November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vyama vya siasa kukaguliwa Julai 20, mwaka huu

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam.

MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, amevitaka vyama vyote vya siasa kujiandaa na zoezi la uhakiki wa vyama, linalotarajiwa kufanyika Julai 20, mwaka huu.

Akizungumza jijini Dar es Salaam,Jaji Mutungi amesema zoezi hilo ni endelevu na limekuwa likifanyika kila mwaka, likiwa na lengo la kukumbushana matakwa ya sheria ya usajili wa vyama vya siasa.

“Zoezi hili la uhakiki wa vyama, tumekuwa tukilifanya kila mwaka kama mnavyojua wengi wao wamekuwa wakikimbilia katika vyombo vya habari na kuelezea malalamiko yao,kupitia zoezi hili tunatumia fursa hiyo kukumbushana majukumu na kutambua matakwa ya sheria ya usajili wa vyama,nawaomba wote wajiandae kwani tutapita kwa ajili ya ukaguzi na kuangalia kile chama ambacho kilikuwa na dosari na bado hakijajirekebisha basi tutakichukulia hatua,” amesema Mutungi.

Aidha, ameongeza kuwa, mpaka sasa vyama vipya vilivyoomba usajili vipo 18, ambavyo baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa vyama vilivyopo, vyama hivyo vipya vitaweza kusajiliwa endapo vitakidhi vigezo kwa mujibu wa sheria.

“Mpaka sasa vipo vyama vipya 18 ambavyo vimeomba usajili lakini hatuwezi kuvisajili wakati hivi vilivyopo bado vina dosari, hivyo baada ya kuhakiki hivi vilivyopo na hivyo vingine vilivyoomba usajili basi vitasajiliwa endapo vitakuwa vimekidhi vigezo kwa mujibu wa sheria,” ameongeza Mutungi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF, Prof. Ibrahimu Lipumba, ameeleza kuwa sheria vya vyama inamtaka Msajilii wa Vyama kukagua vyama kila mwaka, ambapo miongoni mwa vitu vinavyokaguliwa ni pamoja na kuwepo kwa usajili wa vyama kupitia Rita.

Bodi za Udhamini kuwa hai, kukaguliwa kwa mahesabu na CAG pamoja na kuwepo kwa kumbukumbu ya kudumu ya wanachama.