Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Waandishi wa Habari Wanawake kutoka Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), imewakumbuka watoto wenye tatizo la vichwa vikubwa na mgongo wazi,mkoani Mwanza kwa kuwatembelea na kutoa mahitaji mbalimbali.
Waandishi hao ambao wametembelea kituo cha Nyumba ya Matumaini (Hope of House),kilichopo Nyegezi wilayani Nyamagana mkoani hapa,ambako ndipo watoto hao wanapata huduma mbalimbali za malazi na chakula wakati wakisubilia matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando,ambapo waliungwa mkono na baadhi ya waandishi wa habari wanaume kutembelea kituoni hapo.
Akizungumza wakati wa zoezi la kukabidhi msaada huo,leo Machi 18, 2023,Katibu Mkuu wa MPC, Blandina Aristides, ameeleza kuwa utoaji wa msaada huo ni kutokana na uhitaji uliopo kwa watoto hao pia ikiwa ni njia moja wapo ya kusherekea siku ya Wanawake Dunia ambayo uadhimishwa ifikapo Machi 8, kila mwaka.
Ila walishindwa kuadhimisha siku hiyo kwa sababu ya msiba wa aliyekuwa Mhariri wa gazeti la Nipashe Kanda ya Ziwa Richard Makore,hivyo kusogeza mbele na kusherekea siku hiyo ya Machi 18,mwaka huu.”Tunatambua umuhimu wenu na tunawapenda,tumefanya kwa mara ya kwanza lakini tutaendelea kuja zaidi Mungu atakapo tujalia,tumekuja na hiki kidogo kutoka kwa wadau mbalimbali,”ameeleza Blandina.
Ametaja mahitaji waliotoa ni pamoja na mchele kilo 100, sukari kilo 50, sabuni za vipande boksi 10, mafuta ya kupikia dumu lita 40,juisi katoni 15 pamoja na mafuta kwa ajili ya kupaka mwilini katoni 2 vyenye thamani ya zaidi ya laki 8(800,000).Mratibu wa MPC, Laurancia Bernard, ameeleza kuwa lengo la kuwatembelea watoto hao ni kuwawezesha mahitaji kwa sababu ni wenye uhitaji sana kulingana na changamoto walizonazo za kichwa kikubwa na mgongo wazi.
“Kilichotusukuma kuja mahali hapa ni uhitaji wa watoto waliopo katika kituo hiki,sababu wengi wao ni wategemezi na wanahitaji mahitaji mbalimbali kama chakula ambao wengine wazazi wao wanashidwa kumudu gharama za matibabu,nawashukuru waandishi wa habari pamoja na wadau waliounga mkono kufanikisha jambo hili ikiwemo EWURA, TIRA, NBC, Jeshi la Polisi Mkoa Mwanza na Cecy Toto & Gift Shop ,”ameeleza Laurencia.
Mkurugenzi Cesy toto and gift shop Cecilia Aikaeli,amewapongeza waandishi wa habari wanawake kwa hatua hiyo ya kuwatembelea watoto hao wenye mahitaji maalumu.
Cecilia ameeleza kuwa katika kituo hicho ameona wanawake ambao ni mama wa watoto hao wenye umri mdogo hivyo ipo shida ambapo inahitaji elimu zaidi kwa wanawake wanapokuw a wajawazito kuwahi kliniki pia na kufuatilia taratibu zote wanazopewa na wataalamu wa afya.
Anaeleza kuwa mama asipotumia vidonge vya folic acid pamoja na lishe bora kunachangia mtoto kuzalisha akiwa na mgongo wazi au kichwa kikubwa hivyo elimu inahitajika zaidi ifike katika maeneo yote hususani vijijini.
“Wanapopewa vidonge vya folic acid wamezoe kwani wajawazito wengi awafuatilii wanadai kuwa vina harufu mbaya,vinaleta kichefuchefu wanafika nyumbani wanatupa wakati vinamsaidia kumtengeneza mtoto akiwa tumboni,”.
Kwa upande wake Meneja Nyumba wa Nyumba ya Matumaini , Getruda Butondo,amewashukuri waandishi wa habari wanawake kwa msaada huo huku akieleza kuwa kituo hicho kinapokea watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi wakiwa na wazazi wao kutoka maeneo tofauti tofauti ikiwemo Geita,Tabora, Mwanza,Simiyu.Kichwa kikubwa na mgongo wazi unaosababishwa na ukosefu wa madini ya folic acid ambapo wanawake wengi wanaotoka katika familia duni hivyo wanakosa lishe bora wakiwa wajawazito na wengi wao wanachelewa kwenda kliniki ili wapatiwe vidonge vya folic acid na malaria.
“Idadi ya watoto ambao wapo wengi sana ni Tabora,Bihalamuro,Kigoma na Musoma na idadi kubwa zaidi ni Mwanza kwa sababu huku changamoto ni kuwa tunapokea wazazi wengi ambao hawana uwezo wa kuwahudumia hao watoto huku wanawake wakiwa wametelekezwa,”.
Kituo hicho kilianzishwa ili kusaidia mama wa watoto hao sehemu ya kulala na chakula pamoja na watoto wakati wakisubilia matibabu Bugando kwani awali walikosa sehemu ya kujihifadhi pia wanawasaidia katika vipimo na matibabu huku serikali kupitia hospitali hiyo ikisaidia huduma ya upasuaji bure.
“Tulianzisha kituo hiki mwaka 2017 ambapo kwa wiki kituo kinapokea watu 60 ikiwemo wazazi na watoto wao huku kwa mwaka ni takribani watoto 600, ambapo idadi ya watoto imeongezeka sana kuanzia mwaka jana hii ni kutokana na elimu walioitoa hivyo mama akizaa mtoto mwenye matatizo hayo hamfichi,” ameeleza Getruda.
Naye mmoja wa wazazi wenye watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi Tausi Shija kutokea Mpanda mkoani Katavi ameeleza kuwa,moja ya sababu ya kupata mtoto mwenye tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi ni kutokana na kuchelewa kuhudhuria kliniki kwani alianza mimba ikiwa na miezi mitano hivyo nilichelewa kunywa dawa za folic acid.
“Tunawashukuru waandishi wa habari wanawake waliokuja kutupatia msaada,kwani kulea watoto wenye matatizo kama haya ni changamoto kubwa sana,”ameeleza Tausi.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba