March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waandishi wa habari waombwa kuangazia jinsia katika mabadiliko ya tabianchi

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online 

Imeelezwa kuwa mabadiliko ya tabianchi si suala la mazingira pekee, bali pia ni hoja ya jinsia na haki ya afya huku wataalamu wakisema athari za mabadiliko ya hali ya hewa haziwaathiri watu wote kwa kiwango sawa, kwani wanawake na wasichana hukumbwa na changamoto kubwa zaidi kutokana na mifumo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa iliyopo.

Katika jamii nyingi, wanawake ndio wanaobeba jukumu la kutafuta maji, kutunza familia na kusimamia mahitaji ya kaya. Hali ya ukame, mafuriko au majanga mengine yanayochochewa na tabianchi huongeza mzigo huo na wakati mwingine kuwaweka katika hatari ya ukatili wa kijinsia au kupoteza fursa za kiuchumi na kielimu.

Kwa mujibu wa wadau wa afya na maendeleo, changamoto hizi hujitokeza pia katika eneo la afya ya uzazi, afya ya mama na mtoto, lishe na upatikanaji wa huduma za afya wakati wa dharura za tabianchi.

Hayo yamebainishwa Februari  12,2026 katika mafunzo  maalum  yaliofanyika kwa njia ya mtandao(zoom), yaliyoandaliwa  na  Media for Environment, Science, Health and Agriculture(MESHA) na kuwakutanisha  waandishi wa habari kutoka nchi sita za Afrika ikiwemo Kenya,Tanzania naUganda yenye  lengo la kuwajengea uwezo wa kuandika habari za kina na za uwajibikaji kuhusu mabadiliko ya tabianchi, matumizi sahihi ya data na tafiti za kisayansi pamoja na kufuatilia utekelezaji wa sera na ahadi za serikali.

Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo Mratibu wa Mawasiliano  na Ushawishi wa Kanda,Mission Inclusion Audrey Masitsa,amesema vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuunda uelewa wa umma na kushawishi vipaumbele vya sera kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi.

Audrey amesema,mabadiliko ya tabianchi hayana upendeleo wa kijinsia, lakini athari zake hutofautiana kati ya wanawake, wanaume na vijana. Hivyo, namna ambavyo habari zinaandikwa inaweza aidha kuendeleza ukosefu wa usawa au kusaidia kuleta mabadiliko chanya.

“Waandishi wa habari si watazamaji tu wa hatua za kukabiliana na tabianchi, bali ni sehemu ya mabadiliko hayo,” amesema.

Pia amesema,ufuatiliaji wa maudhui ya habari unaonesha kuwa masuala ya jinsia huingizwa kama kipengele cha kukamilisha taarifa, bila kuchambua mizizi ya ukosefu wa usawa kama vile ukosefu wa mitaji, nafasi za maamuzi na nguvu ya soko.

Hivyo  amewashauri waandishi kufuatilia safari nzima ya mabadiliko katika jamii, badala ya kuripoti tukio la mafunzo au warsha pekee.

 Hata  hivyo Audrey,amesema matumizi ya lugha yana mchango mkubwa katika kujenga mtazamo wa jamii akitokea mfano kauli kana  “wanawake walio hatarini” au “kuwawezesha wanawake” zinapaswa kufafanuliwa kwa ushahidi na muktadha.

Vivyo hivyo, katika matumizi ya picha, amewashauri waandishi  waoneshe  wanawake  katika nafasi za uongozi na utekelezaji wa shughuli, badala ya kuwaonesha katika majukumu ya kijadi pekee.

Amesema katika kuimarisha usimamizi shirikishi wa rasilimali za bahari na ukanda wa pwani, mradi wa ReSea Project unatekelezwa katika nchi za Kenya, Tanzania, Mozambique, Madagascar na Comoros,mradi huo unaongozwa na Mission Inclusion kwa kushirikiana na IUCN, kwa ufadhili wa Global Affairs Canada.

Amesema,lengo la mradi huo  ni kukuza suluhisho za asili linalozingatia jinsia, kuimarisha utawala wa bahari unaojumuisha jamii, na kuwezesha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika uchumi wa buluu.

“Wanawake   sasa wanaongoza kamati za usimamizi wa mikoko,hatua hiyo si tu inalenga kurejesha mazingira, bali pia inalinda fukwe dhidi ya mmomonyoko, kupanua vyanzo vya kipato na kuwajengea wanawake uwezo wa uongozi.Simulizi nyingi za vyombo vya habari bado huwaonyesha wanawake kama waathirika au wanufaika wa miradi, badala ya kuwa wabunifu na viongozi wa suluhisho,”amesema 

Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Martha Fatael,amesema  uandishi unaozingatia jinsia katika masuala ya tabianchi si utetezi bali ni usahihi wa taarifa kwa kuandika habari zilizo kamili na zenye muktadha hivyo amehimiza  vyombo vya habari  kuongeza uelewa kwa umma, kuchochea sera bora na kuangazia suluhisho linalotekelezwa katika jamii.

Naye Mkuu wa Hali ya Tabianchi(Climate Justice Lead) kutoka ActionAid International,Teresa Anderson, amesema ufadhili unaotilewa na Mfuko wa Fedha kwa Ajili ya Ubadilishaji wa Tabianchi(FRLD),wa dola milioni 250 ni dhaifu ikilinganishwa na mahitaji ya dola bilioni 395 kwa mwaka.

Hivyo mfuko unahitaji kupanuliwa haraka hadi dola bilioni 400 kwa mwaka, uwe na uwezo wa kusambaza fedha kwa haraka, kutoa ruzuku moja kwa moja kwa jamii, na kuwa kamili kwa madhumuni yake ili kukabiliana kwa ufanisi na mabadiliko ya tabianchi.