November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vituo vya Afya vyatakiwa kupanuliwa, wanawake 600 kujifungua kwa mwezi ilemela

Na Daud Magesa,Timesmajira Online, Mwanza

IDADI kubwa ya wanawake wanaojifungua imeishtua Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),Mkoa wa Mwanza,na kuagiza Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ifikirie kupanua vituo vya afya ili kuipunguzia Hospitali ya Wilaya hiyo mzigo wa kuhudumia akina mama hao.

Hayo yameelezwa na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mwanza,leo baada ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM wilayani Ilemela huku Israel Mtambalike akisema idadi ya wanawake 600 wanaojiofungua kila mwezi katika Kituo cha Afya Buzuruga ni kubwa,hivyo kwa miaka kumi kutakuwa na ongezeko kubwa la watu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza,Michael Masanja ‘Smart’ ameagiza kuwa, msongamano uliopo wa wanawake wanaohitaji huduma za kujifungua kituo cha afya Buzuruga,kipanuliwe na Zahanati ya Nyambiti ikamilishwe itoe huduma.

“Tumpongeze Rais Dk.Samia kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa maslahi ya wananchi.Hapa Ilemela angalieni Ikama ya watumishi wa sekta ya afya kama inakidhi mahitaji utoaji huduma,”amesema.

Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Mwanza Adela Mayengela,amewapongeza akina mama wa Ilemela kwa kutekeleza neno la Mungu ‘Zaeni mkaongeze mkaijaze dunia’, hivyo watoto waliozaliwa jana,Rais Samia ameona aendelee kuleta fedha na kuwataka wataalam wakazisimamie zikaipaishe CCM na kuepuka maswali wakati wa uchaguzi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Hassan Masalla amesema wamepokea maelekezo ya jumla na wameshachukua tayari hatua ya kuwekeza katika utoaji wa huduma za afya eneo walipo watu wengi,wamejenga Zahanati Nyambiti itakayotoa huduma za kujifungua.

“Umuhimu wa uwekezaji tunaofanya kukabiliana na kupunguza msongamano kituo cha Buzuruga,tumejenga zahanati kwa milioni 50 eneo la Nyambiti linaloongoza kwa wanawake wengi wanaojifungua ambapo Hospitali ya Wilaya inahudumia watu 5,000,”amesema.

Mjumbe wa NEC Mkoa,Jamal Babu amesema wenye dhamana hawajaitendea haki serikali kwa kazi iliyofanyika kwa sababu wananchi wanahitaji wafahamu yaliyofanywa na serikali yao.

“Niwaombe wakuu wa idara mpo kwa ajili ya wananchi,mnapotoa huduma mtangulizeni Mungu,kwani mnapofanya vizuri mnaisaidia CCM mkiharibu kinalaumiwa chama, pia matumizi bora ya ardhi tulinde mazingira sababu Jiji limezungukwa na miamba ya mawe,eneo linavurugwa kwa kibali cha sh.50,000 hebu watumishi tutoke ofisini kuepuka migogoro na jamii,”amesema.

Aidha Mchumi wa Manispaa ya Ilemela,Herbert Bilia amesema kila sentiinayoletwa haina makato inatumika kwa weledi,wamejipanga kuifanya manispaa iwe na uchumi imara kupitia ushuru wa huduma na mapato ya ushushaji wa mazao ya samaki na samaki Soko la Kirumba (Mwaloni).

“Mkurugenzi wa TAFICO alikuwa hapa karibuni,wana mpango wa kujenga kiwanda cha kusindika vyakula vya samaki, tunataka kuibadilisha Ilemela iwe ya viwanda tupate mapato kupitia ushuru wa huduma,”amesema.