Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Vyombo vya Ulinzi na Usalama nchini vimetakiwa kuongeza usimamizi wa sheria na tochi barabarani ili kunusuru wananchi kupata ajali huku Watanzania wakitakiwa kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile wakati akifunga semina ya siku tano ilioanza Novemba 27 hadi Desemba 1,mwaka huu ya Kanda ya Afrika kuhusu mpango wa usalama barabarani iliokutanisha nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania,Afrika Kusini,Burundi ,Rwanda Botswana iliondaliwa na Shirika lisilo la kiserikali linalohusika na utoaji wa elimu ya usalama barabarani la Tanzania Safety Roads Initiatives(TARSI) iliofanyika jijini Mwanza.
“Juzi mlisikia treni imegongana na gari Dodoma tena Singida na kila sehemu tunasikia ajali niwaombe wenzangu wa vyombo vya usalama tafadhali ongezeni kusimamia sheria ya usalama barabarani ni mara 1000 mlaumiwe kwamba mmezidisha tochi kuliko taifa tuendelee kushuhudia wasio na hatia,nguvu kazi , wazazi na Watanzania wenye nguvu wanazidi kufariki na kuacha watoto wasio na hatia,”amesema Kihenzile.
Pia ameeleza kuwa vijana hao wazalendo wa TARSI baada ya kuona hali ngumu ya ajali nchini wakaamua kuanzisha taasisi hiyo kwa ajili ya kutoa elimu nchini pia kupitia semina hiyo kwa ajili ya kujadiliana namna ya kukabiliana na ajali katika nchi hizo.
“Kila siku tunasikia ajali nchini hapa,watu wanakufa,wanavunjika ,vyombo vinaharibika athari kubwa kwenye nchi tunapata siyo nchi yetu tu hata nchi zingine hivyo wenzetu waliamua kuita nchi zaidi ya 27 ili kujadiliana ya namna gani ya kuenenda na hali ya ajali katika nchi yetu na nchi nyingine hivyo nimeunga.mkono jambo hili,”amesema Kihenzile.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TARSI Maliki Barongo, ameeleza kuwa muitikio ulikuwa mzuri kwa washiriki pia kutokana semina hiyo imeonesha nchini kuna uhitaji mkubwa wa kuwa na mada kama hizo kuhusu usalama barabarani.
Barongo ameeleza kuwa utofauti uliopo nchini hapa na nchi nyingine ni ujenzi wa miundombinu ambao ni barabara.
“Kwa sababu kwa wenzetu watu wakijenga barabara wanahakikisha kwamba viwango vya kimataifa kwa kila barabara vinakuepo kuanzia kwenye mchoro mpaka kwenye kuweka alama za barabarani kwa kwetu hapa wajenzi wengi wanajenga mwisho wa siku hawafikii mwisho wa barabara inayohitajika kimataifa,”amesema Barongo.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa,ameipongeza taasisi hiyo kwa kuandaa semina hiyo ambayo na Askari wamepata kushiriki hivyo Jeshi hilo limepata ujuzi katika kubadilishana mawazo kutoka nchi mbalimbali kujua mataifa mengine yanafanyaje kudhibiti ajali.
“Tumepata uzoefu wa kusaidia kuboresha kazi zetu za usimamizi wa sheria maelekezo ya Naibu Waziri tumeyapokea ya kusimamia sheria, taratibu na kanuni za usalama barabarani pasipo kuogopa lawama na kweli katika kipindi hiki lazima hatua madhubuti zichukuliwe kwa watu wanaovunja sheria,”amesema Mutafungwa.
Pia ameeleza kuwa kundi la bodaboda linachangamoto zake lakini mikakati iliopo ni mikubwa katika kuwabadilisha kifikra ili waweze kufuata sheria za usalama barabarani sababu ajali ikitokea haimbagui yeye.
“Ajali ikitokea wakati mwingine Ina gharimu maisha yake,majeraha pia wanaleta shida kwa wengine,tunazidi kuwaelimisha tunazani katika hatua tunazokwenda nazo za kuwaelimisha zaidi wakati mwingine usimamizi wa sheria zaidi tutafika mahali na sisi tutakuwa kama maeneo mengi,”amesema.
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
HAYA HAPA MATOKEO YOTE FORM II NA DARASA LA IV
Ufaulu waongezeka matokeo ya Darasa la Nne na Kidato cha Pili