January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vyombo vya habari viwe mstari wa mbele kufichua ukatili kwa wazee

Na Catherine Sungura-TimesMajira online,Dodoma

VYOMBO vya habari nchini vimetakiwa kuwa mstari wa mbele kusaidia kufichua uovu na pia kuelimisha jamii kuondokana na mila potofu zinazosababisha vitendo vya ukatili kwa Wazee na wote wasio na hatia.

Waziri wa Afya Dkt.Dorothy Gwajima akiongea na wazee pamoja na wataalam wa wizara mbalimbali wanaoshughulikia masuala ya wazee.

Rai hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa kikao kazi cha kujadili uratibu wa masuala ya wazee kilichowajumuisha wizara mbalimbali pamoja na vyama na wadau wanaohusika na wazee nchini katika ukumbi wa wizara jijini Dodoma.

“Vyombo vya habari vitusaidie kufichua uovu,Serikali kwa upande wake itaendelea kushirikiana na wadau kutoa elimu kwa jamii kuachana na imani potofu zinazochangia ukiukwaji wa haki za wazee ikiwemo haki ya kuishi” amesisitiza.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika ya Wazee Tanzania(TOP) Coldita Kokupima akiongea wakati wa kikao kazi hicho.

Hata hivyo Dkt.Gwajima amesema wizara yake haitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa wale wote watakaopatikana na hatia ya kuwakosesha wazee haki zao sanjari na mauaji dhidi yao.

“Cha msingi tupeane tu taarifa maana tatizo taarifa nyingine zinafichwa ama kuchelewa kutufikia sasa tutakomeshaje lakini kubwa elimu iende kwa kasi kwani mauaji hayakubaliki” amesema.

Picha ya pamoja ya Waziri wa Afya na viongozi wa Wazee,wadau na wataalam wa wizara mbalimbali mara baada ya kufungua kikao kazi kwenye ofisi za wizara jijini Dodoma.

Dkt. Gwajima amesema licha ya mafanikio yaliyofikiwa na serikali lakini bado inaonekana kuwa upatikanaji wa huduma na ustawi wa wazee bado ni tatizo kwa msingi huo katika kupambana dhidi ya mapungufu na udhaifu wa matunzo kwa wazee serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Sera, Sheria, Mikakati na Miongozo katika kuboresha huduma na ustawi wa wazee katika jamii.

“Kamishna wa ustawi wa Jamii nilishasema hili tunapaswa kuja na mkakati kabambe wa kukomesha mauaji ya wazee kwa kujenga mazoea ya kukaa vikao ngazi ya familia, mtoto ukimsimulia mambo mazuri na mabaya atakua na uwezo wa kuyapambanua ili atakapofika umri mkubwa akiambiwa huyu mzee ni mbaya atakataa kuaminishwa na mtu mwingine na hivyo kutokufanya mauaji” ameongeza Dkt. Gwajima.

Baadhi ya wazee wakimsikikiza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakati wa kikao kazi hicho.

Aidha,Dkt.Gwajima amezitaka halmashauri zote nchini ambazo hazijawatambua wazee na kuwapatia vitambulisho vya matibabu kwenye maeneo yao wafanye hivyo mara moja na pia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wateue waratibu wa wazee ili kuweza kuwasaidia katika upatakanaji wa matibabu kila eneo.

Hadi kufikia Desemba 2020 jumla ya wazee 1,897,162 walitambuliwa na kati yao wazee 1,042,403 walipatiwa vitambulisho vya kuwawezesha kupata huduma ya matibabu bila malipo kwa mujibu wa Sera ya afya ya mwaka 2007.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Mtandao wa Mashirika ya Wazee Tanzania (TOP),Clotilda Kokupima amesema wamemshukuru Waziri wa Afya kuitikia wito wao wa kukaa pamoja na kujadili masuala ya wazee na kwamba matumaini yao changamoto za wazee zitashughulikiwa ikiwemo kutungiwa sheria, Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 pamoja na huduma za afya hususan upatikanaji wa dawa kwa wazee.

Kokupima ameomba vitambulisho vya wazee vya kutibiwa bure viweze kuongezwa eneo ili mzee anapougua nje ya mkoa wake aweze kupata huduma mahali popote nchini wakati wanasubiri bima ya afya kwa wote.

Naye Dkt.Edwin Mng’ong’o kutoka Shirika la HelpAge International amesema wazee wanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa huduma za afya, upatikanaji wa kipato pamoja na usalama wa wazee hata hivyo wanaishukuru serikali kwa hatua zilizochukuliwa hadi sasa mauaji ya wazee yamepungua tofauti na zamani ambapo kwa mwaka takribani wazee mia tano walikua wakiuwawa nchini.

-Mwisho-