Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
UPATIKANAJI wa maji katika Mji wa Korogwe umekuwa ukiongezeka kwa kasi kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoka asilimia 43 mwaka 2020 hadi zaidi ya asilimia 85 kwa sasa, na kuondoa adha kubwa kwa wananchi kukosa huduma ya maji safi na salama.
Huku Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) ameweza kujenga barabara nyingi kwa kiwango cha lami kwenye mji huo na kufanya upendeze hasa nyakati za usiku sababu ya taa pembezoni mwa barabara na kuongeza shughuli za kiuchumi hasa biashara za chakula usiku.
Hayo yamesemwa Juni 7, 2024 na Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga Dkt. Alfred Kimea mbele ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa Dkt. Emmanuel Nchimbi,kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa soko la Manundu mjini Korogwe.
Dkt. Kimea amesema kazi kubwa ya maboresho ya maji kwenye Mji wa Korogwe imefanywa vizuri na watu waliopewa dhamana kwenye sekta ambapi amewataja kuwa ni Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe Mhandisi William Tupa, na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM) Mhandisi Yohana Mgaza.
“Kwenye Sekta ya Maji, wakati tunaingia madarakani mwaka 2020, Korogwe ilikuwa ni moja ya miji yenye changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji, watu wa Korogwe ni mashahidi. Lakini leo tunapeleka salamu zetu kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyowapendelea wananchi wa Jimbo la Korogwe Mjini hasa kwenye Sekta ya Maji.
“Mwaka 2020 tulikuwa tunapata maji kwa asilimia 43, lakini kwa sasa tunapata maji zaidi ya asilimia 85, na kuweza kuwatua wamama ndoo kichwani,
na nitoe pongezi kwa watu waliopewa dhamana hiyo ya maji na kuweza kutekeleza miradi, Mhandisi Upendo, Mhandisi Tupa, na Mhandisi Mgaza.
“Hawa wamehakikisha Korogwe tunapata maji safi na salama Hivi sasa wanatujengea chujio kubwa ambayo itachuja maji yote yatakayoingia kwenye Mji wa Korogwe, ile uhaba wa maji, na maji machafu kuingia kwenye mabomba haitakuwepo” amesema Dkt. Kimea.
Aidha Dkt. Kimea amesema Mji wa Korogwe sasa hivi ni kama Jiji la Toronto nchini Canada, kwani kuna barabara za lami kila kona na taa zinawaka mji mzima.
“Kwa upande wa barabara, sasa hivi mji wetu ni kama Toronto (Canada), unapendeza hasa nyakati za usiku, kwani unawaka taa kila kona. Hii pia ni kazi nzuri iliyofanywa na TARURA kuona barabara zenu zinakuwa za lami na kuwekwa taa. Bado Rais Dkt. Samia amefanya kazi kubwa kwenye sekta ya afya, elimu na kufanya tufurahie na kujivunia uongozi wake” amesema Dkt. Kimea.
Naye Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CPA Amos Makalla amesema wakati huo akiwa Naibu Waziri wa Maji anajua shida ya maji katika Mji wa Korogwe sababu alikuwa anakwenda Korogwe kikazi, lakini pia kama Ujombani, hivyo anapongeza jitihada za Serikali kuona tatitzo la maji limepata ufumbuzi.
“Nataka tu kueleza kwamba, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (2020- 2025) imetekelezwa vizuri na mimi ni shahidi.
“Korogwe naijua,mimi nilikuwa Naibu Waziri wa Maji, kila nikija hapa tulipanda milimani huko, lakini sasa kuna maendeleo makubwa na yanaonekana, na heshima na shukurani tumpelekee Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kuna mabadiliko makubwa, iwe Sekta ya Afya, iwe maji, iwe barabara, kila sekta amegusa.
“Iwe katika elimu, utaona madarasa, utaona vituo vya afya, utaona katika zahanati, kwa hiyo utaona mambo mengi sana yametekelezwa” amesema Makalla.
More Stories
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi
Mbunge Ndingo:CCM imejidhatiti kuwaletea maendeleo wananchi