November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vivutio vya michezo chanzo cha watoto kupenda shule

Na Esther Macha, Timesmajira, Online, Masasi

Uwepo wa vivutio vya michezo ya bembea na vitu vingine katika shule ya msingi Mkuti B ,iliyopo katika Mji wa Masasi mkoani Mtwara umefanya kuwa na mwitikio mkubwa kwa wanafunzi wa madarasa ya awali kujiunga na kuhamia katika shule hiyo.

Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mji Masasi , Erica Yegella akiwa na baadhi ya wakuu wa idara na Mkuu wa shule ya msingi Kambarage

Mkuu wa shule ya msingi Mkuti B ,Nurdin Musa amesema hayo leo wakati uongozi wa Halmashauri Mji huo ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Mji wa Masasi, Erica Yegella alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa shule za msingi na awali kupitia mradi wa Boost kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Musa amesema kuwa mradi huo kwa shule ya msingi Mkuti B ,unajumuisha vyumba viwili vya madarasa ,matundu sita ya vyoo na kwamba mpaka sasa wamekamilisha ujenzi huo kwa asilimia 99

“Tunashukuru huu mradi kama neema kwetu maana mfano halisi toka tumefungua shule tarehe 3/7 /2023 mpaka sasa kuna watoto 24 wa madarasa ya awali wamehamia sababu ya kuvutiwa na bembea ,mtelezo na vivutio vingine kwani imekuwa ikiwapa motisha watoto ya kuja shule”amesema Mkuu huyo wa Shule.

Hata hivyo Mkuu huyo wa shule Mkuti B amempongeza Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyoitendea haki sekta ya elimu na Tanzania kwa ujumla.

Akizungumzia hali ilivyokuwa nyuma kabla vivutio hivyo vya michezo amesema kuwa watoto walikuwa hawafiki shule sababu hakukuwa na vitu vya kuwavutia katika shule.

“Sisi tulipokea Mil.66.3 mwaka huu mradi huu unajumuisha vyumba viwili vya madarasa na matundu sita ya vyoo na tayari vitu vingi vimekamilika,”amesema.

Erica Yegella ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mji wa Masasi amesema kuwa wana furaha miradi hiyo ya Boost imetekelezwa vizuri shule hizo zitakuwa na uzio kwa ajili ya watoto wa awali kutakuwa na kila kitu sehemu za kusomea nzuri na kujifunzia na tumetekeleza yote yaliyokuwa yanatakiwa katika mradi huu.

“Tunamshukuru sana Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia zaidi ya shilingi Mil.66 kwa kweli sisi kama watendaji tunamuunga mkono katika utendaji wake ametusaidia upande wa afya,elimu,maji, maendeleo ya jamii pamoja na lishe hivyo lishe bora ndo msingi wa maendeleo bila afya bora elimu haitakuwepo ,mmeshawai kuona bembea kwenye shule zetu za serikali lakini mama Samia Suluhu Hassan ameonesha,”amesema.

Nhandi Washington ni Mkuu wa shule ya msingi Kambarage amemshukuru Rais Dkt . Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia mil 77 .1 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vitatu na matundu matatu ya vyoo ujenzi umekamilika .

Shule ya awali Mkuti B ilijengwa kwa mradi wa Boost

Amesema kuwa kujengwa madarasa hayo kutaongeza chachu ya kuongeza elimu Masasi kwa sababu wanafunzi hawatarundikana tena darasani na kutoa usikivu katika ujifunzaji na kuwa awali wanafunzi 140 darasa moja kutokana na madarasa ya awali kuwa na wanafunzi wengi .