July 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Kilimo, Josephat Hasunga

Vyama 3,348 vyafutwa kwa kukiuka masharti

Zipo SACCOS 2,513, AMCOS 229, zoezi linaendelea,
vyama kuchukuliwa hatua kwa kukiuka masharti

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imetangaza kufuta vyama vya Ushirika 3,348 ambavyo vingi ni hewa, huku ikisisitiza kwamba utaratibu huo utakuwa ni endelevu kwa vitakavyoshindwa kutekeleza majukumu ya kuanzishwa kwake.

Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Kilimo, Josephat Hasunga wakati akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma. Pia amevitaka vyama vilivyobakia kuimarisha mwenendo wao.

Vyama ambavyo vimefutwa ni Saccos 2,513, AMCOS 229, Mifugo 77, vyama vya walaji 27, vyama vya huduma 70, vyama vya ufugaji nyuki 15, vyamavya wenye nyumba 9, vyama vya madini 22, vyama vya wenye viwanda 79, vyama vya vvuvi 32, vyama vya umwagiliaji 31 na vinginevyo 244.

Kabla ya kufutwa kwa vyama hivyo, idadi ya vyama vya ushirika ilikuwa 11,626 hivyo baada ya kufutwa kwa vyama 3,348 vinabaki 8,611. Waziri Hasunga aliwataka wanachama na wakulima wanaotumia vyama vya ushirika nchini kufungua akaunti Benki ili mkulima kujihakikishia malipo yake.

Alisema kama wakulima wakifanya hivyo itakuwa ni mojawapo ya suluhu kwa udanganyifu unaofanywa na baadhi ya viongozi wa vyama vya ushirika wasio waaminifu wakati wa malipo.

Akizungumzia mfumo wa ununuzi wa mazao nchi nzima, Waziri Hasunga alisema njia pekee ya kumkomboa mwananchi ni kupitia ushirika hivyo kuwataka wananchi wajiunge na vyama hivyo ili wanufaike na ushirika.

“Wananchi wakiuza kwa pamoja ni rahisi kupata bei nzuri, hata hivyo kumetokea malalamiko mengi katika baadhi ya mikoa kuwa wananchi wananyanyasika sana na mfumo wa vyama vya ushirika na stakabadhi
ghalani,”alisema na kuongeza;

Sasa ili mfumo wa stakabadhi ghalani uweze kufanyika sawasawa naagiza kuwepo kwa chama cha msingi kilichosajiliwa katika kijiji husika, kuwepo kwa ghala lililosajiliwa na Bodi ya Maghala, kuwepo kwa mfumo wa kufanya minada kwa njia ya ushirika na kuwepo kwa wanunuzi wa kununua kwa minada.”

Kutokana na changamoto hizo, Waziri Hasunga ameagiza kuhakikisha kuwa katika kila kijiji kunakua na soko la awali ambalo wananchi watauza mazao yao lakini pia kuwe na soko la upili ambalo wananchi, vyama vya ushirika na wafanyabiashara wa ndani wataruhusiwa kuuza mazao yao kwa wafanyabiashara wa nje.

Kwa upande wake mwenyekiti wa vyama vya Ushirika nchini ,Titus Kamani aliishukuru Serikali kwa namna ambavyo imekua ikizingatia maslahi mapana ya wananchi na kwa kusimamia vema uendeshaji wa vyama hivyo.