa Rais Dk.Samia katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia Afrika na hasa Tanzania.
Spika wa Bunge Dk.Tulia Ackson ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Maadhimishi hayo alisema kuna kila sababu za Rais Dk.Samia kupewa tuzo na wabunge hao pamoja na Oryx kwani amekuwa kinara katika nishati safi ya kupikia na juhudi zake zinashuhudiwa na Watanzania, Afrika na Dunia kwa ujumla.
Amesema Rais Samia alipokuwa Dubai na hivi karibuni alipoenda katika mkutano uliofanyika Paris ametambulika na dunia nzima kama kinara wa nishati safi ya kupikia.Hivyo wanaendelea kusisitiza Rais Samia ndiye kinara wa nishati safi ya kupikia.
Amesema katika Bara la Afrika kunachangamoto ya nishati ya kupikia na takwimu zinaonesha asilimia 80 barani Afrika wanatumia nishati isiyo safi ya kupikia na ili kutoka katika nishati hiyo na kurudi katika sifrui kabisa itachukua muda.
“Hivyo Rais Dkt.Samia anasaidia kuupunguza muda kwa kuendelea kutafuta fursa kubadilisha upikaji kwa kuacha kutumia nishati chafu na kuhamia katika nishati safi ya kupikia kama gesi.Juhudi hizo za Rais zimeanza hapa nchini Tanzania na takwimu nchini zinaonesha asilimia 90 za wananchi mpaka sasa wanatumia nishati isiyo safi ya kupikia.
“Hivyo juhudi za Rais zinatusogeza angalau kutoka asilimia 90 na kusogea mpaka 25 ili wawe wachache wanaotumia nishati chafu ya kupikia.
Akifafanua zaidi Dkt.Tulia Ackson amesema wanafahamu nishati isiyo safi ina madhara kwa binadamu na kwa hapa nchini inaonesha vifo takribani 33000 hutokea kila mwaka kutokana na athari za kutumia nishati isiyofaa na hivyo kupoteza nguvu kazi ya Taifa kwa sababu tu za kutumia nishati safi.
Amesema mbali ya vifo, lakini kutumia nishati chafu kumekuwa kukisababisha athari mbalimbali za kimazingira na kijamii huku akitumia nafasi hiyo kueleza namna ambavyo wanawake na mabinti wamekuwa wakitumia muda mwingi kutafuta kuni na mkaa badala ya kufanya shughuli za kimaendeleo, hivyo Rais Samia amedhamiria kuwaondoa wananchi katika changamoto zinazotokana na nishati chafu ya kupikia.
“Tunampongeza Rais Dk.Samia kwa hatua anazochukua kwasababu zitamfanya mwanamke ambaye ndiye huwa anashinda jikoni na athari nyingi zinampata mwanamke na binti na katika kuhakikisha mwanamke anasogea mbele katika maendeleo,”amesema.
Amesisitiza kuwa juhudi hizo za Rais Samia zinakwenda kumaliza athari zinazotokea kwa binadamu lakini pamoja na mazingira kwani hekta zaidi ya 500000 zinaharibiwa kila mwaka kwasababu ya kukata kuni na mkaa.
“Katika kufanikisha kampeni ya nishati safi ya kupikia Rais Dk.Samia ametafuta wadau mbalimbali na hapa nimefurahi kuona Oryx wanaungana na wabunge wanawake katika kumuunga mkono Rais Samia katika hatua alizochukua katika maeneo mbalimbali ya kuhakikisha mazingira yetu yanakuwa salama.
“Hivyo siku ya leo Rais Dk.Samia anapopewa tuzo hii kwa kweli anastahili kwani unapotazama juhudi anazochukua kuhakikisha wananchi wa Tanzania tunakuwa salama lakini pia Bara la Afrika kwa ujumla linakuwa salama.Pia tunafahamu Rais aliagiza Serikali yake kuchukua hatua katika eneo hili na yeye mwenyewe akiwa kinara na ndio maana tayari kuna mkakati wa taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia wa mwaka 2024 mpaka 2034,”amesema Dk.Tulia.
Akitaja baadhi ya mambo yaliyomo katika mkakati huo wa Serikali wa kipindi cha miaka 10 ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kupunguza bei ya gesi kila mwananchi aweze kumudu gharama sambamba na utolewaji wa ruzuku kwa ajili ya kununua vifaa vya nishati safi pamoja na kupunguza baadhi ya tozo kwa vifaa vya gesi.
“Nawapongeza wabunge kwa hatua wanazocukua za kuishauri Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha juhudi hizi zinazofanywa na taasisi binafsi kama Oryx basi Serikali nayo inaenda huko.Tumesikia Oryx wametoa mitungi zaidi ya 35000 lakini ni dhahiri kaya tunazo nyingi zaidi ya hizo walizotoa na tungetamani wafike mbali zaidi.”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Oryx Gas Tanzania Benoit Araman amesema katika kutambua mchango wa Rais Samia katika nishati safi wameamua kutoa tuzo kwa Rais kama sehemu ya kumuunga mkono kwa juhudi anazofanya kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo.
Kuhusu ujumbe ulioandikwa katika tuzo hiyo Benoit amesema imeandikwa hivi, “Kampuni ya Oryx Energies inatoa tuzo hii kwa Mh.Dkt.Samia Suluhu Hassan ,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,kwa kutambua UONGOZI wake wa kipekee katika kushinda na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania na Afrika.”
Akitoa ahadi ya kampuni hiyo amesema hadi sasa wameshatoa mitungi ya gesi na majiko yake 35,000 kwa makundi mbalimbali nchini na wataendelea na mkakati wao kwani dhamira yao ni kuona asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2032 inafikiwa kama ambavyo ambavyo Rais Samia ameelekeza.
Awali Mwenyekiti wa Wabunge Wanawake nchini Shally Raymond amesema wabunge wanawake pamoja na wabunge vinara wa nishati kwa kushirikiana na Oryx wameamua kutoa tuzo kwa Rais huku akitumia nafasi hiyo kupongeza jitihada zinazochukuliwa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia nchini.
More Stories
Balozi Nchimbi kuongoza waombolezaji mazishi ya Kibiti leo
Dkt.Tulia,apewa tano kuwezesha wananchi
Nkasi yajipanga kukusanya mapato