October 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi, wafanyabiashara watakiwa kusaidia jamii kwa vitendo

Raphael Okello, Timesmajira Online,Musoma

Serikali, viongozi wa madhehebu ya dini na wafanyabiashara,wameshauriwa kusaidia jamii kwa vitendo na siyo kuishia kwenye maneno.

Kauli hiyo imetolewa Jana na Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo,wakati wa sherehe za Jubilei ya miaka 40 ya Upadre wa Mhashamu Askofu,Michael Msonganzila wa Jimbo Kuu la Musoma mkoani Mara,iliofanyika mjini Musoma.

Kardinali Pengo, amesema viongozi wa dini, serikali na mashirika mbalimbali wamekuwa wakitetea makundi yaliyosahaulika, kwa maneno bila vitendo.Huku akimuelezea Askofu Msongazila kuwa amekuwa mfano katika utumishi wa kanisa kwa takribani miaka 40.

“Kumekuwepo na tabia ya kukemea vitendo vya ukatili,kwa maneno bila vitendo.Unakuta mwanamke au binti ametendewa ukatili hana makazi,basi isiishie hapo mjengeeni nyumba ili aishi
salama,”ameeleza Kardinali Pengo na kuongeza:

“Tumechukua mfano mzuri kwa Askofu Msongazila, alipoona watoto wa kike hapa Mara wanafanyiwa ukatili wa kijinsia, alichukua hatua kwa kushirikiana na Mfuko wa Graca Machel, kwa kuhakikisha wasichana hao wanaondokana na vitendo vya ukatili,”.

Pia ameeleza kuwa,ndani ya jamii Kuna watu wanaopitia wakati mgumu huku wakikosa msaada,hivyo ni vyema jamii ikawasaidia kuliko kuwaacha wakiendelea kupata mateso.

Akiwasilisha zawadi ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania , Dkt. Samia Suluhu Hassan kiasi cha milioni 30,Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Degratius Ndenjebi,amesema kuwa miaka 40 si haba ukiwa kazini,”hivyo tumetakiwa kuiga na kutenda mema,”.