Na Daud Magesa, Timesmajira Online,Mwaza
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mwanza imewapa viongozi wa Dini na Baraza la Wazee, mafunzo ya athari za rushwa katika uchaguzi.Ili iwasaidie kuelimisha jamii kupambana na vitendo vya rushwa.
Agosti 29,2024,Mkuu wa TAKUKURU mkoani Mwanza James Ruge,akifungua mafunzo hayo ,amesema,yataongeza uelewa na kuhamasisha jamii kukataa vitendo vya rushwa, kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani,vinavyohusishwa na kupatikana viongozi wasio waadilifu na wanaoharibu utawala bora na kukwamisha maendeleo.
Amesema TAKUKURU inatambua ushawishi mkubwa wa viongozi wa dini katika jamii,wanayo nafasi ya kuzuia rushwa kwa kufundisha maadili na kutoa mahubiri ya kuliunganisha taifa katika mapambano dhidi ya rushwa.Hivyo watumie nyumba za ibada kukemea vitendo vya rushwa katika chaguzi mbalimbali.
“Rushwa ni adui wa haki,ni kosa la kimaadili, kiimani na kijinai kwa mujibu wa sheria ya TAKUKURU sura ya 329 na majerejeo yake ya mwaka 2022.Pia rushwa ni dhambi,serikali inafanya juhudi kuhakikisha mapambano dhidi ya rushwa yanaendelea, hivyo mkakati wa kuwafundisha viongozi wa dini athari za rushwa unaweza kutoa mwanga wa vitendo hivyo kwa waumini wao,”amesema Ruge na kuongeza:
“Kukuza na kuhamasisha misingi ya utawala bora,ni lengo la kila mwananchi la kutokomeza rushwa nchini.Moja ya majukumu ya TAKUKURU ni kuzuia vitendo vya rushwa, kwa kushirikisha wananchi kwa njia ya elimu, mafunzo haya yataongeza ujuzi na ufanisi wa kutekeleza jukumu la kuelimisha jamii ubaya wa rushwa,kuwahamasisha wananchi kushiriki mapambano dhidi ya rushwa,kwa kuzuia, kukemea na kutoa taarifa kwa wanachokiona tunapoelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani,”.
Naye Ofisa wa TAKUKURU Dawati za Uzuiaji Rushwa,Stella Bukuru,ameonesha umuhimu wa kuelimisha jamii kuhusu maadili mema ili kupunguza rushwa,hasa wakati wa uchaguzi kwa kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu rushwa ya chakula na khanga kuwa,kunaweza kusaidia kupunguza vitendo vya rushwa katika uchaguzi kwa kuzingatia kauli mbiu ya “Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu:Tutimize Wajibu Wetu.”
“Uelewa mdogo wa jamii ni kihatarishi kinasababisha washindwe kutambua madhara ya miaka mitano yanayotokana na rushwa ya khanga au wali.Hivyo ukosefu wa maadili ni eneo ambalo viongozi wa dini mtakuwa msaada kwa TAKUKURU mkilisimamia katika madhabahu na mimbari kuwakumbusha watu maadili kuelekea uchaguzi,vile vile kuwaondolea giza walilomo la uelewa mdogo wa nini athari za rushwa kwa viongozi wanaowachagua,”amesema.
Ofisa Uchaguzi Jiji la Mwanza,Francisca Mshashi, amesema viongozi wa dini wanapaswa kuhamasisha waumini wao kuchagua viongozi waadilifu na kuhimiza wanawake kujitokeza kuwania nafasi za uongozi,ili kuonesha jitihada za kuhakikisha kuwa chaguzi zijazo zinakuwa na uwakilishi mzuri na wa haki.
Kwa upande wao Wenyeviti wenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Mwanza,Sheikh Hasani Kabeke na Askofu Dk.Charles Sekelwa wameishukuru TAKUKURU kwa kuandaa mafunzo hayo na kuaihidi ushirikiano wa karibu katika kupambana na rushwa.Kwamba ushirikiano huo ni muhimu kwa mafanikio ya mapambano dhidi ya rushwa.
“Rushwa katika Uislamu ilivyo ni dhuluma,amelaaniwa mtoaji na mpokeaji, ni mauaji jambo linalofanyika chini ya kiwango ni mauaji,sote tunakumbuka ajali ya Igandu na Msagali.Taifa hili ni dhamana kwetu rushwa isituharibu,ndicho TAKUKURU inachohangaika kukifanya,”amesema Sheikh Kabake.
“Rushwa ni mtindo wa maisha ya mtu asiye mwadilifu,rushwa ni changamoto endelevu,rushwa ni kosa la jinai na kimaadili na hakuna kiongozi wa dini anayehitaji hayo ndiyo tunayoyafundisha katika dini.Tunamfundisha tabia njema mtu aende kwa Mola wake, hivyo sisi na makundi mengine mtufanye marafiki tusiotafuta faida kama mnataka kufanikiwa,”amesema Askofu Dk.Sekelwa.
More Stories
TMDA:Toeni taarifa za ufuatiliaji usalama wa vifaa tiba ,vitendanishi
The Desk & Chair yashusha neema Gereza la Butimba
TVLA,yapongezwa kwa kuzalisha chanjo