December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waasisi wa TAMWA wapewa Tuzo za Heshima

Na Penina Malundo,TimesMajira. Online

MWENYEKITI wa Baraza Ia Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuna mafanikio makubwa yaliyofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA), kusaidia kupunguza matukio mbalimbali ya ukatili yaliyokuwa yakilitia aibu taifa kama mauaji ya watu wenye ualbino, vikongwe na ubakaji miaka ya nyuma.

Ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam jana wakati wa utoaji wa Tuzo za Heshima, kutambua mchango wa waasisi wake 12 walioanzisha chama hicho katika kuadhimisha Siku ya Wanamke Duniani.

Amesema TAMWA kupitia waasisi wake, walifanya mapambano ya kupinga masuala ya ukatili ambapo hali haikuwa rahisi na kauli iliyokuwa ikitawala ni kuwa kila mwanaume mwenye mafanikio, nyuma yake kuna mwanamke ambapo hadi sasa wanawake wanaonekana katika sehemu mbalimbali.

Dkt. Mwakyembe amesema, harakati za akinamama kupata haki zao ilikuwa changamoto na chama hicho ambapo kupitia, TAMWA waliweza kupigana na kuchangia kwa kiasi kikubwa kupata haki za wanawake.

“Nawapongeza sana hawa wanawake 12 wa nguvu kwa kukataa kuwezeshwa wao wenyewe wakaanzisha TAMWA, kwani TAMWA imechangia sana wanawake kupata haki zao,” amesema na kuongeza;

“Ninawapongeza TAMWA kwa kusimamia kesi ngumu za watoto na wanawake wanaofanyiwa ubakaji na mimba za utotoni hili linajenga taifa imara kupitia waasisi 12, ambao tunawaongelea leo, wameweka alama ya kudumu katika taifa letu, binafsi nawapongeza sana”.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa TAMWA, Rose Reuben amesema waliamua kuadhimisha Siku ya Mwanamke kwa kuwaenzi waasisi hao 12, ambao walikuwa na msukumo wa kutetea haki za wanawake na watoto wa kike.

Amewataja wanawake hao kuwa ni Halima Shariff, Elizabeth Marealle, Rose Kalemera, Leila Sheikh, Nelle Kidela (marehemu) Fatma Alloo, Edda Sanga, Ananelia Nkya, Rose Haji, Pili Mtambalike, Jamila Chipo (marehemu) na Valeria Msoka.

Amesema waasisi hao kwa nyakati tofauti walishika nyadhifa katika taasisi serikali, zisizo za kiserikali na za kimataifa ambapo waliweza kuhamasisha utawala bora kwa kuhimiza ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi.

Rose amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema ‘Mwanamke katika uongozi, chachu kufikia dunia yenye usawa’ wanajivunia waasisi hao wa TAMWA ambao wameweza kutimiza wajibu wao’.

Amewataka wanawake vijana, kuanzisha mawazo yatayosaidia watu wengine kama ambavyo waasisi hao walivyofanya.

“Waasisi walionzisha TAMWA wawili kati yao wameshafariki dunia, lakini mawazo yao yanaishi hadi sasa, haki zinatendeka chini ya sheria zilizopitisha kupitia mawazo waliyoyatoa. Niwaase wanawake vijana msilale na mawazo yawasilisheni kwa ajili ya kusaidia mabadiliko ya wenzetu,” amesema.

Naye mwasisi wa chama hicho, Fatma Alloo amesema ni chama cha hiari kilizaliwa wakati hawana nafasi au uwezo kila kitu walikuwa wanajitolea.

“Nawaasa waandishi wa habari wa sasa kupenda kusoma ili muongeze maarifa na kuhakikisha mnapendana, kufanya kazi kwa bidii na kutimiza malengo mliojiwekea,” amesema.

Kwa upande wake mwasisi mwingine wa TAMWA, Rose Haji amesema haikuwa kazi rahisi kuanzisha chama hicho wakati huo, changamoto zilikuwa nyingi lakini walishikamana kuhakikisha wanatimiza lengo hilo katika wakati, ambao wanawake walikuwa hawapewi kipaumbele kwa kuwa hawakuaminika.