December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viongozi wa dini zaidi ya 100 wawasili Dodoma na Treni ya umeme

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

VIONGOZI wa Dini kutoka katika madhehebu mbalimbali wamewasili jijini Dodoma kwajili ya kuliombea Taifa kwa kutumia treni ya kisasa inayotumia umeme ya majaribio kutoka Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kuwapokea viongozi hao jijini hapa leo,Aprili 21,2024,Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt.selemani Jafo akiwa na viongozi wengine mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Rosemary Senyamule pamoja na wananchi amesema kuwa viongozi hao wanatarajiwa kushiriki ibada maalum ya kuliombea Taifa katika uwanja wa Jamhuri leo Aprili 22,2024 wakiongozwa na Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango.

Waziri Dkt.Jafo amesema kuwa wakati taifa linaelekea kuadhimisha miaka 60 ya Muungano suala la viongozi wa dini kusafiri kwakutumia treni ya kisasa ya umeme ni mafanikio makubwa na serikali imeona ni vyema viongozi wa dini kuwa wa kwanza kusafiri na usafiri huo wakiwa wanaenda kuliombea Taifa.

“Ndugu zangu najua mmetoka mbali tunawakaribisha sana Dodoma lakini naomba niwambie viongozi wa dini serikali inayoongozwa na Dkt.Samia inawapenda sana na kesho tutakuwa na maombi ya kuliombea Taifa letu kwa tunu ya Muungano tulionao,”amesema Dkt.Jafo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Shirika la Reli Tanzania(TRC)Masanja Kadogosa amesema kuwa wanaposafiri na treni hiyo wanatesti madaraja kuhakikisha ubora wake upo vizuri pamoja na makaravati.

Aidha amesema kuwa Treni hiyo ya umeme iliyobeba watu mbalimbali pamoja na viongozi wa dini 160 imetumia umeme wa shilingi milioni 1.2 kutoka Dar es Salaam  hadi Dodoma kwa saa 3 na dakika 21.