June 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi waanza kuwaogopa wajumbe Morogoro

Na Mwandishi Wetu,Morogoro


WAJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Morogoro wamelazimika kuhudhuria kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho Wilaya huku wakitakiwa kuzima simu huku lengo ikidaiwa kuwa ni kudhibiti ‘uvujishaji wa siri za kikao hicho.

Hatua hiyo imedaiwa kutokana na agizo lililotolewa na Katibu wa Chama hicho wa Wilaya hiyo Twalib Berege, baada ya kudaiwa kuvuja Kwa taarifa za kikao cha ndani kilichofanyika June 6 baina yake na watendaji wa chama hicho ngazi ya kata ambao walidaiwa kugawa fedha kwa wajumbe 27 walioudhuria kikao hicho iliyodaiwa kutolewa na mbunge wa sasa Morogoro Mjini.

Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao, baadhi ya wajumbe wa kikao hicho wakiwemo Madiwani, Wenyeviti na Makatibu na Wenezi wa chama hicho Kata walisema amri hiyo ilitolewa na Katibu wa kikao hicho mara baada yakuingia katika kikao hicho walipewa maelekezo yakukusanya simu ambazo ziliandikwa majina kupitia vikaratasi maalum na kupelekwa meza kuu.

” Leo (jana) tumefanya mkutano katika Ukumbi wa Kingaru, lakini kabla ya yote wajumbe wote zaidi ya 129 tuliamriwa na Katibu wa CCM Wilaya kukabidhi simu zetu ili kuepusha siri za kikao hicho kuvuja, kwa madai wapo baadhi ya wajumbe katika kikao kilichopita baadhi ya watu walitoa taarifa kwa waandishi wa habari na kutaja jina la mmoja wa waandishi hao ambaye aliazindika taarifa hizo” alisema mmoja wa wajumbe hao.

Alisema Katibu huyo pia alikiri kupigiwa simu na mwandishi huyo wa habari huku akitaja sehemu ya zamani aliyokuwa akifanya kazi mwandishi huyo kana kwamba anamfahamu vizuri hivyo lengo lake hilo ni kudhibiti taarifa hizo kumfikia.

Alisema kikao hicho kilichohudhuliwa na viongozi wote wa chama hicho wilaya akiwemo Mbunge wa Jimbo hilo, kilimalizika kwa wajumbe wote kupewa posho ya Sh 20,000 na wakiambiwa kuwa posho hiyo ni kama ‘rasha rasha’ na kwamba mvua inakuja, kauli inayodaiwa kutolewa na Mbunge huyo.

Aidha diwani huyo ameomba Chama kufuatilia mwenendo wa vikao hivyo na ikibidi hata kuchukua hatua kwa Katibu huyo pamoja na Mbunge ili kudhibiti mwenendo wa kujirudia kwa matukio ambayo kwa namna moja au nyingine yanaweza kuleta dosari ndani ya chama hicho

Awali akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa CCM Wilaya hiyo Fikiri Juma aliwaasa viongozi wote wa Chama hicho kujiepusha na tabia ya kuwabeba wagombea na badala yake wajikite katika kutenda haki kwa wagombea wote bila kujali kuwa amewahi kupita madarakani au mgombea mpya.

Alisema hadi sasa chama hicho kimepitisha majina ya wagombea watatu akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan katika nafasi ya ugombea wa Urais Tanzania, Dk Hussein Mwinyi, mgombea Urais Zanzibar pamoja na Dk Emmanuel Nchimbi kwa nafasi ya mgombea mwenza.

Zimesalia takribani siku 17 kufunguliwa cha dirisha la ya uchukuaji wa fomu kwa ajili ya mchakato wa ndani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuomba kuteuliwa kabla ya baadae majina ya waliojitokeza kuchujwa ili kuwapata wawakilishi katika nafasi za Ubunge na Udiwani.