Na Ashura Jumapili, TimesMajira Online, Kagera
Viongizi mbalimbali wa dini wametakiwa kuisaidia serikali kupitia mafundisho ya dini kubadilisha Jamii kuacha kushiriki vitendo vya mauaji na ukatili kwa wanawake na watoto.
Hayo yamesemwa na Askofu wa Kanisa la Carivary Assembly of God Jimbo la Kagera A, Damian Rwabutukura katika ibada ya kuwasimika wachungaji waliomaliza mafunzo ya kichungaji katika Kanisa la Bihabo lililopo Wilaya Kyerwa mkoani Kagera.
Askofu Rwabutukura, amesema serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawategemea viongozi wa dini kuibadilisha jamii kuachana na tabia za kujichukulia sheria mkononi.
“Ninyi mmepewa majukumu hayo, Mungu amewaamini, serikali imewaamini na Kanisa linawaamini, mwende mkafanye kazi hiyo ya kuibadilisha jamii ili kuachana na tabia za uvunjifu wa Sheria kwa kutenda matendo maovu ambayo kidini hayakubaliki,Jamii ya Watanzania inatakiwa kujifunza kutoka kwenu, hakuna namna ya kukwepa jukumu hilo kama wachungaji ambao mmeaminiwa,” anasema.
Anasema wachungaji hao wamethibitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa na Halmashauri Kuu ya Jimbo baada ya kuonekana wana sifa ya kuwa wachungaji tangu 2018 lakini wanatakiwa kutambua kuwa kazi ya uchungaji ni ngumu kwa sababu siyo rahisi kukibadilisha kizazi ambacho kimepinda ambacho kinafurahia dhambi kuliko utakatifu, kinachoona wokovu ni kitu kigumu, sio kazi rahisi.
Pia aliwataka wachungaji kuibadilisha jamii kuachana na uzinzi unaopelekea wanawake kutoa mimba na kusababisha mauaji ya watoto lakini wakati huo wanaume kuwaua wake zao pale wanapowafumania.
“Uzinzi unaosababisha wivu wa mapenzi umekuwa miongoni mwa sababu kubwa zinazosababisha mauaji katika Jamii na kumekua na matukio mengi ya namna hiyo”anasema.
Wakati huo huo Askofu Rwabutukura,anasema serikali inawategemea wachungaji kwenda kuhamasisha Jamii kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa ya watu na makazi ili kuhakikisha wanahesabiwa na kujulikana idadi ili serikali iweze kuwahudumia.
“Kuna watu wana tabia ya kupuuza wakiamini kuwa serikali ina nia mbaya inapotangaza suala la sensa ya watu na makazi lakini wanasahau kuwa hata nyumbani kwako unapopika chakula cha Watu watano wakala 10 hawawezi kushiba.
Hivyo ili serikali itoe huduma stahiki kwa Jamii inatakiwa kujua ina watu wangapi. Kwa kuwa mmeaminiwa mnatakiwa mkaihamasishe Jamii iweze kushiriki kikamilifu katika kuhesabiwa.”
Askofu Rwabutukura aliwataka waumini kuachana na imani potofu ya kuamini kuwa watu wakihesabiwa wanakufa kwa kuwauliza waumini hao kuwa, “hivi siku ambazo hakuna zoezi la sensa na watu hawahesabiwi je watu hawafi? Sasa unaunganishaje swala la kufa na sensa?”
Pia Jamii inatakiwa kuzingatia kila mtu anahesabiwa kwa sababu Kumekuwepo na kasumba ya watu wanaowaficha watu wenye ulemavu kwa kisingizio kuwa hawatakiwi kujulikana kwenye Jamii kwa kuwa nimikosi.
Mchungaji Chrisostom Ndamukama wa Kanisa la Carivary Assembly of God Nkwenda wilayani Kyerwa ni miongoni mwa wachungaji waliosimikwa anasema Kanisa limekuwa likishirikiana na serikali katika kuihudumia jamii hivyo maagizo waliyopewa na Askofu Rwabutukura wanaenda kuyatekeleza.
Jukumu la kuielimisha na kuihamasisha Jamii hatuwezi kulikwepa hivyo tunaenda kuondoa imani potofu kwa waumini wetu.
Sensa ni jambo la maendeleo kwa Jamii ili serikali iweze kutujua idadi na kuweza kutuhudumia kikamilifu.
Na kuhusu mauaji aliwaomba wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kuthaminiana na kusamehe pale wanapokosena.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa