December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi watakiwa kuelimisha wananchi adhima ya serikali kupumzisha Z.Tanganyika

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Nkasi

KAIMU Mkuu wa Wilaya ya Nkasi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Razaro Komba amewataka Madiwani,Viongozi wa vijiji na watumishi wote wa serikali kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi wa maeneo yao juu ya adhima ya serikali ya kutaka kulipumzisha Ziwa Tanganyika kwa muda wa miezi mitatu.

Komba amesema amesema kuwa lengo la serikali ni kutaka kulipumzisha ziwa hilo ili kuwapa muda samaki kuweza kuzaliana na kuongeza kipato cha wavuvi kwa kuweza kuvua samaki wengi na wakubwa wanaostahili.

Hayo ameyazungumza kwenye kikao kilichowakutanisha kati ya Madiwani na viongozi wa vijiji vilivyo mwambao mwa Ziwa Tanganyika pamoja na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Amedai kuwa kinachotakiwa ni wananchi kuuelewa mpango huo vizuri na kujua faida zitakazopatikana baada ya ziwa hilo kupumzishwa huku kila mmoja akitakiwa kuwa mlinzi kwa mwenzie kwa kuhakikisha katika kipindi hicho cha miezi mitatu hakuna mtu atakayefanya shughuli ya uvuvi ziwani humo.

Sambamba na hilo ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuongeza vikundi vya uvuvi (BMU) kwani uzoefu unaonesha kuwa katika maeneo ambayo BMU zimeanzishwa kuna ufanisi mkubwa na wamekuwa walinzi kwa wenzao wanaokwenda kinyume na huku akitamani zoezi hilo lingefanyika kabla ya Mei 15,2024 ziwa hilo litakapopumzishwa.

Mteknolojia wa Samaki kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Masui Munda amedai kuwa mpango wa kupumzisha ziwa hilo umetokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa na kuona kuwa ziwani hapo samaki wameendelea kupungua kwa kasi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uvuvi haramu na kuharibu mazalia ya viumbe maji hivyo kitendo hicho ndio suluhisho pekee la kuwapa nafasi ya kuzaliana.

Masui ameeleza kuwa kama Wizara walienda mbali zaidi kwa kushirikiana na nchi tatu zinazolitumia Ziwa Tanganyika ambazo ni Zambia,DR –Congo na Burundi na kuweka azimio la pamoja ambapo nchi zote itakapofika Mei 15,mwaka huu zitalifunga ziwa hilo na kufanya doria ya pamoja ya kukabiliana na wavuvi ambao watashindwa kutekeleza agizo hilo la serikali.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uvuvi na Kaimu Mkurugenzi wa tafiti na mafuzo ya uvuvi
Imelda Adamu pamoja na Ofisa Uvuvi Mkuu Owen Kibona wamesema kuwa kama zoezi hilo litakwenda vizuri wananchi wenyewe watayaona matokeo baada ya kupumzishwa kwa kipindi hicho cha miezi 3 kwa maana mavuno ya samaki yataongezeka na kuongeza kipato chao katika ngazi ya familia na pato la taifa

Kwa upande wao Madiwani wameitaka serikali kuhakikisha katika kipindi hicho wanawadhibiti Watendaji wa Idara ya Uvuvi ili wasitumie muda huo kujinufaisha kwa kuwaruhusu watu wachache wafanye uvuvi na kuomba kuwepo na kikosi maalumu cha doria kuweza kuwadhibiti wavuvi watakaokaidi agizo hilo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Nkasi Pankrasi Maliyatabu amesema kama viongozi wa vijiji na Madiwani watatekeleza wajibu wao sawasawa wa kuielimisha jamii juu ya mpango huo wa serikali wa kulipumzisha ziwa anaamini jambo hilo litakelezeka kwa maana Wananchi wengi wanao uelewa wa mambo pia na wao wanaona hali ya uvuvi ilivyo dorora na samaki wanaovuliwa ni wadogo hivyo ni lazima watakubaliana na mpango huo wa serikali.