Na Hamisi Miraji, Timesmajira Online
WAANDISHI wa habari ni wahudumu wa jamii lakini si wanasiasa kwa tafsiri ya kawaida ya neno hilo, ingawa jukumu lao la kijamii lina uzito wa kisiasa.
Maadili ya msingi wa kazi yao ya kiweledi ni maadili ya ulimwengu mzima: amani, demokrasia, uhuru, mshikamano, usawa, elimu, haki za binadamu, haki za wanawake, haki za watoto, maenndeleo ya kijamii, nk. Hivyo kazi yao inachangia kuleta mabadiliko ya kijamii na kisiasa.
Mwanahabari ni nani?, ni mtu aliyesomea na kuhitimu taaluma ya uanahabari. Ni mtu anayeelewa mbinu, mikakati, michakato, kanuni na hata kinga za kukusanya, kuchakata na kusambaza habari kwa njia inayoweza kuridhisha hadhira yake.
Mwanahabari anaweza kutumia mifumo anuwai kufikisha zao lake kuu, ambalo ni habari, kwa hadhira. Anaweza kutumia maandishi; akachapisha gazeti, jarida au vipeperushi kwenye nyezo za jadi au za kisasa kama vile mitandao.
Lakini pia, anaweza kutumia sauti pekee au mseto wa sauti na video, au mbinu mahuluti ya maandishi, video, sauti, picha, michoro, data na kadhalika.
Wapo wanahabari wa mbinu mahuluti ambao kwa Kiingereza wanaitwa ‘multimedia journalist’.
Hivyo Waandishi wa Habari wana majukumu muhimu sana nchini, yakiwemo kuwataarifu, kuwaelimisha na kuwaburudisha wananchi,
Kwa kuzingatia hilo Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambegele, anasema waandishi wa habari wamekuwa kiungo kikubwa kupitia taarifa za habari, vipindi na makala katika kutoa elimu ya mpiga kura.
Anasema elimu hiyo ni muhimu kuwafikia walengwa kote nchini ili waweze kupata taarifa ya nini wanapaswa kufanya kwa mustakabali wa Taifa.
Jaji Mwambegele ameyasema hayo hivi karibuni kwenye mkutano wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam.
“Tunawasihi muendelee kutuunganisha na wadau. Tume itaendelea kuweka milango wazi kwa ajili ya kutoa taarifa za mara kwa mara.
“Wananchi wanapaswa kupata taarifa sahihi kuhusu kujiandikisha na umuhimu wake, hivyo Tume imejikita katika kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa ili uboreshaji uwe wa mafanikio,” anasema Jaji Mwambegele.
Hata hivyo anasema, katika Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kuna Mifumo miwili itatumika ukiwemo wa (VRS) Mfumo Mkuu na (OVRS) ikiwa ni mfumo kwa njia ya mtandao.
Anasema, mifumo yote miwili itahusisha fomu tatu, Namba moja, Kuandikisha wapiga kura wapya, Namba 5A wanaoboresha taarifa zao, wanaohama vituo, waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika, na namba 5B kuondoa taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa za kuwepo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Uandikishaji wa wapiga kura utahusisha uchukuaji wa alama za vidole vya mikono, picha na saini na kuhifadhiwa kwenye kanzidata ya wapiga kura.
Aidha, anasema uboreshaji wa Daftari wa mwaka 2024/2025 utatumia teknolojia ya BVR Kits zilizoboreshwa kwa kuwekewa program endeshi ya kisasa zaidi.
Kuelekea zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini itakayoanza Julai 20 mwaka huu, waaandishi wa habari wametakiwa kutumia majukwaa yao kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kuwa wapiga kura.
Lakini pia, kuboresha taarifa zao katika Daftari hilo ili waweze kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowataka.
Mkurugenzi wa Huduma za Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi Andrew Kisaka anasema, waandishi wa habari wamekuwa nyenzo muhimu ya upatikanaji wa tarifa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari.
Hivyo zina wajibu wa kushirikiana na Tume kwa ukaribu zaidi hususani katika wakati wa kabla na kipindi cha uchaguzi.
Akizungumzia nafasi ya vyombo vya habari upande wa utangazaji, Mhandisi Kisaka anasema utangazi kwa nia ya redio ndio wenye kufikia watu wengi zaidi na kusikilizwa kuliko chombo chochote cha mawasiliano.
“Hii ni kwa sababu ya unafuu wa ‘bei za receiver’ ambapo wananchi wa hali ya chini kiuchumi, hali ya kati na juu wanaweza kumudu kununua chombo hiki na kupata taarifa
“Watu wengi huweza kusikiliza matangazo kupitia redio kwa vile huweza kuendelea kufanya shughuri zao zingine za kiuchumi huku wakisikiliza matangazo kupitia redio. Hivi sasa matangazo kwa njia ya redio nchini (FM), yanafikia asilimia 75 ya watu,” anasema Mhandisi Kisaka.
Majukumu ya vyombo vya Utangazaji
Akizungumzia majukumu ya utangazaji kwa njia ya Televisheni Mhandisi Kisaka anasema Televisheni hupendwa na watu wengi kwa sababu ya kuweza kusikia pamoja na kuona mwenendo wa matukio yanayoendelea
Hata hivyo, anasema tofauti na redio, bei za televisheni ni kubwa hivyo kufanya watu wachache kumiliki ‘TV sets’, pia viwango vyake vimeuhishwa (Global harmonisation of standard)
Aidha, Mhandisi Kisaka amezungumzia wajibu wa vyombo vya Utangazaji kuwa, sera ya utangazaji ya mwaka 2003 inaitambua sekta hiyo kuwa ni sekta ya huduma kwa jamii ambayo huduma inayotolewa inatambulika kama haki ya msingi ya raia kama inavyotamkwa kwenye katiba ya Jmhuri ya Muungano wa Tanzania 1977. ibara ya 18.
Anasema Dhima ya sekta ya habari na utangazaji katika jamii ni kutoa habari, kuelimisha na kuburudisha kupitia vyombo vya habari na utangazaji.
Mhandisi Kisaka anasema, vyombo vya Utangazaji vinashauriwa kufahamu kwa ukamilifu sheria na kanuni zinazotoa miongozo ya mchakato mzima wa uchaguzi lakini pia kutenga vipindi maalumu kwa ajili ya kutoa elimu masuala ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na ile inayohusu oboreshaji wa daftari la kujiandikisha kupiga kura.
Vilevile anasema, vipindi vya uchaguzi kutengewa muda ambao ni ‘prime time’ ambao wasikilizaji hadira kubwa inakuwa ipo nyumbani, kukaribisha wataalamu mbalimbali kutoa elimu, kuifahamu hadhira unayoipelekea habari.
Hivyo, Vyombo vya Utangazaji ni nguzo muhimu sana ya mafanikio katika mchakato mzima wa kuelekea kwenye uchaguzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (Maelezo), Patrick Kipangula anaelezea maadili ya uandishi wa habari hasa wakati wa uchaguzi.
Anasema, Tume inatarajia kupata ushirikiano mkubwa zaidi kutoka kwa waandishi huku akiwataka kuzingatia sheria, kanuni, miongozo, taratibu na maelekezo wakati wa kuwafikishia wananchi taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
Kipangula anasema Vyombo vya habari vina nafasi kubwa na muhimu sana katika mchakato mzima wa uchaguzi, kuanzia kipindi cha maandalizi, wakati wa Kampeni, siku ya kupiga kura hadi baada ya matokeo kutangazwa.
Anasema, katika kipindi chote hicho vyombo vya habari nina jukumu la kutoa habari za kweli na sahihi, kutoa fursa sawa kwa wagombea wote na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la kidemokrasia.
Maadili ya Vyombo vya Habari wakati wa mchakato wa Uchaguzi
Akizungumzia hilo Kipangula anasema, Vyombo vya habari vina wajibu wa kutoa taarifa za ukweli na sahihi kwa umma wakati wote wa uchaguzi, kupotosha au kutoa taarifa zisizo sahihi kunaweza kusababisha hofu, kuchochea ghasia na kupunguza imani ya wananchi kwa mchakato wa uchaguzi.
Lakini pia, habari itaonekana kuwa ni ya ukweli iwapo hoja za tukio au suala husika zinaeleweka kikamilifu na kuonesha uhalisia wa tukio/jambo lenyewe kama ilivyoelezwa na pande zote zinazohusika katika suala la msingi.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 16 (5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Na. 1 ya Mwaka 2024, Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utakuwa mara mbili kati ya kipindi kinachoanza mara baada ya uchaguzi mkuu na kabla ya siku ya uteuzi. na wanaohusika katika zoezi hili ni wananchi ambao: –
1.Wametimiza umri wa miaka 18 na kuendelea ambao hawakuandikishwa hapo awali;
2.Watakaotimiza miaka 18 kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025;
3.Waliojiandikisha awali na wamehama Kata au Jimbo moja kwenda jingine;
4.Waliopoteza sifa mfano wale waliofariki kuondolewa katika Daftari;
5.Wenye taarifa zilizokosewa wakati wa uandikishaji; na
6.Waliopoteza au kadi zao kuharibika.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC)pia imetoa wito kwa waandishi wote wa habari kutumia majukwaa, taasisi na mashirika yao kuhamasishana kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia