December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waandishi wa habari wanolewa kuhusu uharibifu wa mazingira

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Katika kuhakikisha suala la mazingira linapewa kipaumbele katika kuhifadhiwa na kutunzwa,jumla ya waandishi wa habari 40 nchini wanapatiwa mafunzo ya kuandika habari za uharifu(uharibifu) wa mazingira.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari za Kupinga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu Tanzania (OJADACT) Edwin Soko wakati wa mafunzo ya siku moja ya namna ya kuripoti habari za uchokonozi zinazohusu uhalifu wa mazingira kwa awamu ya kwanza yaliofanyika mkoani Mwanza yalioandaliwa na chama hicho kwa ufadhili wa shirika la Environmental Reporting Collective(ERC).

Soko, amesema mafunzo hayo yanafanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ni hiyo ilio fanyika mkoani Mwanza huku jumla ya washiriki 20 wamepata mafunzo hayo.

Ambapo awamu ya pili itashirikisha waandishi 20 kutoka mikoa mbalimbali nchini hapa ambayo yatafanyika Aprili 9 mwaka huu kwa njia ya mtandao hivyo kufanya jumla ya waandishi 40,kunufaika na mafunzo hayo.

Soko amesema,lengo la mafunzo hayo kwa waandishi wa habari ni kuwajengea uwezo, kubobea na kuwa chachu katika kuandika na kuripoti habari za uhalifu wa mazingira ili kuhakikisha taifa linakabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na yanayosababishwa na uharibifu wa mazingira.

Awali akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi,Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana Yonas Alfred,amesema suala la mazingira ni maisha ya wote na hakuna namna ya kulikwepa,hivyo waandishi wa habari wakibobea katika kuripoti suala la mazingira litakuwa na tija na maslahi kwa taifa na jamii.

Yonas amesema, serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia inatoa kipaumbele kwenye suala la mazingira ndio maana ipo sera ya mazingira na kanuni mbalimbali zinazosisitiza kutunza na kuhifadhi mazingira.

“Suala la uhifadhi wa mazingira kwa sasa ni ajenda ya kidunia,bila mazingira viumbe akiwemo binadamu kesho yetu haiwezi kukamilika,hivyo kuandika habari za uhifadhi wa mazingira ni jambo muhimu sana,hivyo napenda kuwapongeza OJADACT na ERC mmefanya jambo jema kuandaa mafunzo haya kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Mwanza,” amesema Yonas.

Amesema kuna mifano ilio wazi,kama Wilaya ya Nyamagana na Mkoa wa Mwanza una changamoto nyingi za kimazingira ikiwemo uvuvi haramu ndani ya Ziwa Victoria,ukataji ovyo wa miti kwa ajili ya shughuli za uchomaji wa mkaa.

Hivyo kutokana na changamoto hizo alitumia fursa hiyo kuwaomba waandishi walioshiriki mafunzo hayo kutumia elimu walioipata kuandika habari za uhifadhi wa mazingira na waende kufichua uharibifu huo wa mazingira kwa kutumia kalamu zao vizuri.

“Ni neema tumepewa mazingira,tumejikuta tuna Ziwa,misitu,wanyama na wazee wetu zamani walikuwa marafiki wa mazingira na yakawatunza,suala la mazingira na dawa za kulevya ni la kidunia kuandika habari kuhusu mazingira ni jambo zuri,Rais wetu analipa kipaumbe suala la uhifadhi wa mazingira na dawa za kulevya,”amesema Yonas.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Neema Emmanuel,amesema yamemsaidia kupanua wigo wa uelewa juu ya uharibifu wa mazingira hivyo elimu alioipata itamsaidia katika kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira na athari za uharifu uharibifu wa mazingira ili kuwa na taifa salama.

Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari za Kupinga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu Tanzania (OJADACT) Edwin Soko akizungumza wakati wa mafunzo ya siku moja ya namna ya kuripoti habari za uchokonozi zinazohusu uhalifu wa mazingira kwa awamu ya kwanza yaliofanyika mkoani Mwanza yalioandaliwa na chama hicho kwa ufadhili wa shirika la Environmental Reporting Collective(ERC).
Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana Yonas Alfred, akifungua mafunzo ya siku moja ya namna ya kuripoti habari za uchokonozi zinazohusu uhalifu wa mazingira kwa awamu ya kwanza yaliofanyika mkoani Mwanza yalioandaliwa na chama hicho kwa ufadhili wa shirika la Environmental Reporting Collective(ERC) kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana Yonas Alfred,( wa pili kulia walio kaa) huku wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa OJADACT Edwin Soko,wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya siku moja ya namna ya kuripoti habari za uchokonozi zinazohusu uhalifu wa mazingira kwa awamu ya kwanza yaliofanyika mkoani Mwanza yalioandaliwa na chama hicho kwa ufadhili wa shirika la Environmental Reporting Collective(ERC).