December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wabia wa maendeleo waombwa kuunga mkono juhudi za serikali kukuza ujuzi na ajira

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

NAIBU Waziri wa Kilimo ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Dodoma Mjini,Anthony Mavunde ametoa wito kwa Wabia wa Maendeleo na sekta binafsi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwa ajili ya kukuza ujuzi na ajira kwa vijana.

Mavunde ametoa wito huo alipokuwa anafunga Kongamano la ujuzi na ajira liliondaliwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)kwa kushirikiana na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ) kupitia programu yake ya Kukuza Ajira na Ujuzi kwa Maendeleo Afrika (E4D)iliyowanufaisha jumla ya vijana 3,258 kupata mafunzo ya ajira na ujuzi.

“Tunahitaji kuwekeza katika miundombinu bora ya elimu na mafunzo, kuboresha upatikanaji wa mitaji na mikopo kwa vijana wajasiriamali, na kuweka mazingira rafiki ya biashara,

“Pia tuendelee kuhamasisha ushirikiano kati ya vyuo vya ufundi, taasisi za elimu na waajiri ili kuhakikisha kuwa mafunzo yanalingana na mahitaji halisi ya soko la ajira.

Amesema vijana ni rasilimali muhimu na nguvu kazi yenye kuleta mabadiliko na kuchangia katika maendeleo ya nchi yetu hivyo wanapaswa kuwezeshwa kutimiza ndoto zao, kuendeleza ujuzi wao ili wachangie katika ujenzi wa Tanzania bora na endelevu.

Aidha ametoa pongezi kwa vijana waliofanya maamuzi ya kuja kuchukua mafunzo ya Ufundi Stadi katika fani za Ufundi Bomba wa Majumbani, Ufundi Bomba wa Viwandani, Ufundi Uchomeleaji na Uungaji Vyuma wa Viwandani, na Mekatroniki.

“Nimepewa taarifa kuwa hadi sasa, tayari vijana 3,258 wamepata fursa ya kujifunza na kuendeleza ujuzi wao katika vyuo vya VETA Dodoma, Manyara, Lindi, na Kipawa, Hii ni hatua muhimu katika kuwawezesha vijana kupata ajira au kujiajiri wenyewe, kuwa wajasiriamali na kuwa sehemu ya kuleta mabadiliko chanya kiuchumi na kijamii nchini,

“Nimeelezwa kuwa, kongamano hili ni moja ya shughuli kuu za program ya E4D ambalo linatoa fursa nzuri ya kuonesha mafanikio kwa kuwakutanisha wahitimu, waajiri, taasisi za kifedha, na wadau wengine ambao wamechangia katika kukuza ujuzi na ajira kwa vijana.

“Maonesho haya yanatoa fursa ya kubainisha talanta na ujuzi uliopatikana kupitia mafunzo na kuanzisha mazungumzo kati ya wahitimu na waajiri ili kuwezesha kupatikana kwa ajira na fursa za biashara,”amesema Mavunde.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA , CPA Anthony Kasore ameeleza kuwa VETA inatekeleza mradi huo kupitia vyuo vya Dodoma RVTSC, Manyara RVTSC, Lindi RVTSC na Kipawa ICTC. Shabaha ni kuwafikia vijana 4,000 katika fani za Mechatronics, uchomeleaji viwandani, pamoja na ufundi bomba majumbani na viwandani.

Huku akitaja shughuli zinazotekelezwa katika mradi huo kuwa ni pamoja na Utengenezaji wa Mtaala inayoendana na mahitaji ya Soko la Ajira, ambapo wadau wote muhimu walishirikishwa katika kutengeneza mitaala ya mafunzo yaliyolengwa kwenye mradi.

“Mafunzo kwa Walimu na Wasimamizi Wa Mafunzo, Walimu wote wanaoshiriki katika kutekeleza mradi, walipewa mafunzo kwa ajili ya kufundisha mitaala mipya kwa kutumia wataalamu toka viwandani, kwenye fani za Ufundi Bomba Viwandani na Ufundi wa Uchomeleaji na Uungaji Vyuma Viwandani,”amesema.