GOMA, Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeamuru kuwahamisha watu kutoka mji wa Mashariki wa Goma baada ya volcano kulipuka katika mlima Nyiragongo uliopo karibu na mji huo wa mpakani.
Waziri wa Habari Patrick Muyaya ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba operesheni ya kuwaokoa watu kutoka eneo hilo imeanza.
Lakini hata kabla ya tangazo hilo, maelfu ya wakazi wa mji huo walikuwa wameanza kuondoka huku wakibeba vitu vichache walivyoweza kunusuru.
Gavana wa Kijeshi wa Jimbo la Kivu Kaskazini ambako Goma ni mji mkuu, Jenerali Constant Ndima amethibitisha kuwa volcano hiyo ya Nyiragongo ilianza kulipuka saa moja jioni Jumamosi ikirusha lava yake.
Mara ya mwisho volcano hiyo ililipuka Januari mwaka 2002 na zaidi ya watu 100 waliuawa. Mlipuko mbaya zaidi wa volcano hiyo ulitokea mwaka 1997 ambapo zaidi ya watu 600 walikufa.
Awali Shirika la Habari la Taifa nchini Rwanda liliripoti kuwa, karibu watu 3,000 kutoka mji wa Goma tayari wamevuka mpaka na kuingia kwenye wilaya ya Rubavu nchini Rwanda.
Shirika hilo lilinukuu mamlaka za uhamiaji kwenye mpaka kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wilaya ya Rubavu waliowasili wamehifadhiwa kwenye majengo ya shule na maeneo ya ibada ambayo yalianza kutayarishwa tangu taarifa za kutokea mlipuko wa Volcano zilipofahamika.
Balozi wa Rwanda nchini Congo, Vincent Karega aliandika kwenye ukurasa wa Twitter kuwa, “mipaka iko wazi na majirani hao wanakaribishwa kwa amani”.
More Stories
Wizara ya Nishati yawasilisha utekelezaji wa bajeti 2024/2025 kwa Kamati ya kudumu ya bunge Nishati na Madini
Watanzania milioni 13.5 kusambaziwa umeme ifikapo 2030 kutoka milioni 5.2 ya sasa
Mhandisi Kundo agoma kuweka jiwe la msingi mradi wa maji