Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
TAASISI ya Elimu ya Juu na Vyuo na Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO), imeandaa tamasha la burudani ya muziki na komedi kwa wanafunzi wote wa Mkoa wa Dar es Salaam likalofanyika katika Viwanja vya Taasisi ya Uhasibu (TIA) Kurasini jijini Dar es Salaam.
Kamishna wa Michezo na Burudani wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO), Sixbert Sitta, ametangaza hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema lengo la tamasha hilo kubwa kuwahi kutokea nchini, kuwakaribisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliojiunga na vyuo vikuu katika mkoa wa Dar es Salaam, kuwaleta pamoja wanafunzi wote wa vyuo kwaajili ya kukutana pamoja kubadilishana mawazo na kufahamiana.
“Sote ni mashaidi kuwa wanafunzi tunapoingia vyuoni tunakuwa na kipindi kifupi cha kuwa pamoja kwa miaka kuanzia mitatu hadi mitano na mara nyingi tunafikiria kuwa ‘busy’ na masomo bila kujihusisha na mambo ya burudi na michezo hali inayosababisha kutofahamiana baina ya chuo na chuo na wakati mwingine kumaliza miaka mitatu bila kutembelea chuo kingine ilihali wapo mkoa mmoja.
“Sisi kama TAHLISO tumeona si sawa ni vyema sasa tukawa kitu kimoja kwa kufanya jambo kubwa badala ya kila chuo kuandaa ‘Welcome First Year’ yake,” amesema Sitta.
Ameendelea kusema kuwa, anaamini kupitia tamasha hilo, litaenda kufungua fursa za wanafunzi kushirikiana kwenye mambo mbalimbali yakiwamo ya elimu na kijamii, baina ya chuo na chuo, kujenga umoja na kupanua mtandao wa wasomi hata baada ya kuhitimu masomo.
Aidha, amesisitiza zaidi kuwa, “Kama ambavyo tunafahamu Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia suluhu Hassan, ambavyo imekuwa ikihamasisha na kuunga mkono sekta ya michezo na burudani nchini, ni vyema kama wasomi kuangalia pia fursa hizo kupitia vipaji mbalimbali tulivyonavyo li tunapohitimu masomo wengine tupate fursa za kujiajiri kupitia vipaji tulivyonavyo.”
Amesema mbali na mafikio ya serikali katika sekta yaa michezo pia sekta ya elimu serikali imefanikiwa kuboresha mitaala, kutoa elimu bure kuanzia shule za msingi hadi sekondari, waliokatishwa masomo kwasababu za ujauzito kurejea shuleni, mabweni kujengwa na miundombinu mingine, walimu wamepandishwa madaraja na wanafunzi wa vyuo vikuu wananufaika na mikopo kwa idadi ya wanufaika kuendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.
Naye Rais wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),Tyson Lucas Kwigendaho, amesema tamasha hilo linafanyika kwa kushirikiana na Tanzania Leo, M-Media na Clouds Media.
Amesema tamasha hilo linalojulikana kama UNIFEST 255, litakalofanyika siku ya Jumamosi ya Tarehe 23, Novemba, mwaka huu, katika Viwanja vya TIA Kurasini, kuanzia saa 11:00 jioni hadi saa 6:00 usiku.
Amesema kabla ya tamasha hilo watafanya ziara katika vyuo vikuu vyote mkoani humo ili kuelezea umuhimu wa tukio hili kwa wanafunzi wote.
Naye Rais wa TIA na mwenyeji wa tamasha hilo, Charles Macelo, amesema chuo hicho kipo tayari kupokea wanafunzi hao zaidi yaa 10,000 wanaotarajiwa kushiriki na kuwataka kujitokeza kwa wingi.
More Stories
Msuya aipongeza SMZ kwa kufadhili wanafunzi 200
AU yaipatia Tanzania Dola za Kimarekani 200,000 mchango Maafa Hanang
NIC yazindua msimu wa pili kampeni ya NIC KITAA