December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Vituo 24 kuchukua sampuli za Corona

Ni katika Jiji la Dar, majina yawekwa hadharani, walengwa ni wenye dalili za Corona

Na Mwandishi Wetu

WIZARA ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetaja vituo 24 vilivyoteuliwa kwa ajili ya kuchukua sampuli ya vipimo vya vya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (COVID-19) mkoani Dar es Salaam.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, jana ilieleza kwamba hatua hizo ni mwendelezo wa hatua za wizara kuimarisha hatua za awali za mchakato wa uchunguzi wa kimaabara wa ugonjwa huo, hasa katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na visa kadhaa vya watu waliopatikana na ugonjwa wa Corona.

“Lengo ni kuhakikisha kuwa ugonjwa huu wa Corona unadhibitiwa na kutokomezwa kabisa,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba wahisiwa wote wa ugonjwa huo wamekuwa wakipimwa katika Maabara Kuu ya Taifa na majibu yao kupatikana kwa wakati kama Muongozo unavyoelekeza.

“Changamoto mojawapo ambayo imekuwa ikijitokeza ni kwa baadhi ya watu wenye dalili za ugonjwa huu kupita katika vituo kadhaa vya kutolea huduma za afya na hivyo kuchangamana na watu kadhaa kabla ya kugundulika kuwa na ugonjwa,” ilieleza taarifa hiyo ya RC Makonda na kuongeza;

“Hali hii inaweza kuchangia kuongezeka kwa visa vya ugonjwa husika kwa kasi kubwa sana. Hivyo Mkoa umejipanga kupunguza ueneaji wa ugonjwa kwa kuainisha vituo maalum vya wahisiwa wanaokidhi vigezo vya tafsiri ya ugonjwa(suspects) kuchukuliwa sampuli kwa ajili ya vipimo vya maabara katika Maabara Kuu ya Taifa.

Taarifa hiyo ilisisitiza kwamba vituo hivyo havitatumika kupima samapuli, bali ni vituo vya kukusanyia sampuli za wahisiwa tu.

Aidha, taarifa hiyo ilifafanua kuwa vituo hivyo vipya vitawawezesha wahisiwa kupata huduma ya vipimo kwa kuchukuliwa sampuli katika maeneo yao ya karibu kabla ya kuchangamana na watu wengine na kusababisha kusambaza virusi hivyo.

“Hivyo vituo hivi vitaongeza kasi ya mapambano dhidi ya ugonjwa huu hatari wa Corona (Covid-19),” alisisiza taarifa hiyo na kuongeza;

“Vituo hivi vitatumika kuchukua sampuli kutoka kwa wahisiwa na hatimaye kupeleka Sampuli hizo Maabara Kuu ya Taifa.”

Kwa upande wa Manispaa ya Kinondoni vituo vitakavyotumika ni Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Kituo cha Afya Magomeni, Kituo cha Afya Mikoroshini, Kliniki ya Masaki, Hospitali ya TMJ na Hospitali ya Rabininsia iliyopo Wazo.

Kwa upande wa Ilala vituo hivyo ni Hospitali ya Rufaa Amana, Hospitali ya Buguruni iliyopo Mnyamani, Hospitali ya Mnazi Mmoja, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hindu Mandal, Agha Khan na Regency.

Katika Manispaa Temeke vituo vitakavyotumika ni Hospitali ya Rufaa ya Temeke, Hospitali ya Mbagala Rangi Tatu, Kituo cha Afya Yombo na Hospitali ya TOHS iliyopo Chang’ombe.

Kwa upande wa Manispaa ya Ubungo vituo hivyo ni Hospitali ya
Sinza, Kituo cha Afya Kimara, Hospitali ya Mloganzila na Hospitali
BOCHI.

Katika Manispaa ya Kigamboni ni Kituo cha Afya Vijibweni, Kituo cha Afya na Hospitali ya Agha Khan (Kibada).