November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vital Kamereh

Vital Kamereh ahukumiwa miaka 20 jela, kazi ngumu kwa ufisadi wa mabilioni serikalini

Na Mwandishi Maalum, TimesMajira Online, Kinshasa

Mahakama ya Juu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imehukumu, aliyekuwa Mkuu wa Utawala, Vital Kamereh katika Serikali ya Rais Felex Tsishekedi kifungo cha miaka 20 jela na kazi ngumu kwa makosa ya kufuja mali ya umma na matumizi mabaya ya madaraka na ofisi ya umma.

Katika uchaguzi wa 2018 wawili hao walikubaliana kuunganisha nguvu na kufanikiwa kupata ushindi. Pia wachambuzi wa masuala ya kisiasa na taarifa za siri zilifichuwa kuwa,katika uchaguzi wa 2013, RaisTsishekedi angempisha Kamereh agombee urais nchini humo.

Kamerhe amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa ufisadi na wizi wa zaidi ya dola milioni 50. Kamerhe amepatikana na hatia ya kupora dola milioni 50 ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu.

Kamerhe alikanusha tuhuma dhidi yake katika kesi hiyo ambayo imetajwa kuwa ni ishara ya azma ya serikali ya nchi hiyo ya kupambana na ufisadi.

Kamerhe, mwenye umri wa miaka 61 ni mwanasiasa mkongwe katika siasa za taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya  Congo na alitoa mchango mkubwa katika kumsaidia Rais Felix Tshisekedi kuchukua madaraka.

Hukumu hiyo inamfanya Kamerhe kuwa mwansiasa wa ngazi za juu zaidi kukabiliwa na mashtaka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, nchi ambayo inatajwa kuwa na kiwango kikubwa cha ufisadi.

Wakati jaji alipokuwa akitangaza hukumu hiyo, Vital Kamerhe alitulia kimya na kuonekana akitabasamu mara kwa mara. Kesi ya Kamerhe imekumbwa na utata baada ya jaji aliyekuwa akiongoza jopo la majaji  kuuawa kwa kupigwa kichwani.

Wiki iliyopita, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilitangaza kuanzisha uchunguzi baada ya jaji Raphael Yanyi Ovungu kuuawa kwa kupigwa kichwani. Yanyi ambaye alifariki dunia Mei 26 usiku, alikuwa anasimamia kesi ya Kamerhe na washtakiwa wenzake nchini humo.