Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
VIONGOZI wa Vijiji kwenye kata za Vugiri na Lewa katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga wamesema Mradi wa Forests, Rights and Livelihoods (FORLIVES) umeweza kuwasaidia kurudisha uoto wa asili kwenye misitu ya asili kwa wananchi wa vijiji vinne baada ya kupewa elimu huku wakiwezeshwa ili kutunza mazingira.
Wamesema mradi huo uliotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kwenye vijiji vya Mashindei, Vugiri, Bagamoyo na Old Ambangulu, umebadilisha sio uhifadhi wa mazingira tu, bali pia kuwasaidia wananchi kiuchumi kwa kuwafundisha kilimo cha mazao ya biashara na chakula, huku wakipewa elimu ya ukusanyaji mapato.

Walitoa ushuhuda wao Septemba 29, 2025 kwenye kikao cha pamoja kati ya viongozi wa vijiji, viongozi wa Mradi wa FORLIVES, mfadhili wa mradi huo Shirika la Danmission la nchini Danmark, Shirika la Uhifadhi wa Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Goodluck Mwangomango.
Julius Mntambo ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Vugiri, Kata ya Vugiri amesema Mradi wa FORLIVES umewasaidia kurudisha uoto wa asili, ambapo wameweza kutunza mazingira kwa kushirikiana na Shirika la TFCG, ambapo wanafanya mikutano ya hadhara na kukubaliana ni mambo gani wafanye ili kutunza mazingira. Ni baada ya shirika hilo kuwasaidia kutunga Sheria Ndogo za Vijiji.
Naye Rajab Gao ambaye ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mashindei amesema changamoto ni nyingi kulinda misitu, lakini uwezeshaji walioupata kutoka kwa Shirika la FORLIVES ni mkubwa sana, na hiyo iliwasaidia kuondoka kwenye mvutano wa mara kwa mara

Mwenyekiti wa Kijiji cha Bagamoyo, kilichopo Kata ya Vugiri, Daud Ponda amesema wamewahamasisha wananchi kulima kilimo cha kutunza mazingira. Kuna wataalamu wanakwenda kutoa elimu ya kulima kwa kuchimba matuta, matumizi ya mbolea ya asili ya samadi na mboji.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Bagamoyo Obed Revocatus amesema zile changamoto zilizowekupo za wananchi kuvamia misitu na kuvuna miti zimeondoka baada ya wananchi kupata uelewa, na sasa hawatumii nguvu nyingi kuweza kutunza mazingira.
Kiongozi wa kidini kutoka Kijiji cha Bagamoyo Hamdan Almas alisema wanajivunia kwa jinsi walivyofanya kazi ya kuhamasisha wananchi juu ya utunzaji wa mazingira na shughuli nyingine za kiuchumi.

Mdau wa mazingira, Rajab Mhidini aliitaka Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kujiandaa kuwezesha wananchi wa vijiji hivyo vinne kuendelea kutunza mazingira, na kusema umefika wakati wananchi waweze kujisimamia wenyewe hasa kwenye mambo ya msingi, badala ya kila siku kuwatagemea wafadhili.
Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia Mwenyekiti (mstaafu) wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Sadick Kallaghe amesema kinachotokea sasa duniani, na Tanzania, sio Mabadiliko ya Tabianchi, bali mabadiliko ya tabia za watu kuharibu mazingira yanayotuzunguka, hivyo umefika wakati kuweza kutatua changamoto kwa kuchukua hatua kazi za kisheria.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, ambaye pia alikuwa mgeni rasmi, Goodluck Mwangomango ameushukuru Mradi wa FORLIVES kwa kusema sio tu kuwa walikuwa wanafanya kazi kwa weledi, lakini pia kila siku walikuwa wanawapa mrejesho wa kila kinachofanyika kwenye mradi huo.

“Kwa kipekee niwashukuru kwa Program hii, kwani imekuwa na manufaa kwetu. Wote mnajua, Serikali ndiyo yenye jukumu la kulinda mazingira na watu wake. Kazi hizo zote ni zake kwa mujibu wa sheria na Katiba ya Jamhuri ya Tanzania, lakini tunafahamu uwezo wa Serikali unategemea makusanyo kutoka kwa wananchi. Sasa kwenye nchi hizi zetu changamoto ni nyingi hakuna eneo ambalo limekamilika, hivyo unajikuta matumizi ni makubwa kuliko unachokusanya
“Sasa kupitia mahusiano ambayo nchi yetu imeyajenga na nchi nyingine sasa tumekuwa tukipata fursa kama hizi, tunapata mashirika ambayo yanakuja kufanya kazi za kijamii kwenye nchi yetu kwenye maeneo ambayo sisi hatufiki. Serikali inafanya asilimia 70, na wao wanamalizia asilimia iliyobaki. Hivyo tunawashukuru ndugu zetu wa Danmark kupitia Danmission kwa kuweza kujenga mahusiano mazuri ya muda mrefu kwa kusaidia jamii yetu” amesema Mwangomango.
Mkurugenzi Mtendaji wa TFCG Charles Meshack amesema moja ya kazi zilizofanyika kwenye mradi huo wa FORLIVES ni kuimarisha mipango bora ya matumizi ya ardhi na misitu, kuimarisha makubaliano ya ulinzi wa misitu, kulinda zaidi ya hekta 200 za misitu kwa doria na upandaji miti na kuimarisha Kamati za Maliasili za Vijiji zenye usawa wa kijinsia na ushirikishwaji wa vijana.

“Pamoja na hayo, mradi unaunga kilimo rafiki kwa ajili ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, kuanzishwa vikundi vya wakulima na kuwajengea uwezo wana jamii zaidi ya 600 wakiwemo vijana na viongozi wa dini. Hata hivyo, changamoto bado zipo ikiwemo migongano ya ardhi, shinikizo la maisha linalotokana na kipato duni kwa jamii ambayo inapakana na misitu, na hitaji la kudumisha matokeo baada ya huu mradi” amesema Meshack.
Mkurugenzi wa Danmission kwa Ukanda wa Afrika Mashariki Signe Atim Allimadi, ambao ndiyo wafadhili wa Mradi wa FORLIVES kutoka nchini Danmark, amesema amefurahishwa kuona ushirikiano mkubwa uliokuwepo kwa kipindi chote cha mradi kati ya wananchi, viongozi wa jamii, viongozi wa dini, siasa na uongozi wa halmashauri.
Allimad amesema kazi wanazofanya viongozi hao ni ngumu na kubwa, lakini wameweza kushirikiana na wananchi kufanikisha mradi huo, na uweze kuendelea na kufika mwisho, na hilo limeleta mafanikio makubwa kwa wananchi kuweza kutunza mazingira, kufanya shughuli za kilimo na kujipatia kipato kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi mara baada ya kikao hicho, Meneja wa Mradi wa FORLIVES Bettie Luwuge amesema mradi umetekelezwa kwa miaka mitatu, na unakwenda kufikia mwisho Desemba, mwaka huu, ambapo umeweza kuimarisha na kuwawezesha jamii zinazotegemea misitu kwa kusimamia haki zao za ardhi na maliasili kupitia usimamizi endelevu wa misitu na ardhi, na kuboresha maisha ya jamii katika Kata ya Lewa, na Vugiri, kwenye vijiji vya Mashindei, Vugiri, Bagamoyo na Old Ambangulu.
Luwuge amesema vijiji hivyo vipo eneo lenye umuhimu wa Bioanuwai la Tao la Mashariki (West Usambara). Mradi ulipata ufadhili wa miaka mitatu (2023- 2025) kutoka Shirika la Danmission kutoka nchi ya Denmark. Shirika la Danmission ni la kidini na linadhamiria kuona dunia ambayo watu wanaishi pamoja kwa amani katika mazingira yao.
“Mradi una matokeo makuu matatu, Mosi; Jamii zinazoishi kandokando mwa hifadhi za misitu katika Milima ya Usambara Magharibi zimenufaika moja kwa moja na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu ifikapo mwishoni wa mwaka 2025. Pili: Jamii zinazoishi pembezoni mwa Milima ya Usambara Magharibi zimeboresha mbinu za kilimo kufikia mwaka 2025, na tatu; Uwezo wa jamii zinazoishi pembezoni mwa Milima ya Usambara Magharibi na taasisi za kidini umeimarika katika nyanja mbalimbali zinazopelekea utumiaji endelevu, utekelezaji thabiti na usimamizi bora wa maliasili kufikia mwaka 2026″amesema Luwuge.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi