December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waandishi wapewa elimu wachangamkie fursa za uchumi wa bluu

Judith Ferdinand na Daud Magesa,Mwanza

WAANDISHI wa Habari zaidi ya 20 na wanachama wa Chama Cha Waandishi wa kuendeleza Shughuli za Bahari na Uvuvi Tanzania (TMFD),wamapatiwa elimu juu uchumi wa bluu ili waweze kuchangamkia fursa katika eneo hilo na kuondokana na umasikini.

Kabla ya mafunzo hayo walitembelea mradi wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba katika Ziwa Victoria kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo uendeshaji wa shughuli hiyo ili kuwaelimisha wafugaji na jamii ziara iliofanyika maeneo ya Luchelele na Butimba.

Mratibu wa kongamano hilo Betty Massanja akizungumza wakati wa mafunzo yaliotolewa na TMFD kwa waandishi wa habari mkoani Mwanza

Akizungumza Machi 8,2024 katika kongamano la Uchumi wa Bluu lililoenda sanjari na maonesho ya picha lililoandaliwa na TMFD na kufanyika jijini Mwanza Mratibu wa kongamano hilo Betty Massanja limelenga kuongeza uelewa kwa waandishi wa habari kufahamu na kuchangamkia fursa za uchumi huo.

Betty ameeleza kuwa waandishi wa habari wakizifahamu fursa za uchumi wa buluu wataielisha jamii na kuhamasisha wananchi kupitia kalamu zao kuchangamkia fursa zilizopo katika uchumi huo ikiwemo ufugaji samaki kwa njia ya vizimba, uuzaji wa dagaa,usafirishaji wa mazao ya uvuvi,upishi katika meli kubwa za kitaifa,kilimo cha mwani na shughuli nyingine nyingi.

“Wanahabari katika kukuza sekta ya uvuvi, wakiwa mstari wa mbele kuhamasisha wadau na wananchi wataweza kuchangamkia fursa za uchumi wa buluu,watajiongezea kipato na kutoa mchango kwa taifa,”amesema Betty na kuongeza;

“Binafsi sitaki kuwa masikini,wito wangu kwa wanahabari wenzangu,tufanye kila linalowezekana tuwekeze tupate miradi ya kututoa kiuchumi na kuionesha dunia kuwa inawezekana.”

Baadhi ya Waandishi wa Habari wakiwa kwenye mtumbwi ndani ya Ziwa Victoria eneo la fukwe ya ‘Stress Free’ uliopo Butimba jijini Mwanza kwa ajili ya kujifunza utalii wa kuvua samaki

Pia amesema bado zipo fursa nyingi katika uchumi wa buluu kupitia vyanzo vilivyopo vya Bahari ya Hindi,mito na maziwa ambapo Mwanza kuna Ziwa Victoria”hivyo tusibaki nyuma na kubweteka tuchangamkie fursa hizo tuinuke kiuchumi na kujiongezea vipato”.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la Luchelele, Mkurugenzi wa Kampuni ya My fish Tanzania inayojihusisha na ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, Elpidius Mpanju,amesema uchumi wa buluu ni agenda ya dunia na mwelekeo wa kupata samaki ifikapo 2030,utakuwa asilimia 70 kwa wafugaji na asilimia 30 ni uvuvi wa asili.

Amesema ma ufugaji wa samaki kwa vizimba una tija zaidi tofauti na uvuvi wa asili ambao mvuvi hana ukakika wa kupata samaki wa kutosha, hivyo serikali iwekeze na kuhamasisha ufugaji huo.

Mpanju amesema ufugaji huo samaki utatatua changamoto ya uhaba wa samaki katika Ziwa Victoria unaosababishwa na kuongezeka kwa mahitaji huku mazalia ya samaki yakipungua kutokana na changamoto za uharibifu wa mazingira na uvuvi haramu.

Amesema teknolojia inakua kutokana na kubadilika kutoka ile ya awali,imerahisisha shughuli za ufugaji wa samaki kwa vizimba,mashamba ya kuzalishia ni mengi,mbegu bora za samaki zinapatikana na kuwafanya waende haraka, wataalamu wa ukuzaji wa viumbe hai wapo kuhakikisha kinachofanyika ni sahihi.

“Zipo fursa nyingi za kufuga kutokana na kuwepo eneo la maji (Ziwa Victoria),kuna soko kubwa la samaki wa maji baridi hasa sato na hivi karibuni Serikali ilitoa bilioni 20 kwa wavuvi wafuge kwa njia ya vizimba, tunamshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutuona sisi wavuvi,”amesema.

Mkurugenzi wa My Fish,Elpidius Mpanju

Naye Msimamizi Ufukwe wa ‘Stress Free Beach’ Darius Salvatory unaoendeshwa na Jeshi la Magereza katika eneo la Butimba jijini Mwanza,amesema ufugaji samaki katika ufukwe huo umeongeza chachu kwa wateja ambapo hupata fursa ya kufanya utalii wa uvuvi kwa kuvua samaki kwa ajili ya kitoweo.

Baadhi ya vizimba vya kufugia samaki eneo la Luchelele