November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waandishi wa habari waombwa kutumia kalamu zao kuisaidia serikali kuhamasisha jamii juu ya sensa

Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Waandishi wa habari wameombwa kutumia kalamu zao kuisaidia serikali katika kuhamasisha jamii juu ya sensa.

Zoezi la sensa na ya watu na makazi nchini hapa linatarajiwa kufanyika Agousti 23 mwaka huu,ambapo sensa ya mwisho kufanyika ilikuwa mwaka 2012.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Abubakar Karsan,wakati akifungua mkutano wa kupitia na kuthibitisha kanuni na maadili ya uandishi wa habari mtandaoni na vyombo vya habari vya kawaida uliofanyika mkoani hapa.

Karsan ameeleza, waandishi wa habari wawe chachu kuisaidia serikali kwa kuhamasisha na kuelimisha jamii umuhimu wa sensa kwa maendeleo ya taifa.

“Tutumie kalamu zetu kuisaidia serikali kushawishi na kuelimisha jamii kuhusu zoezi la sensa na umuhimu wake kwani watu wengi wanahusisha zoezi hilo na masuala ya chanjo ya uviko-19,”ameeleza Karsan.

Aidha amewataka waandishi wa habari za kuzingatia maadili ya uandishi wa habari kwa kutoandika habari zisizo na ukweli na zinazopotosha.

Sanjari na hayo Karsan ameeleza kuwa wanafanya jitihada za kuwawezesha waandishi wa habari wanawake kushika nafasi mbalimbali katika sekta ya habari.

Hata hivyo Karsan ametumia fursa hiyo kueleza waandishi hao wa habari kuwa anatarajia kustaafu kazi hiyo ifikapo Desemba mwaka huu baada ya kuitumika kwa muda wa miaka 19.

Amesema uamuzi wa kustaafu ameuchukua toka mwaka jana na hajashurutishwa na mtu bali anawaachia vijana kuendesha taasisi hiyo ambayo imeanza toka mwaka 2003.

“Tayari utaratibu za kumpata Mkurugenzi mpya atakayeiongoza UTPC umeshafanyika na baada ya kustaafu nitakuwepo nikimwangalia Mkurugenzi mpya kwa takribani miezi mitatu,” amesema Karsan.

Hata hivyo Mwezeshaji wa mkutano huo Pili Mtambalike,amewataka waandishi kuchapisha maudhui mazuri ambayo yatawasaidia kupata watu wengi.

Mkurugenzi wa UTPC Abubakar Karsan katika mkutano wa kupitia na kuthibitisha kanuni na maadili ya uandishi wa habari mtandaoni na vyombo vya habari vya kawaida uliofanyika mkoani hapa.(Picha na Judith Ferdinand)