Na Penina Malundo,timesmajira,online
KAMATI ya Viongozi wa Dini inayohusu Haki za Kijamii na Uadilifu wa Uumbaji (ISCEJIC) inayoundwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwa kushirikiana na Mtandao wa Watetezi wa Haki za binadamu Tanzania (THRDC) imeendesha mafunzo kwa viongozi wa dini mkoani Kilimanjaro.
Lengo la mafunzo hayo ni kukuza uwezo kwa viongozi hao kuweza kusaidia kushiriki na kutatua changamoto za kijamii hasa katika ulinzi na utetezi wa haki za binadamu pamoja na kushiriki katika mabadiliko ya kisera ili kusaidia kukuza utawala bora nchini.
Semina hiyo imekutanisha viongozi wa dini takribani 40 kutoka katika Kamati za Dini Mbalimbali za mikoa ya Manyara, Dodoma pamoja na Kilimanjaro.
Akizungumza jana jijini Arusha wakati wa warsha hiyo,Askofu Mkuu wa kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Askofu Fredrick Shoo amepongeza hatua ya viongozi hao wa dini kuona umuhimu wa kukutana na kujadiliana namna wanaweza kushiriki katika utetezi wa haki za Binadamu katika nafasi walizonazo katika jamii na kanisa.
“Viongozi wa dini ni wadau wakubwa wa maendeleo katika nchi yetu, kupitia taasisi zetu tunaendesha sehemu kubwa ya utoaji wa huduma za jamii hapa nchini, hii sio siri sisi ni wadau wakubwa maendeleo ya nchi hii,taasisi za dini ni walezi wa jamii kupitia imani na mafundisho ya imani ambayo msingi wake ni ulinzi na uendelezaji wa utu wa mtu,” amesema na kuongeza
“Kuna kipindi kutaja suala haki ilikuwa ni jambo gumu,sisi wenyewe tuwe Watetezi wa haki, tuzingatie haki za msingi za kila mwanadamu, ni kama ibilisi amefunga midomo ya watanzania tusitaje neno haki, tunataja upendo na Amani peke yake lakini tunahitaji kuongeza haki kwa sababu haki, ni jambo la msingi, pasipo haki hakuna Amani, Amani ni Tunda la Haki,” amesema Askofu Shoo.
Kwa Upande wake Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Sheikh Shaban mlewa amepongeza jitahada hizo zilizochukuliwa na viongozi wa dini katika kujifunza namna mbali mbali za kushiriki katika utetezi wa haki za binadamu.
“Ni vyema tukajua wajibu wetu wa sasa ni kuijenga jamii na kuikumbusha kuzingatia haki, ni wajibu wa kila kiongozi kuwa na huruma, kuwa na Imani thabiti, kuonyesha upendo na haki yenyewe ambayo ndio msingi wa yote hayo. Kusema kunaweza kusikilizwa na yoyote, lakini utendaji unaweza ukafuatiliwa na wengi, tunaweza kusema lakini tukafuatiliwa tunatenda kama tunavyoamrisha?, mara nyingi tuhamasishe tunayotenda ikiwemo kutenda haki ambayo ni wajibu wetu” amesema Sheikh Mlewa
Kwa upande wake Mtoa mada katika mkutano huo ambaye ni Mratibu kitaifa wa mtandao wa Watetezi wa haki za binadamu Tanzania THRDC, Onesmo Olengurumwa amepongeza hatua ya viongozi wa dini kuona umuhimu wa kujadiliana na kuongeza ujuzi katika uzingaatiaji wa Maswala ya Haki ambayo ni msingi wa Amani n aupendo kwa jamii.
More Stories
Dkt.Tulia ashiriki ibada, asisitiza waumini kushiriki uchaguzi serikali za mitaa
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia