Judith Ferdinand, Timesmajira Online,Mwanza
Waandishi wa habari wameombwa kuepuka kutoa taarifa zenye lugha ya uchochezi, matusi, au zinazoweza kusababisha vurugu au chuki za kijamii, kikabila, au kidini hasa wakati huu wa kampeni na kuelekea kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 29,mwaka huu.
Huku wakitakiwa kuripoti habari na matukio yote ya uchaguzi kwa usahihi,haki na bila upendeleo kwa chama, mgombea au msimamo wowote wa kisiasa na kuweka uwiano sawia wa taarifa kwa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi.

Wito huo umetolewa Septemba 22,2025, na Ofisa Uchunguzi Mwandamizi Haki za Binadamu na Utawala Bora, Yohana Mcharo,kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora(THBUB),wakati akiwasilisha mada katika mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari na jeshi la polisi kuhusu haki za binadamu na wajibu wakati wa uchaguzi mkuu.
Mcharo amesema,waandishi wa habari wachukue tahadhari zaidi kuepuka kuchangia au kueneza chuki wakati wanaporipoti matukio katika kipindi hiki cha uchaguzi na badala yake wafichue vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji misingi ya utawala bora pamoja na kuheshimu usiri wa mtu.
“Ni ukweli usiopingika kuwa waandishi wa habari wana nafasi kubwa kwa jamii hasa kipindi cha uchaguzi. Kwa kupitia taaluma yenu mna uwezo wa kulinda haki za binadamu ama kuwa sehemu ya uvunjifu wa haki hizo,”amesema Mcharo na kuongeza:
“Ni wajibu wa waandishi wa habari kulinda haki za binadamu kipindi chote cha uchaguzi,ili kutoa fursa kwa wananchi wenye sifa kutumia haki yao ya kikatiba kushiriki uchaguzi,”.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza(MPC),Edwin Soko,amewataka waandishi wa habari kuzingatia maadili,sheria na miongozo wakati wa kuripoti uchaguzi mkuu ili kuhakikisha unapita salama.
“Tutoe nafasi sawa,na kuandika habari kwa kuzingatia mizania na usawa kwa vyama vyote vya siasa kuelekea uchaguzi mkuu,ili watu wote waweze kunadi sera zao ili wananchi waweze kufanya maamuzi,”amesema Soko.

Sanjari na hayo Soko,ameiomba Tume hiyo kutumia jicho kuangazia madhira ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwa waandishi wa habari wanayoyapata hasa kipindi cha uchaguzi na kuja na mkakati wa namna ya kuyashughulikia.
Akitoa salamu kwa niaba ya Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Msataafu Mathew Mwaimu,Ofisa Uchunguzi -Sheria,Saumu Mgeni,amesema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa kwa waandishi wa habari na jeshi la polisi kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria wakati wa uchaguzi.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina