Na Eliasa Ally, Iringa
SHIRIKA la One Acre Fund Tanzania limesema kuwa viwavi jeshi kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo vimeathiri kwa wingi mazao hususani mahindi na mazao mengine ya nafaka, hivyo kuwapa changamoto kubwa wakulima.
Afisa Habari wa One Acre Fund Tanzania, Dorcas Tinga amesema hayo jana mjini hapa wakati akizungumza na Majira.
Alisema kuwa, katika Chuo Kikuu cha Sokoine mwaka 2018 ripoti inaonesha kuwa, takribani hekta 34,000 zilishambuliwa na viwavi jeshi ambapo waliathiri kwa wingi mimea ya mahindi na mazao mengine ya nafaka suala ambalo linaweza kusababisha upungufu wa chakula kwa baadhi ya kaya nchini Tanzania.
Tinga amesema kuwa, Shukrani Kilundo ni mmoja ya wakulima wadogo kutoka Kijiji cha Tagamenda wilayani Iringa ambaye alikabiliana na wadudu hao kwa muda mrefu, hivyo kuathiri ustawi wa mazao yake.
“Shukrani anasema alijaribu kuweka majivu kipindi cha asubuhi, lakini yalioshwa na mvua ulipofika mchana, ila tunaishukuru Serikali ya Tanzania inafanya kazi kwa bidii kuwasaidia wakulima kupambana na wadudu hao nchini kote,”alisema.
Amesema, maafisa ugani wamesambazwa nchi nzima kutoa elimu kwa wakulima kupitia vikao na wakulima, kusambaza vipeperushi na kupitia vipindi vya redio.
Hata hivyo, Kitengo cha Kilimo mkoani Iringa mara kwa mara huomba muda katika redio za Furaha na Nuru FM ambapo hufundisha wakulima matumizi sahihi ya dawa za wadudu na jinsi ya kuchanganya kwa kiwango sahihi kutegemeana na ukubwa wa shamba.
ìKupitia kutembelea mashamba tunafanya uchunguzi wa awali na utabiri unaotuwezesha kugundua na kuweka mikakati ya namna ya kupambana dhidi ya mashambulizi ya wadudu, Daudi Chilagane, Afisa afya ya mimea kutoka idara ya kilimo wilayani Iringa amesema.
Pia tunatoa wito kwa wadau wa kilimo kushiriki kwenye huu mpango kwa kutoa mafunzo na vifaa vya kukabiliana na wadudu kwa wakulima,”ameongeza.
Katika kuungana na serikali kupambana na wadudu hao, Shirika la One Acre Fund, linalotoa huduma za kilimo kwa mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Songwe na Arusha ambapo katika msimu huu wa kilimo shirika limetoa zaidi ya mabomba 7,000 ya kupulizia dawa kwa wakulima, kwa njia ya mkopo.
Pamoja na mabomba ya kupulizia dawa, shirika limekuwa likitoa mafunzo na ushauri kwa wakulima juu ya kukabiliana na wadudu.
Shirika lilitoa mafunzo kwa wakulima ya jinsi ya kuwatambua viwavi jeshi mashambani na kuuza dawa za wadudu kwa wakulima kwa mkopo.
Henry Mwanilwa ni mkulima mdogo kutoka wilaya ya Iringa anasema kuwa, katika mwaka huu amechukua bomba la kupulizia dawa kwa mkopo kutoka One Acre Fund, na kupata mafunzo juu ya kukabiliana na wadudu shambani.
Bomba la kupulizia dawa limenisaidia kuokoa muda. Sasa hivi naweza kuchukua siku moja kupulizia shamba langu zima wakati awali lilikuwa likinichukua siku mbili hadi tatu.
“Ni muhimu wakulima kupata msaada wa kutosha kutoka kwa wadau wote wa kilimo,”amesema.
Tinga amesema kuwa, watahakikisha kwamba wakulima kote nchini wanapata mavuno bora msimu huu.
Pia aliongeza kuwa, One Acre Fund ni shirika linalotoa huduma za kilimo na pembejeo na kuongeza kuwa shirika hilo lilianzishwa nchini mwaka 2013, hadi sasa linawahudumia wakulima zaidi ya 55,000.
Tinga amesema kuwa, nchini shirika linafanya kazi katika mikoa mitano ya Iringa, Njombe, Songwe, Mbeya na Arusha.
“Tunawapatia wakulima wadogo wadogo ufadhili na mafunzo wanayoyahitaji ili kujiwekea njia za kudumu za kufanikiwa. Kupitia kifurushi kamili cha huduma kwa mkopo, shirika linapeleka pembejeo zenye ubora kwa wakulima mahali wanapoishi wakulima, kuwafundisha wakulima njia ambazo zitawapelekea kuvuna kwa tija,”amesema.
Amesema kuwa, pia huwafundisha namna ya kuongeza kipato kupitia mazao yao. Shirika kwa sasa linahudumia wakulima milioni moja nchini Kenya, Rwanda, Burundi, Tanzania, Uganda, Zambia na Malawi.
More Stories
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya