January 6, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waandishi watakiwa kuandika habari sahihi

Na Ahmad Mmow,TimesMajira Online. Lindi

WAANDISHI wa habari Mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Pwani wametakiwa kuandika kwa usahihi habari zinazohusu mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ili jamii ipate taarifa za kweli zinazohusu mpango huo.

Wito huo umetolewa juzi mjini hapa na Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Rehema Madenge wakati wa kikao kazi cha kuwajengea uelewa waandishi wa habari kuhusu mzunguko wa pili wa awamu ya tatu ya utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini.

Rehema amesema waandishi wa habari ni nguzo muhimu ya kuelimisha, kufundisha na kuhabarisha jamii taarifa mbalimbali tena za kweli na sahihi.

Amesema watu wengi wanasikia mpango huo na wanataka kujua ukweli wa hayo wanayosikia hivyo waandishi wa habari, ambao wanafika katika maeneo ya utekelezaji wana kila sababu ya kueileza jamii kuhusu ukweli na usahihi wa wanayoyaona.

Rehema amesema kazi ya uandishi ni ibada, hasa waandishi wanapoandika habari chanya zinazogusa watu wengi na hatimaye watu hao, wakabadilika kutoka katika hali moja na kwenda hali nyingine ya mafanikio.