March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wabunge Mashabiki Simba na Yanga kuchuana Bunge Bonanza

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

Tamasha la michezo la Bunge bonanza 2026 linatarajiwa kufanyika Januari 31 katika viwanja vya shule ya Sekondari John Merlini jijini hapa ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Mwigulu Nchemba

Bonanza hilo kutanguliwa zoezi la mashabiki wa klabu za Yanga na Simba kushiriki kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wenye uhitaji, katika bonanza la Bunge litakalofanyika Januari 31, jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Bunge Bonanza ambaye pia ni Mbunge wa Makete, Festo Sanga, amesema tamasha hilo linatarajiwa kuwa na mgeni rasmi ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba.

“Bonanza hili litakuwa  na michezo na burudani mbalimbali, ikiwemo kukimbiza kuku, mbio, mpira wa pete, kuvuta kamba, mpira wa kikapu pamoja na kushindana ya kula,”amesema Sanga.

Amesema mashabiki wa Simba na Yanga wanatarajiwa kupimana nguvu katika bonanza hilo litakalowakutanisha wabunge, wafanyakazi wa Bunge, wizara pamoja na taasisi mbalimbali.

“Bonanza hili ni maono ya Bunge, menejimenti na Spika kuhakikisha linakuwa kiungo cha kuimarisha mahusiano na wadau mbalimbali, kwa kuwa Bunge ni chombo cha wananchi,” amesema Sanga.

Ameongeza kuwa bonanza hilo pia linalenga kudumisha umoja na mshikamano kati ya Bunge na taasisi mbalimbali, sambamba na kuunga mkono  sekta ya michezo.

Kwa upande wake, Meneja Mahusiano wa Azania Benki, Elizabeth Nyayega,ambao ndiyo Mdhamini Mkuu wa Bonanza hilo amesema benki hiyo imeendelea kudhamini bonanza hilo kwa kutoa vifaa vya michezo na huduma nyingine za kimfumo pamoja na huduma za kibenki kwa washiriki na jamii.

Amesema ushiriki wa Azania Benki kama mdhamini mkuu wa bonanza hilo unalenga kuhimiza faida za michezo ikiwemo kuboresha afya, mshikamano wa kijamii, malezi kwa vijana na maendeleo endelevu ya jamii.