November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vita ya mimba kwa wanafunzi izingatia mambo haya

Na Reuben Kagaruki, TimesMajira,Online,Dar

SERIKALI ilitunga Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 ili kuhakikisha wanafunzi wote hasa wa kike wanakamilisha mzunguko wa elimu katika ngazi husika bila kupata ujauzito.

Kwa mujibu wa sera hiyo, Serikali itaondoa vikwazo vinavyozuia fursa ya wanafunzi kuendelea na masomo na hatimaye kukamilisha mzunguko wa elimu katika ngazi.

Akizungumza kwenye mafunzo ya waandishi wa habari yaliyofanyika mkoani Mtwara, mwanaharakati, Kudra Abdallah, alisema Sera ya ELimu inaeleza wazi kwamba Serikali itaendelea kuongeza fursa anuwai za elimu na mafunzo kwa usawa kwa makundi yote ya kijamii katika ngazi zote ikiwemo watoto wenye mahitaji maalumu.

Hata hivyo, alisema kiwango cha mdondoko wa wanafunzi wa kike kinaathiri ndoto zao. Anasema kwa sasa wasichana wengi zaidi wanakatisha masomo yao hususan kuanzia darasa la tano, ambapo wengi wanaacha shule kwa kupata ujauzito.

Akichangia kwenye semina hiyo Ofisa Ustawi wa Jamii, Edgar Swai, anasema sababu zinazochangia baadhi ya watoto wa kike kukatisha masomo ni pamoja na wazazi kutokuwa na mwamko wa elimu, ambapo baadhi yao wanawaficha wanaowapa ujauzito watoto wao.

“Ni vyema wadau wa elimu wakaangalia upya suala la wanafunzi wanopata ujauzito wakiwa shule kwa ajili ya kuwalinda waweze kutimiza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu bila vikwazo,” anasema.

Pamoja na wanafunzi kurubuniwa na kupata ujauzito, kikwazo kingine kinachochangia watoto wa kike kushindwa kufikia ndoto zao vi vitendo vya ubakaji.

“Idadi kubwa ya watoto kike wanaopata ujauzito hawaupati kwa ridhaa yao, wengine wanabakwa na ndugu wa karibu.

Tuna ushahidi baadhi ya vijana huwavizia wanafunzi wa kike wanapotoka shule na kuwabaka mwishowe huwapa ujauzito na kusababisha kukatisha masomo yao,” anasema Swai.

Mwanasheria kutoka Shirika la Ndoto ya Kesho, Suzana Tallas, alisema wanaume walaghai hupata mwanya mzuri wa kuwarubuni wanafunzi wanaopanga mitaani kutokana na shule nyingi kutokuwa na hosteli.

“Kwa sababu watoto hao wanakuwa pia wana shida ya fedha za kujikimu, zikiwemo za chakula na malipo ya vyumba, hulazimika kujiingiza kwenye vitendo vinavyosababisha mimba kwa watoto wetu,” alisema na kuongeza;

“Baadhi ya wanafunzi wa kike hupata mimba si kwa kujitakia. Bali kutokana na mazingira na maisha ya shule kuwaweka katika hali ya hatari kubwa wakiwa bado ni watoto.

Wanafunzi wanaokatisha masomo kwa kupata ujauzito ni wataalamu watarajiwa, hali hii ikiendelea tutakosa wataalamu, ni vyema wadau wa elimu waliangalie upya ili kunusuru kizazi cha kesho.”

Anashauri yaanzishwe makazi ya salama kwa wanafunzi wa kike, ikiwemo ujenzi wa mabweni ambayo yapunguza kwa kiwango kikubwa mimba kwa wanafunzi wa kike.

“Jamii ikihamasika kwa kutambua na kuthamini elimu ya sekondari hasa kwa mtoto wa kike itaweza kumkinga kupata mimba kwa kuwa ni hatari kwa afya,” anasema Swai.

Mshiriki wa mafunzo hayo, Asha Kashakala alisema kuna kila sababu, wenye viti wa vijiji hasa kule ambako shule za kata zimejengwa, madiwani, wabunge, viongozi wa halmashauri na wote waliopo sehemu husika kwa pamoja wakawa wanaitisha vikao vya dharura mara kwa mara ili kuona ni nini wanaweza kufanya ili mazingira ya shule zinazowazunguka yaboreshwe na yawe salama kwa wanafunzi wa kike.

Wanafunzi wakitoka shuleni wakipita katika mazingira yasiyokuwa rafiki

“Viongozi hawa wakizinduka na kulipa kipaumbele suala la elimu maeneo yao yatafanya maajabu ya kupigiwa mfano kwenye shule za kata,” anasema na kuongeza;

“Viongozi wakiamua kufanya mambo ya kuleta mabadiliko kwa kuhakikisha kunakuwepo walimu wa kutosha na wanaofanyakazi kwa furaha bila malalamiko ya ukosefu wa nyumba, mishahara kutoongezwa, kutopandishwa madaraja kwa wakati nao watabadilika na badala yake watahakikisha watoto kike wanahitimu masomo yao na kufaulu bila kupata ujauzito,” anasema.

Hata hivyo, anasema kwa mazingira ya sasa hofu ya wasichana watakaokuwa viongozi inazidi kuongezeka kutokana na wanafunzi wengi wa kike kukatiza masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo za kupata mimba.

Akithibitisha ukubwa wa tatizo la mimba kwa wanafunzi, Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Sengerema Mrakibu wa Polisi, Kulwa Misogalya, anasema kwa mwaka jana (2020) matukio ya kesi za ujauzito yaliyoripotiwa kwenye Dawati la Jinsia wilayani humo yalikuwa 168.

Kati ya hayo ya ubakaji yalikuwa 69. Miongoni mwa matukio hayo ni kesi ya kubakwa ambapo mzee mmoja aliyekuwa akibaka watoto wake, ambapo alihukumiwa kwenda jela miaka 50.

Misogalya alitoa takwimu hizo wakati wa Maadhimishi ya Siku ya Mtoto wa Kike yaliyofanyika Oktoba 11, mwaka huu wilayani humo. Aidha, alisema mwaka huu (2021) makosa ya kuwapa ujauzito wanafunzi yalikuwa 68 na kutorosha wanafunzi 25.

Takwimu za miaka miwili za Wilaya ya Sengerema zinaonesha wazi kwamba tatizo la wanafunzi kukatiza masomo kwa sababu za ujauzito ni mkubwa, hivyo hatua zaidi zinahitajika kulinda watoto wa kike waweze kufikia ndoto zao.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Sengerema, Tumsifu Barnabas, anasema jamii ni lazima itambue kwamba, siyo kila mtoto wa kike anayepata mimba ni malaya, kwani wapo watoto wanaobakwa na kujikuta wakipata ujauzito.

“Baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutambua kwamba wapo watoto wanabakwa, wanaofanyiwa vitendo vya ukatili na watu ambao wamewaamini sana tena wengine ndani ya familia, ikaona inafaa sasa kutengeneza sheria kali, ambazo zitamlinda mtoto hasa wa kike dhidi ya vitendo hivyo vinavyofanywa na watu wenye uchu,”alisema Tumsifu.

Mwanasheria mwingine, Mwanahamis Nassoro, anasema mwaka 1998 Bunge lilitunga Sheria inayoitwa Sheria ya Makosa ya Kujamiiana iliyoanza kutumika Julai 1, 1998 ili kulinda watoto wa kike.

“Sheria hii inamlinda mtoto katika maeneo ya kudhalilishwa na hata
mila ya kukeketa watoto wa kike imefanywa kuwa kosa la jinai,” anasema na kuongeza kwamba Sheria kama hiyo pia imepitishwa Zanzibar.

Madhumuni ya sheria hii ya makosa ya kujamiiana ni kuingiza katika sheria za jinai za Tanzania masharti maalum kisheria kuhusiana na makosa hayo ya
kujamiiana au yanayowahusu watoto.

Alisema nia ni kuimarisha azma ya taifa ya kuhifadhi stahili za watoto
na wanawake kuhusiana na haki binafsi za uzima, heshima na uhuru.

“Mtoto analindwa na Sheria hii katika vifungu vilivyorekebisha Sheria ya Kanuni za Adhabu na katika vifungu vipya vilivyowekwa, mambo yafuatayo ni
makosa kwa yeyote atakayetenda dhidi ya mtoto;

Makosa hayo ni udhalilishaji watoto kijinsia, utumiaji potofu wa watoto
kijinsiakukeketa watoto wa kike, kuingiza watoto katika
masuala ya umalaya,” anasema.

Hata hivyo, anashauri ili sheria hiyo iweza kuwa mlinzi kamili wa mtoto wa kike ni lazima ndani ya jamii zikaanzishwa Kamati za Kuzuia Ukatili wa Kijinsia.

Anasema kamati hiyo zikianzishwa ndani ya jamii itakuwa rahisi kuzipatia elimu kwa ajili ya kumlinda mtoto wa kike. “Lakini ni vyema Serikali ikawarejesha shuleni wanafunzi waopata ujauzito ili kuongeza idadi ya wataalamu wa Taifa la kesho,” anasema.