November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waajiri wa wafanyakazi majumbani washauriwa kutoa elimu ya hedhi salama

Na Judith Ferdinand,TimesMajira online,Mwanza

WITO umetolewa kwa waajiri wa wafanyakazi wa nyumbani kuwapa elimu inayohusiana na afya ya uzazi ikiwemo hedhi pamoja na kuwapatia taulo za kike,ili waweze kuepuka changamoto ya ukosefu wa hedhi salama.

Neema Jacob wa kwanza kulia akizungumza na Majira lilipotembelea Shirika la WoteSawa ambapo alitoa wito kwa waajiri wa mabinti wafanyakazi wa nyumbani kuwapatia elimu ya afya ya uzazi ikiwemo ya hedhi salama pamoja na taulo za kike mabinti wao wa kazi

Huku Serikali ikiombwa kuweka mazingira rafiki ya upatikanaji wa taulo za kike na kwa gharama nafuu kwa kuondoa kodi katika bidhaa hizo sanjari na kuhakikisha maji yanafika kwa asilimia kubwa maeneo yote hususani vijijini ili kusaidia mabinti kujisafisha kwa urahisi.

Wakizungumza na Majira katika ofisi za Shirika la WoteSawa linalojishughulisha na mabinti wafanyakazi wa nyumbani lililopo mkoani Mwanza,wamesema changamoto inayowakabili mabinti wafanyakazi wa nyumbani ni pamoja na ukosefu wa elimu juu ya hedhi salama na taulo za kike.

Ofisa Msimamizi wa Makao na Uwezeshaji wa Shirika la WoteSawa linalojishughulisha na mabinti wafanyakazi wa nyumbani, Demitila Faustine akizungumza kuhusu juu ya mabinti wafanyakazi wa nyumbani.Picha na Judith Ferdinand

Mmoja wa mabinti waliokolewa na WoteSawa Neema Jacob, amesema changamoto nyingi zinazowakabili wasichana wafanyakazi wa nyumbani wakati wakiwa katika siku zao ni pamoja na kukosa muda wa kumpumzika maana kazi ni nyingi na vifaa vya kutumia katika kipindi hicho vinakuwa shida na kupeleka binti kukaa mchafu mchafu.

Jacob amesema,kutokana na maumbile ya kike kuwa wazi ile damu inaweza kuwasababishia kansa au magonjwa mengine kwa sababu wamekuwa wakishinda na pedi au kitaambaa kimoja kwa siku nzima.

Pia amesema,mabinti wengi wafanyakazi wa nyumbani waajiri wao hawapatiwi elimu kuhusiana na afya ya uzazi ikiwemo ya hedhi salama kwani mabosi wengi huondoka asubuhi na kurudi usiku hata muda wa kuzungumza haupo.

“Unakuta kazi nyingi,watoto hawajala na bosi anarudi usiku na unakuta huna taulo za kike na chupi yenye ni moja,pengine mshahara haujapewa na ndiyo unautegemea upewe ndio uvae na ufanyie mahitaji mengine, inakuwa ni ngumu kupata taulo za kike,” amesema.

Hivyo ametoa wito kwa waajiri wa mabinti wa kazi wawe wanakaa na wasichana wao wa kazi na kuwapatia elimu kuhusu afya ya uzazi ikiwemo suala la hedhi ili kutengeneza hedhi safi na salama.

Kwanza wawapatie pedi safi ili kujikinga na magonjwa na wawapatie elimu kwa ufasaha ili wale walioenda kufanya kazi za ndani katika umri mdogo na bado hawaja anza kupata hedhi siku wakikutana na hali hiyo wajue ni kitu gani wafanye.

Pia ameiomba Serikali kuhakikisha maji yanapatikana kwa urahisi katika maeneo yote nchini hususani vijijini ili kumpa urahisi binti kuweza kufua na kujisafisha hata kama atatumia vitambaa wakati wa hedhi pamoja na kushusha bei ya taulo za kike kwa kuondoa kodi.

“Mimi ukweli ni kwamba nilikua natumia vitambaa na wakati mwingine nilikua nakaa navyo siku mbili maana inakuwa ni shida hata maji maana nilipokuwa nakaa maji yalikuwa mbali,kabla sijaja shirika la WoteSawa bosi alikuwa hajawai kunieleza kuhusu suala zima la hedhi alichokuwa anataka ni kazi tu,baada ya kufika kwenye shirika hili walinipatia elimu ya afya ya uzazi na salama walinishauri niwe nabadili pedi mara tatu kwa kutwa na niwe na jitahidi ninapoingia kwenye hedhi iwe siri yangu siyo kila mtu afahamu,” amesema Jacob.

Revina Thomas,amesema waajiri wanatakiwa kukaa na mabinti zao kuweza kuwajenga na kuwapatia elimu kuhusu hedhi na mambo gani akiingia katika hedhi anatakiwa aweje,abadilishe pedi mara ngapi maana hapaswi kukaa nayo kuanzia asubuhi mpaka jioni.

“Kwangu mimi ilikuwa ngumu sana sikuweza kutambua hii kitu natakiwa kiweje baada ya kuokolewa na WoteSawa na wakanipatia elimu ya kuwa nikiwa katika kipindi hichi nifanyeje wamenijenga sana na sasa najitambua kuwa napaswa kukaa na pedi kwa muda gani,nibadilishe mara ngapi na niwe kwenye hali ya usafi na kutambua kuwa nikikaa na pedi muda mrefu naweza kupata madhara baadae,”amesema Revina

Pia amesema,serikali iweke mazingira rahisi ya upatikanaji wa taulo za kike hususani maeneo ya vijijini kwani wengi wao wana hali duni ambapo fedha ambayo ingetumika kununulia pedi ndio hiyo ambayo inawasaidia kununua chakula ambapo unakuta wanamudu kutumia vitambaa ambavyo navyo unakuta vinamuda mrefu
na vimeisha chakaa lakini anaendelea kutumia kwa sababu yote yanasababu ya kutokuwa na uwezo na zishushwe gharama.

Kwa upande wake Ofisa Msimamizi wa Makao na Uwezeshaji wa Shirika la WoteSawa Demitila Faustine, amesema shirika hilo limekuwa mstari wa mbele kwa kuwapa taarifa mabinti na wakina mama wanaofanya nao kazi kuhusu afya zao ambayo tumekuwa tukitoa kwenye makao tunamfahamisha aweze kufahamu masuala ya hedhi salama pamoja na kuwapatia taulo za kike ambazo zipo za kutosha.

Pia wameenda mbali zaidi ambapo wamekuwa wakienda shuleni ambapo tumekuwa tukitoa taulo za kike pamoja na elimu kwa wasichana ambao wapo shule kwani tunaamini kuna wasichana ambao wapo shule ya msingi akimaliza darasa la saba baadae anaweza kwenda kuwa mfanyakazi wa nyumbani.