Mwandishi wetu
Uongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) umekutana na waagizaji na wasambazaji wa dawa za binadamu za moyo ili kujua changamoto zinazowakabili na jinsi ya kuzitatua ikiwa ni kuboresha upatikana wa dawa kwa wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
Kikao hicho cha wadau hao kilifanyika hivi karibuni katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam ambapo wawakilishi zaidi ya 30 kutoka kampuni mbalimbali za dawa walihudhuria.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi alisema lengo la kukutana na wadau hao ilikuwa ni kuangalia changamoto zinazowakabili na namna ya kuzitatua.
Prof.Janabi ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema ukikosa dawa za moyo unahatarisha maisha ya mgonjwa hivyo basi kujenga uhusiano na wadau hao ni jambo la muhimu. Siku za nyuma mawasiliano yao yalikuwa kwa kupitia mitandao (barua pepe), simu na sio kuonana uso kwa uso kama ilivyotokea katika kikao hicho wameweza kufahamiana jambo ambalo litawasaidia katika utendaji wao wa kazi wa kila siku.
“Kulikuwa na changamoto za mawasiliano, kutokufuatwa kwa taratibu za kuagiza dawa, kutokufahamu maoteo ya dawa sawa sawa, kutoletwa dawa zote kamili kama zilivyoagizwa haya yote tumeyazungumzia na kupata utatuzi. Katika Taasisi yetu hatukuwa na matatizo ya upatikanaji wa dawa kwa asilimia 85, ninaamini baada ya kikao hiki tutakuwa na uhakika wa upatikanaji wa dawa kwa asilimia 100 na mgonjwa atapata dawa zote alizoandikiwa na daktari”.
“Tutakuwa na maoteo ya dawa sahihi zaidi baada ya mazungumzo yetu, kwani ukiwa na dawa za kutosha kwa kipindi cha miezi 3 hadi 4 na ikifika katikati ya miezi miwili ukaagiza zingine una uhakika wa kuwa na dawa za kutosha muda wote. Haya ni baadhi ya mambo ambayo tumekubaliana”, alisema Prof. Janabi.
Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema tangu kuanzisha kwa Taasisi hiyo sasa ni mwaka wa sita na hii ni mara ya kwanza kuwa na mkutano na wasambazaji wa dawa. Wamekubaliana kadri hali itakavyoruhusu watakutana angalau mara moja kwa mwaka.
“Sisi tunanunua dawa zetu kutoka Bohari ya Dawa (MSD) kama MSD hawana baadhi ya dawa tunazohitaji tunatangaza zabuni hivyo basi hawa waigizaji na wasambazaji wa dawa ni wadau muhimu kwetu”, alisisitiza Prof. Janabi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi cha Taasisi hiyo Bunare Danieli aliwajulisha washiriki kuwa ununuzi wa umma unaongozwa na Sheria ya Ununuzi wa Umma Na.7 ya mwaka 2011 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2013 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2016. Hivyo, aliwaasa wajumbe hao kuifahamu vyema sheria hiyo na kuizingatia wakati wote wanaposhiriki katika zabuni za umma na utekelezaji wa mikataba.
Aidha, aliwakumbusha kushiriki mafunzo mbalimbali ya Sheria ya Ununuzi wa Umma yanayoandaliwa na taasisi zilizothibitishwa kutoa mafunzo hayo hapa nchini.
Bunare pia aliwakumbusha watoa huduma hao kuwa kuanzia Januari, 2020 Ununuzi wa Umma ulianza kufanyika kupitia Mfumo wa Kielektroniki (Tanzania eLectronic Procurement System – TANePS). Mfumo huo una lengo la kuongeza ufanisi na uwazi katika ununuzi wa umma.
“Changamoto kadhaa zinazotukabili wakati wa utekelezaji wa mikataba ya ununuzi ni pamoja na ucheleweshaji wa bidhaa tofauti na muda ulioainishwa kwenye mkataba hali inayosababisha Taasisi kukosa dawa na malipo kwa wazabuni kuchelewa, baadhi ya wazabuni wanawasilisha mahitaji nusu nusu badala ya kuwasilisha kwa pamoja na pia wazabuni wamekuwa wakichanganya oda zaidi ya moja kwenye hati moja ya madai bila kutoa maelezo yanayojitosheleza”, alifafanua Bunare.
Nao waingizaji na wasambazaji wa dawa walishukuru kwa mkutano huo ambao umeonesha ni jinsi gani Taasisi hiyo ina nia ya kufanya nao kazi na kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati sahihi na kuziomba Taasisi zingine kuiga mfano huo.
Wazabuni wengi walionesha nia ya kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kurekebisha kasoro zilizoainishwa kwenye kikao hicho kwa lengo la kuhakikisha wao pia wanakuwa sehemu ya mafanikio ya Taasisi hiyo.
Emmanuel Kasembe mwakilishi kutoka kampuni ya Laborex Tanzania Ltd alisema kuitishwa kwa mkutano huo kunaonesha ni jinsi gani Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamejipanga kuboresha huduma za matibabu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati sahihi
“Changamoto kubwa tuliyokuwa tunakutana nayo ni jinsi ambavyo tenda ilikuwa inatangazwa kwa muda mfupi na utunzaji wetu wa kumbukumbu. Katika mkutano huu maelezo ya kina yametolewa ya jinsi ya kukabiliana na changamoto hizi na ninaamini tutakuwa na matokeo bora zaidi katika utendaji wetu wa kazi”, alisema Kasembe.
“Mkutano huu umesaidia kujenga na kuimarisha uhusiano kati yetu na JKCI. Ninaomba uendelee kuwepo kwani tumeweza kuzifahamu changamoto zinazowakabili JKCI nasi pia tumesema changamoto zetu na kufikia muafaka. Hii itatusaidia kuimarisha huduma za usambazaji wa dawa tunazozitoa siyo tu JKCI hata katika maeneo mengine”, alisema Jackline Mally kutoka Horizon Pharmacy Ltd.
“Kitu kizuri kwa Taasisi hii wanalipa madai yetu kwa wakati ndio maana leo unatuona tupo hapa makampuni zaidi ya 30 lakini hamna mwenye kuidai Taasisi hii”, alipongeza Rupesh Pillai Mkurugenzi Mtendaji wa Philips Pharmaceutical (T) Ltd.
More Stories
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi