December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waajiri wakumbushwa kujiisajili, kuwasilisha michango WCF


NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, MWANZA

MKUU wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Amos Makalla ametoa wito kwa waajiri kujisajili na kuwasilisha michango katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa manufaa ya wafanyakazi pindi watakapopata changamoto za kuumia au kuugua kutokana na kazi.

Ameyasema hayo Mei 22, 2023 katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masalla wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya tathmini za ulemavu uliosababishwa na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi kwa madaktari wa mikoa ya kanda ya Ziwa ikijumuisha Mwanza, Kagera, Mara, Simiyu, Geita na Shinyanga katika ukumbi wa chuo cha BoT jijini Mwnaza.

“Ili uweze kunufaika na huduma au mafao yanayotolewa na WCF, ni lazima waajiri wajisajili na kuwasilisha michango ya wafanyakazi waliowaajiri.” Alifafanua.

Alisema hivi sasa wafanyakazi wanao uhakika wa kinga na kipato kutokana na majanga yanayosababishwa na ajali, magonjwa na vifo kutokana na kazi kufuatia uwepo wa Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi (WCF).

“Waajiri nao wanapata muda zaidi wa kushughulikia uzalishaji na uendelevu wa biashara zao na hivyo kuongeza tija inayopelekea kuongezeka kwa pato la taifa.” Alisema.

Aliwaasa washiriki kuwa waadilifu wanapotekeleza jukumu hilo la kufanya tathmini ya ulemavu utokanao na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi ili WCF iweze kutoa fidia stahiki na kwa wakati.

Alisema uwepo wa Mfuko wa Fidia ni hatua muafaka katika mazingira ya sasa ambapo serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea na kazi ikiwemo ya kujenga uchumi na hivyo kuwa na ongezeko kubwa la maeneo ya uzalishaji.

“Katika hali ya kawaida ongezeko litakwenda sambamba na ongezeko la matukio na athari zinazotokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi hivyo jukumu la WCF sio kulipa fidia pekee bali pia kushirikiana na wadau katika kubuni na kuendeleza mbinu za kupunguza au kuzuia ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.” Alisisitiza.

Awali akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar alisema mafunzo hayo ni sehemu ya hatua muhimu ya kuuwezesha Mfuko kutekeleza vyema jukumu la kufanya tathmini sahihi na hatimaye kutoa fidia stahiki pindi mfanyakazi anapoumia au kuugua kutokana na kazi.

“Katika mwaka huu wa fedha tayari tumetoa mafunzo kwa madaktari 85 na leo tunawafundisha madaktari 100 na hivyo watafanya idadi ya madaktari ambao tayari wamepatiwa mafunzo na WCF, ya kufanya tathmini za ulemavu uliotokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi kufikia 1,585 nchi nzima.”Alifafanua Dkt. Omar.

Akielezea zaidi umuhimu wa mafunzo hayo, Dkt. Omar alidokeza kuwa Madaktari ni kiungo muhimu, ni daraja baina ya Mfuko na wahanga wanaopata magonjwa au ajali zinazotokana na kazi.

“Madaktari hawa wakijengewa uelewa wa kuweza kujua na kubaini magonjwa yanayotokana na kazi, vilevile wakaweza kufanya tathmini za ulemavu, itawawezesha hawa wahanga kupata haki zao za fidia kwa wakati lakini kupata stahiki zao.” Alisisitiza.

Kwa upande wa madaktari wameishukuru Serikali kwa kuuwezwesha Mfuko kusimamia majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo.

“Ni matumaini yangu kuwa mafunzo haya yatatuwezesha kufanya majukumu yetu ya kuwahudumia wafanyakazi watakaopata changamoto za kuumia na au ulemavu kutokana na ajali na magonwja yatokanayo na kazi kwa usahihi zaidi>” Alsiema Dkt. Pasclates Ijumba kutoka Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Geita.

Aidha Dkt.Julieth Nkovabi kutopka Hospitali ya Bugando, alisema mbali na kupatiwa mafunzo hayo ya tathmini za ulemavu na magonwja yatokanayo na kazi, lakini pia wamepatiwa elimu ya uelewa wa namna ya kuwasilisha taarifa endapo mfanyakazi ataumia au kuugua.

“Na sisi watumishi wa afya tunakumbana na shida mbalimbali, magonjwa ya kuambukiza wakati tunapowatibu wagonjwa wetu, kwa hivyo ni fursa nzuri ya kuelewa hatua kwa hatua jinsi ya kuwasilisha taarifa.” Alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masalla
Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar
Mkurugenzi wa Uendeshaji WCF, Bw. Anselim Peter akiwasilisha mada ya mchakato wa madai ya fidia
Mkuu wa Huduma za Sheria WCF, Bw. Abraham Siyovelwa akiwasilisha mada ya Sheria iliyoanzisha Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.
Sehemu ya madaktari wanaoshiriki mafunzo hayo
Sehemu ya madaktari wanaoshiriki mafunzo hayo
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano WCF, Bi. Laura Kunenge akizungumzia utaratibu wa uendeshaji mafunzo hayo.
Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar (kulia) akizungumza jambo na Meneja Tathmini Dkt. Ali Mtulia