Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
MKATABA wa Uwekezaji wa Bandari umewaibua viongozi wa dini Mkoa wa Mwanza wakishauri Watanzania, madhehebu ya dini,vyama vya siasa na taasisi mbalimbali kulinda na kuitunza amani ya nchi na kuonya,ikitoweka hakuna atakayebaki salama.
Wameishauri serikali kuandaa kongamano na kukutana na viongozi wa dini Kanda ya Ziwa ili kuwapa uelewa zaidi wa mkataba huo wa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii katika kuboresha bandari kati ya Serikali ya Dubai kupitia kampuni ya DP World na iendelee kuwaelimisha wananchi uwekezaji huo.
Pia wamekemea tabia ya watu wachache wanaombeza ,kumdhihaki na kumdharau Rais Samia Suluhu Hassan,watambue kufanya hivyo wanaharibu sifa na nembo ya Tanzania kwa kuwa mamlaka zote duniani huwekwa na Mungu.
Hayo yalielezwa kwa nyakati tofauti, leo jijini humu na wenyeviti wenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza, Askofu Dk.Charles Sekelwa na Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke,wakati wakitoa tamko kwa niaba ya kamati hiyo kuhusu mjadala wa Uwekezaji wa Kampuni ya DP World.
Askofu Dk.Sekelwa amesema kamati hiyo ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Mwanza, imebaini mjadala unaondelea nchini wa Uwekezaji wa Bandari ni kiashiria cha uvunjifu wa amani ya nchi.
Amesema uwekezaji na uendeshaji wa bandari unawahusu Watanzania wote na kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake na kuheshimiwa,hivyo katika masuala ya kitalaamu na ya kiutawala, maoni na ushauri wa kitaalamu sharti ufuatwe na kuheshimiwa.
“Watanzania wote kupitia dini (madhehebu), vyama vya siasa na taasisi zetu mbalimbali,tuendelee kuilinda na kuitunza amani ya nchi yetu kwani ikitoweka hakuna atakayebaki salama,si viongozi wa dini,kisiasa wala wa serikali,” amesema Dk.Askofu Sekelwa.
Amesema viongozi hao wanatambua serikali yetu haina dini lakini wananchi wanazo dini na imani zao zinaheshimiwa, pia nchi inayo mihimili yake Bunge,Mahakama na Serikali nayo inapaswa kuheshimiwa.
“Uwekezaji wa bandari Bunge limeshajadili na kupitisha mkataba huo kwa niaba ya wananchi,hivyo uheshimiwe,baadhi ya Watanzania walitumia haki yao kupinga mahakamani jambo hilo na Mahakama yenye kutafsiri sheria iliona liko sahihi,”amesema Askofu Dk.Sekelwa na kuhoji;
“Tujiulize, serikali yetu inaongozwa kwa matamko na ustashi wa mtu,kundi ama taasisi fulani na je,taasisi zetu zipo kuitisha serikali? tunapaswa kuishauri na kuiombea,uwepo wa vyama vingi vya siasa ni uamuzi wa wachache wakiwemo viongozi wa wakati huo lakini tulikubali na changamoto zinapotokea tunashughulikia maisha yanaendele,”.
Kwa upande wake Sheikhe Hasani Kabeke amesifu na kumpongeza Rais Samia kwa uvumilivu wake, anavyowakusanya Watanazania katika amani na utulivu na kushiriki masuala ya dini zote huku akiwataka wanaopinga mkataba wa uwekezaji wa bandari waoneshe upungufu ulipo.
“Sisi Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini ni grisi ya kulainisha vyuma vinapokaza vifanye kazi, wanaopinga na walioukubali uwekezaji ni kutu,kikubwa tunataka nchi yetu iendelee kuwa ya amani, yanayofanyika yanafanyika katika chombo kiitwacho Tanzania iliyo mama na mbeleko yetu,ikichanika hakuna atakayefanya dini,siasa wala kitu chochote, tutaumia wote na wapo watakaopoteza zaidi ”ameonya.
Sheikhe Kabeke amesema katika mitandao ya kijamii inaonesha watu walivyoparaganyika kuhusu suala la bandari,serikali na wanasheria waelimishe wananchi kwa kuwa hawana uelewa wa sheria, pia maoni ya watu yasibezwe wala yasizungumzwe kwa mzaha na kuleta kero.
“Turudi kwenye mazungumzo, maoni ya wananchi serikali iyaheshimu, mahakama pia imetoa haki lakini bado yanaendelea, yote yaheshimiwe na serikali iendelee kutoa elimu na kuheshimu nembo zetu akiwemo Rais Samia,watu wanadhani kadondoka la hasha!alichaguliwa akiwa mgombea mwenza, hivyo kumbeza, kumdharau na kumdhihaki ni kuharibu sura ya Tanzania,”amesema .
Sheikhe huyo wa Mkoa wa Mwanza amesistiza viongozi wa dini wana nafasi ya kuhakikisha nchi inadumu katika amani, hivyo serikali iendelee kufanyia kazi mapungufu yaliyopo katika mkataba wa uwekezaji wa bandari na sharti tutumie gharama turudi katika mstari ili kutunza na kulinda amani ya nchi.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba