Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Imeelezwa kuwa changamoto ya matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya zinatokana na sababu mbalimbali ikiwemo uelewa mdogo wa jamii juu ya tatizo hilo.
Hivyo Mwenyekiti wa Chama cha Kupinga Matumizi ya Dawa za Kulevya na Uhalifu nchini Tanzania (OJADACT) Edwin Soko,ametoa wito kwa waandishi wa habari kuelimisha jamii juu ya tatizo hilo.
Hayo ameyaeleza wakati Ojadact ikiadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya na usafirishaji haramu, yaliyofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza jijini hapa.
Soko ameeleza kuwa,dawa za kulevya hazina afya kwa jamii na ni nguzo mbaya ya kumomonyoa ustawi,ustarabu,mustakabadhi na umoja wa kitaifa kwa sababu zina athari kubwa.
Ameeleza kuwa wanawahimiza waandishi wa habari waandike zaidi habari za kuelimisha jamii isijaribu wala isitumie dawa za kulevya kwa sababu athari yake ni kubwa.
Hivyo vita dhidi ya dawa za kulevya ianze na waandishi wa habari kwa kuandika na wanafahamu habari ina nguvu na chombo cha habari kinawafikia watu wengi kwa wakati mmoja.
“Maadhimisho hayo duniani ufanyika kila ifikapo Juni 26,na sisi Mwanza tumefanya Juni 30 huku kitaifa yatafanyika Julai 2 mwaka huu jijini Dar-es-Salaam,kama chama tunahitaji waandishi wa habari waweze kuelimisha jamii sana juu ya athari za dawa za kulevya,”ameeleza Soko.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt.Thomas Rutachunzibwa, ameeleza kuwa matumizi ya dawa za kulevya zinaathiri ubongo wa binadamu ambao ndio injini katika mwili hivyo ukiathirika unamuelekeza kufanya jambo lolote.
Dkt.Rutachunzibwa ameeleza kuwa,madhara yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya ni kudhoofisha afya ya mtumiaji pamoja na kusababisha maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na homa ya in hasa kwa watumiaji wa dawa hizo kwa njia ya kujidunga ambao utumia sindano moja watu zaidi ya mmoja hivyo ni rahisi kwao kupata magonjwa hayo na mengine yanayoambukizwa kwa njia ya damu au maji maji.
“Wazazi wahakikishe wanashiriki katika malezi ya watoto wao Ili wakue katika maadili kwani familia inamchango mkubwa katika kuhakikisha watoto hawaingii kwenye matumizi ya dawa za kulevya na ikitokea wameingia basi familia impeleka katika vituo vya afya akapate tiba na elimu ili aweze kuachana na matumizi ya dawa za kulevya,wataalamu wa tiba hiyo wapo na waandishi pelekeni taarifa sahihi za kuelimisha jamii juu ya athari za madawa ya kulevya,”ameeleza Dkt.Rutachunzibwa.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa Methadone Mkoa wa Mwanza,Mratibu wa Afya ya Akili Mkoa wa Mwanza Dkt.Eunice Masangu,ameeleza kuwa athari za dawa za kulevya zinaweza kuwa za moja kwa moja au zisizo za moja kwa moja ambapo kimwili ni kupata magonjwa kama vile kifua kikuu(TB),homa ya ini B na C, Ukimwi/VVU.
Dkt.Masangu ameeleza kuwa madhara ya kisaikolojia ni pamoja na kufanya maamuzi yasiyo sahihi,hisia potofu,magonjwa ya akili,sonona na kuchanganyikiwa huku kijamii ni pamoja kuzorota kiutendaji,kukosa kazi,kushindwa kumudu masomo,umaskini, uhalifu kushindwa kujenga mahusiano katika familia na jamii.
“Tuna vijana wameacha kutumia dawa za kulevya,tunaishukuru serikali kwa kusogeza huduma za matibabu kwa jamii,”ameeleza Dkt.Masangu.
More Stories
Dkt.Tulia ashiriki ibada, asisitiza waumini kushiriki uchaguzi serikali za mitaa
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia