March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waandishi wa habari wajengewa uelewa mabadiliko ya tabianchi kuelekea mkutano wa COP30

Na Martha Fatael,Timesmajiraonline,Morogoro

KUELEKEA Mkutano wa COP30 (Conference of the Parties) wadau wa mazingira wawakutanisha waandishi wa habari na wataalam mkoani Morogoro ili kujengewa uwezo kuhusu mabadiliko ya tabia nchi na umuhimu wa jukwaa hilo la kimatafa kwa Tanzania.

COP30 ni jukwaa kuu la kimataifa linalounganisha nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), likiwa ni mkutano wa 30 wa nchi zote zinazoshiriki katika mkataba huu. Kila mwaka, COP inakusanya viongozi wa serikali, wataalamu, wanahabari, mashirika yasiyo ya kiserikali, na sekta binafsi ili kujadili maendeleo, changamoto na hatua za pamoja za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani.

Meneja uendeshaji kutoka shirika lisilo la kiserikali Climate Action Network Tanzania(CAN), Bonaventure Mchomvu amesema Mkutano huo ni fursa ya kupanua ajenda za sera za kitaifa na kimataifa, kuangalia utekelezaji wa ahadi zilizofanywa katika mikutano ya awali, na kujadili jinsi ya kuongeza ushirikiano wa kifedha, teknolojia na utafiti ili kupunguza hewa chafu na kuongeza uthabiti wa jamii zinazokumbwa na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema mafunzo hayo kwa waandishi wa habari yamefanyika ili kuongeza uelewa, uwezo wa kuandaa habari za mkutano huo wa kimataifa kabla ya mkutano, wakati wa mkutano na baada ya mkutano huo kutokana na umuhimu wake kwa watanzania.

“Ukiangalia nchi imeondoka na maazimio ama malengo makuu Zaidi ya 12 ambayo wanakwenda kuyawasilisha kwa lengo la kuishirikisha dunia juu masuala ya mabadiliko ya tabianchi hasa katika ngazi ya kitaifa maana ni janga mablo lipo na litaendelea kuwepo maana halina mipaka ya kisiasa”amesema Mchonvu

Awali Akizungumza wakati wa kikao kazi hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa TMF, Dastan Kamanzi, amesema kikao hicho kimeandaliwa na Tanzania Media Foundation (TMF) kwa kushirikiana na Oxford Policy Management (OPM), kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Uingereza na Uswisi wakati huo CAN Tanzania ikitoa uelewa na uzoefu wa mabadiliko ya tabia nchi na mchakato mzima wa maandalizi ya COP30.

Amesema kikao kazi hicho chenye lengo la kufanyakazi shirikishi kwa kuwaleta waandishi wa habari pamoja na wataalamu ili kuandaa habari za maudhui takiwa na zenye tija yatakayokwenda sabamba na viwango vya ubora, zenye wingi wa kutosha.

“Mradi huu wa miazi minne, unalenga kuzalisha habari zenye maudhui ya mabadiliko ya tabia nchi mkutano ambao unatarajiwa kuanza 10-21 Novemba kwa kufuatilia mada mtambuka zitakazoibuka wakati wa COP na baada ya COP…hata hivyo kwa sasa tunahitaji kuandika kabla ya COP”amesema Kamanzi.

Nao walezi wa waandishi hao, Rashidi Kejo, Bakari Khalid na Said Mmanga  wamesema kikao kazi hicho waandishi wa habari wanayo kazi kubwa ya kuandaa habari zenye tija za kuwasaidia wtanzania kuelewa mkutano huo wa kimataifa zitakazoleta elimu kwa wananchi na uwajibikaji kwa mamlaka kuhusu COP30.

Nao baadhi ya waaandishi wa habari walioshiriki kikao kazi hicho, Restituta Nyondo, Arodia Peter na Denis Sinkonde wamesema kikao kazi hicho kimekuwa na manufaa kwani waandshi wa habari wamepata mafunzo, wameweka mpangokazi kwa pamoja na wataalamu ili kuleta uelewa na uzalishaji wa habari bora.

Mkutano wa COP30 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi unaotarajiwa kufanyika tarehe 10-21 Novemba 2025 mjini Belem, Brazil, ni sehemu ya mfululizo wa mikutano ya kimataifa inayofanyika kila mwaka chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) ikilenga kuwaleta pamoja viongozi wa serikali, wataalamu wa mazingira, mashirika yasiyo ya kiserikali, na sekta binafsi kujadili hatua za pamoja za kupunguza hewa chafu, kushughulikia athari za mabadiliko ya tabianchi, na kukuza ushirikiano wa kifedha na kiteknolojia kwa nchi zinazokabiliana na changamoto hizi na kila COP hufanyika katika nchi tofauti kila mwaka.

Mikakati na majadiliano katika COP30 yanajengwa juu ya matokeo ya mikutano iliyopita, mfano, COP29, iliyofanyika mwaka 2024 mjini Baku, Azerbaijan, ambayo ilikazia upunguzaji wa hewa ukaa, fedha za tabianchi, na ushirikiano wa kimataifa katika utekelezaji wa ahadi za kupunguza gesi chafu. Hii inafuatia mfululizo wa mikutano ya COP tangu 1995, ambayo kila mwaka huweka msingi wa sera, mipango na ahadi za pamoja za kupambana na mabadiliko ya tabianchi duniani.